Bunge la Ulaya laonyesha musuli zake | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.02.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Bunge la Ulaya laonyesha musuli zake

Hiyo jana Bunge la Ulaya lilifanikiwa kubatilisha makubaliano yaliyoiruhusu Marekani kujipatia data za benki za mamilioni ya wakaazi wa Ulaya kwa kupitia mfumo wa SWIFT unaotumiwa kutuma pesa kati ya benki.

The plenary room of the European Parliament in Strasbourg, eastern France, is seen during the election of the new European Parliament’s president Jerzy Buzek of Poland, Tuesday, July 14, 2009. (AP Photo/Lionel Cironneau)

Bunge la Ulaya mjini Strasbourg.

Makubaliano hayo ya mpito, kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya,yalianza kuwa halali tarehe mosi mwezi huu wa Februari, lakini wabunge wa Ulaya walio na haki zaidi tangu Mkataba wa Lisbon ulipoanza kufanya kazi Desemba iliyopita,wamedhihirisha kuwa wao pia wanapaswa kushirikishwa katika maamuzi ya kisiasa. Wabunge wa Ulaya walikuwa na haki ya kufurahi, kwani kufanikiwa kubatilisha makubaliano ya Swift yaliyokwishaanza kufanya kazi ni tukio muhimu. Wao waliitumia fursa kuu ya kwanza waliyopata, kuonyesha musuli zao katika mfumo mpya wa Umoja wa Ulaya. Wengi wao wanaamini kuwa miaka iliyopita haikuridhisha na imechukua muda mrefu mno kuleta mageuzi katika Umoja wa Ulaya. Maoni yao yalikuwa yakizingatiwa, lakini uamuzi wa masuala muhimu, ulipitishwa katika baraza linalowakilisha serikali za nchi wanachama. Utaratibu huo haupo tena - kwani tangu Mkataba wa Lisbon ulipoanza kufanya kazi tarehe mosi Desemba mwaka 2009, wabunge wa Ulaya pia wanaruhusiwa kuwa na usemi kuamua mambo pamoja na nchi zisizo katika umoja huo. Makubaliano ya Swift ni mtihani mkuu wa kwanza wa Bunge la Ulaya kwani huo ni uamuzi muhimu wa kwanza kupitishwa kuambatana na kanuni za Mkataba wa Lisbon. Je, mwaka jana ilisadif tu kwa baraza la mawaziri la Umoja wa Ulaya kukamilisha makubaliano ya Swift siku moja kabla ya Mkataba wa Lisbon kuanza kufanya kazi? Wala haishangazi kuwa Bunge la Ulaya lilikasirishwa. Hata hivyo, si kisasi au ari iliyowafanya wabunge hao wa Ulaya kubatilisha makubaliano ya Swift bali ni shaka zao zinazohusika na baadhi ya masuala muhimu: vita dhidi ya ugaidi,hifadhi ya data na haki za kiraia. Lakini, kilicho muhimu kabisa ni kuwa kwa kuyakataa makubaliano ya Swift, Ulaya imebainisha mbele ya mshirika mwenye nguvu Marekani, kuwa maoni ya Umoja wa Ulaya kuhusu ulinzi wa data yanatofautina na yale ya Marekani licha ya shinikizo la wanadiplomasia wa Marekani. Kwani katika suala la haki ya kimsingi ya wananchi wa Umoja wa Ulaya wapatao kama milioni 500, waakilishi wa umma huo hawapastahiki kuafikiana. Shaka za wabunge hao zinaeleweka,kwani kuna masuala mengi yanayohitaji kutenzuliwa. Kwa mfano kuna hakika gani kuwa habari zilizokusanywa na Marekani hazitopelekwa kwa serikali nyingine: data hizo zitahifadhiwa kwa muda gani na raia alieathirika ataweza kuchukuwa hatua gani ili kupinga data zake kupelekwa kwengine? Masuala hayo na mengine pia yanapaswa kujadiliwa upya kwa kina ili yapatikane makubaliano mapya yalio bora. Zikipenda zisipende, serikali za pande zote mbili yaani Ulaya na Marekani, hazina budi kujadiliana upya. Kwa hivyo, kukataliwa makubaliano ya Swift sio tu tukio muhimu bali ni sahihi pia. Mwandishi:Henn,Susanne Mhariri: Abdul-Rahman
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com