Boti ya wanaharakati wa Kiyahudi yaelekea Gaza | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.09.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Boti ya wanaharakati wa Kiyahudi yaelekea Gaza

Boti ya misaada ikiwa na wanaharakati wa Kiyahudi kutoka Israel, Ulaya na Marekani iko njiani kuelekea Ukanda wa Gaza likitokea Cyprus ya Uturuki kuvunja ulinzi mkali wa Israel na hatua yake ya kulizingira eneo hilo

Afisa wa usalama wa Israel akilinda bidhaa katika kivuko cha Kerem Shalom kwenye mpaka kati ya Gaza na Israeli. Boti ya Wayahudi iko njiani kuelekea Gaza

Afisa wa usalama wa Israel akilinda bidhaa katika kivuko cha Kerem Shalom kwenye mpaka kati ya Gaza na Israeli. Boti ya Wayahudi iko njiani kuelekea Gaza

Boti iliyopewa jina "Irene" iliondoka kutoka bandari ya Famagusta, kaskazini mwa kisiwa cha Cyprus inayomilikiwa na Uturuki, ikiwa ndani na wanaharakati 10. Reuven Moskovitz, mwenye umri wa miaka 82, aliyepona kutokana na mauaji ya Wayahudi yaliyofanywa na Manazi wa Ujerumani, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa anahisi ana jukumu la kufanya safari ndani ya boti hilo inayotarajiwa kudumu takriban saa 36. Moskovitz amesema, "Ni jukumu takatifu kwangu kuwalinda watu dhidi ya mateso, uonevu na kufungwa kwa watu wengi wa Gaza, wakiwemo watoto 800,000."

Waziri wa ulinzi wa Israel, Ehud Barak, ameonya mara kwa mara kwamba Israel itaizuia meli yoyote itakayokaribia Gaza. Yonatan Shapira, rubani wa zamani wa jeshi la Israel ambaye pia yumo ndani ya boti ya Irene amesema hawataki mapambano na Israel, akisema sera yao ni kutotumia nguvu. Hata hivyo amesema ikiwa wanajeshi wa Israel wataisimamisha boti hiyo, hawatawasaidia kulipeleka katika bandari ya Ashdod.

Wanaharakati wa boti ya Irene wanapanga kupeperusha bendera za rangi mbalimbali zenye madarzeni ya majina ya Wayahudi wanaounga mkono juhudi yao wakati chombo hicho kitakapokaribia Gaza. Misaada iliyo ndani ya boti hiyo ni pamoja na vitu vya kuchezea vya watoto, vifaa vya muziki, vitabu, nyavu za kuvulia samaki kwa jamii za wavuvi wa Gaza na miguu bandia kwa wale waliopoteza miguu katika hospitali za Gaza.

Richard Kupper, mwanachama wa kundi lililoandaa safari hiyo amesema boti hiyo ya Wayahudi ni ishara ya kupinga hatua ya Israel kuyakalia maeneo ya Wapalestina na kuuzingira Ukanda wa Gaza. Kupper aidha amesema ni ujumbe wa mshikamano kwa Wapalestina na Waisraeli wanaotaka amani na haki.

Wakati huo huo, polisi nchini Ugiriki wanasema msafara wa magari ya misaada yakiwa na wanaharakati 40 wa kundi la Viva Palestina, wameondoka leo katika mji wa Alexandroupolis, nchini Ugiriki kuelekea Gaza. Msafara huo unajumulisha motokaa, mabasi madogo na magari ya kubebea wagonjwa, yaliyotundikwa bendera za Palestina wakati ulipokuwa njiani kuelekea mji wa Istanbul nchini Uturuki, ambako unatarajiwa kuwasili baadaye leo. Msafara huo baadaye utaelekea Mashariki ya Kati na wanaharakati wana matumaini ya kuingia Ukanda wa Gaza kupitia kivuko cha mpakani na Misri cha Rafah.

Shirika la Viva Palestina limesema kwenye tovuti yake kwenye mtandao wa intaneti kwamba msafara huo ulianza safari yake mjini London, Uingereza mnamo tarehe 12 mwezi huu, kupitia Lyon Ufaransa na Milan, Italia na kuelekea nchini Ugiriki, ambako ulisimama kwa muda mjini Salonica, Jumamosi iliyopita.

Shirika hilo lililoasisiwa na mbunge wa Uingereza, Georges Galloway, mpinzani mkali wa vita dhidi ya Irak, tayari limeshaandaa misafara mitatu katika miezi 18 iliyopita kuelekea Gaza.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 • Tarehe 27.09.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PNqb
 • Tarehe 27.09.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PNqb
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com