Deutsche Welle yazinduwa jukwaa la kimataifa la vyombo habari | Masuala ya Jamii | DW | 20.06.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Deutsche Welle yazinduwa jukwaa la kimataifa la vyombo habari

Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Vyombo vya Habari linaloandaliwa na Deutsche Welle, umeanza mchana wa leo hii (20.06.2011) hapa mjini Bonn, huku msisitizo ukiwa dhima ya vyombo vya habari katika haki za binaadamu.

Mkurugenzi Mkuu wa Deutsche Welle, Erik Bettermann, akifungua mkutano huo

Mkurugenzi Mkuu wa Deutsche Welle, Erik Bettermann, akifungua mkutano huo

Mkutano huu wa siku tatu umefunguliwa na mkurugenzi mkuu wa Deutsche Welle, Erik Bettermann, ambaye ametumia taswira ya harakati za mageuzi katika ulimwengu wa Kiarabu, kuuita mwaka huu kuwa ni "mwaka wa haki za binaadamu".

Akiwahutubia mamia ya washiriki kutoka kila kona ya dunia na Betterman amesema kuwa, ni lazima kwa tasnia ya habari ulimwenguni kuendelea kubeba jukumu kubwa na la kipekee katika masuala ya haki za binaadamu na demokrasia.

"Mara zote nimekuwa nikisema tunapaswa kushajiisha ushiriki wa watu katika maendeleo yote. Kuendeleza demokrasia, na ujenzi wa demokrasia unatokana na utayarifu wa jamii, vikiwemo vyombo vya habari, kuwekeza kwenye mchakato huo, ikiwa ni pamoja na kupambana na ufisadi katika nchi husika.” Amesema Bettermann.

Takribani wajumbe wapatao 300 wanashiriki mkutano huu kutokea Afrika, Ulaya, Amerika na Asia. Chini ya kivuli cha mada kuu ya changamoto linalovikabili vyombo vya habari katika ulimwengu huu wa utandawazi, mada kadhaa zinawasilishwa na kujadiliwa kwa kina na wataalamu na watu wenye uzoefu wa masuala ya habari na utandawazi ulimwenguni.

Wajumbe wa mkutano wa jukwaa la kimataifa la vyombo vya habari mjini Bonn

Wajumbe wa mkutano wa jukwaa la kimataifa la vyombo vya habari mjini Bonn

Miongoni mwa mada zilizowasilishwa na kujadiliwa hii leo, ni pamoja na biashara harumu ya kusafirisha watu kama uhalifu wa kimataifa, haki ya watu kupata maji safi na salama, haki ya elimu na chakula na changamoto za vyombo vipya vya habari vinavyotumia mtandao wa kompyuta.

Mada nyengine muhimu ni mpishano na mfanano wa habari za nchi masikini zinavyoripotiwa kwenye vyombo vya habari vya kimataifa na pia uhusiano kati ya maendeleo na haki za binaadamu.

Mwandishi wa habari na mtaalamu wa mawasiliano kwa kutumia simu za mkononi, Olivier Nyirubugara kutoka Wakfu wa Voices of Africa, ni mmoja wa washiriki wa mkutano huu, ambaye anasema kuwa pana mahusiano makubwa na ya moja kwa moja kati ya haki za binaadamu na maendeleo, lakini taarifa zake zimekuwa hazipewi kipaumbele katika vyombo vya habari, barani Afrika.

Mkutano kama huu hufanyika kila mwaka, ambapo mada kuu ya mwaka uliopita ilikuwa dhima ya vyombo vya habari katika kutunza na kudumisha mazingira duniani.

Mwakilishi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo na Kiuchumi, Dunja Mijatović

Mwakilishi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo na Kiuchumi, Dunja Mijatović

Waandishi kadhaa kutoka ndani na nje ya bara la Afrika wamekuwa wakihudhuria jukwaa la vyombo vya habari hapa Bonn, kama sehemu ya mpango wa Deutsche Welle kusaidia mabadilishano ya mawazo kati ya nchi za Kusini na Kaskazini.

Miongoni mwa waandishi wapya wanaoshiriki mkutano wa mara hii ni Jacob Mugiri Mwera, mwandishi wa habari wa gazeti la serikali ya Tanzania, Daily News, ambaye anashiriki mkutano huu kwa mara ya kwanza.

Mugiri anasema kwamba amejifunza nguvu na nafasi ya simu za mkononi katika ujenzi wa demokrasia wa haki za binaadamu.

Mkutano huu utaendelea tena hapo kesho, ambapo pamoja na mengine, utajadili uhuru wa vyombo vya habari katika taifa jipya linalotarajiwa kuzaliwa Afrika, Sudan ya Kusini na mashambulizi kupitia mitandao ya kompyuta.

Mada zinazotarajiwa kuwavuta washiriki wengi ni ile ya wanawake kama wahanga wa mapigano na mustakabali wa vyombo vya habari katika ulimwengu wa Kiarabu, hasa baada ya vyombo vipya vya mawasiliano kupitia mtandao wa kompyuta kuchukuwa nafasi kubwa kwenye harakati za mageuzi katika eneo hilo.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Saumu Mwasimba

Sauti na Vidio Kuhusu Mada

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com