Baadhi ya safari zarejea katika bara la Ulaya | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.04.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Baadhi ya safari zarejea katika bara la Ulaya

Viwanja vya ndege katika bara la Ulaya taratibu vimeanza kurejea katika hali ya kawaida leo Jumanne baada ya siku tano za kutokuwa na mawasiliano na maeneo mengine duniani.

Lava kutoka katika volcano ikimwagika katika mlima wakati ilipolipuka.

Lava kutoka katika volcano ikimwagika katika mlima wakati ilipolipuka.

Viwanja vya ndege katika bara la Ulaya taratibu vimeanza kurejea katika hali ya kawaida leo Jumanne baada ya siku tano za kutokuwa na mawasiliano hayo ya safari za anga na maeneo mengine duniani kutokana na wingu kubwa la majivu , lakini baadhi ya anga zimeendelea kufungwa baada ya ripoti za wingu jingine jipya la majivu kutoka Iceland kwamba huenda liko njiani.

Italia, Uswisi na Ufaransa zimefungua viwanja vyao vya ndege mapema leo Jumanne licha ya kuwa safari nyingi zimeendelea kufutwa, na nchini Italia ni safari chache tu zilizoruhusiwa asubuhi ya leo, nyingi zikiwa ni za ndani. Hungary, Slovenia na Moldova pia zimeanza tena kuruhusu safari za anga.

Lakini mamlaka ya taifa ya usafiri wa anga nchini Uingereza , ambayo inadhibiti anga la nchi hiyo , imesema sehemu kubwa ya anga la nchi hiyo litaendelea kufungwa kwa safari za ndege zinazoruka umbali wa futi 20,000 juu ya usawa wa bahari hadi majira ya saa za jioni leo baada ya wadhibiti wa safari za anga kuonya kuwa wingu jingine la majivu linaelekea katika maeneo ya njia kuu zinazopita ndege.

Umoja wa Ulaya ambao umesema jana Jumatatu kuwa mataifa wanachama yamefikia makubaliano kupunguza eneo lililopigwa marufuku kuruka ndege kuanzia saa mbili leo asubuhi saa za Ulaya ya kati, umekiri kuwa hatua za maendeleo zimekuwa za taratibu mno.

Tunafahamu kuwa kuna matatizo mengi kwa wasafiri , msemaji wa halmashauri ya umoja wa Ulaya Helen Kearns amewaambia waandishi habari. Tunakabiliwa na mzozo mkubwa , na hali hii ya kuvurugika kwa safari itaendelea hadi mwishoni mwa wiki hii. Joachim Hunold mwenyekiti wa shirika la ndege la Air Berlin anamatumaini kuwa safari za usiku zitaruhusiwa ili kuweza kurejesha hali ya usafiri katika hali ya kawaida.

Tunazungumzia hapa kipindi cha mpito. Ambacho ni muhimu kuweza kurejea katika hali ya kawaida, kwasababu umuhimu unatiliwa wasafiri kwanza, ambao wamekwama duniani kote, na tunatakiwa kuwasafirisha. Tunaweza kufanya hivyo kwa kuwa na wafanyakazi wengi wa kubadilishana na hii itawezekana kufanyika nyakati za usiku tu.

Ujerumani imesema kuwa itaendelea na marufuku ya kutorusha ndege hadi saa mbili usiku leo, leo, isipokuwa kwa safari maalum.

Finland na sehemu za Sweden na Norway pia zimefunga anga zao. Chini ya makubaliano ya jana ya mawaziri wa usafirishaji wa umoja wa Ulaya, ambayo yamepatikana kutokana na mbinyo mkubwa kutoka kwa mashirika ya ndege ambayo yanapoteza kiasi kinachokadiriwa kufikia dola milioni 250 kwa siku, safari huenda zikaruhusiwa katika maeneo ambayo wingu hilo la majivu halikufika kwa kiasi kikubwa, kwa mujibu wa tathmini za wataalamu wa eneo hilo na ushauri wa kisayansi.

Kufuka upya kwa majivu katika volcano nchini Iceland kumezusha mtafaruku mpya leo Jumanne, na kuvunja matumaini ya wasafiri waliokwama kurejea nyumbani haraka licha ya kufunguliwa kwa baadhi ya viwanja vikuu vya ndege barani Ulaya.

Wakati huo huo wingu hilo la majivu kutoka Iceland linatarajiwa kubadilisha mwelekeo na kuelekea katika eneo la Arctic wakati hali ya hewa itakapobadilika baadaye wiki hii, kutokana na mabadiliko ya upepo na mvua kunyesha, shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani limesema leo Jumanne.

Mwandishi : Sekione Kitojo /DPAE/AFPE/RTRE

Mhariri: Abdul-Rahman

 • Tarehe 20.04.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/N1JL
 • Tarehe 20.04.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/N1JL
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com