1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Askofu Tutu, awatahadharisha wagombea wa nafasi ya uongozi wa ANC:

Halima Nyanza14 Desemba 2007

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Desmond Tutu, amewaambia, washindani wawili katika uongozi wa juu wa Chama Tawalai, Rais Mbeki na mwenzie Jacob Zuma, kuwa nchi hiyo inahitaji viongozi wenye kujali maslahi ya watu.

https://p.dw.com/p/CbsY
Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Askofu Desmond Tutu wa Afrika kusini.Picha: picture alliance / dpa

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, nchini Afrika Kusini, Askofu Desmond Tutu amewataja Rais wa nchi hiyo Thabo Mbeki na Makamu wa rais wa zamani Jacob Zuma kuwa watu wanaoweza kuistawisha au kuififisha nchi hiyo.

Askofu Tutu amesisitiza kuwa taifa hilo linahitaji kiongozi ambaye ni mpenda watu, anayesikiliza mawazo na kujenga umoja wa kitaifa, hasa katika wakati huu ambao Afrika Kusini iko katika kipindi kigumu kisiasa.

Kauli ya mshindi huyo wa tuzo ya Nobel, imekuja wakati ambapo wajumbe wa chama tawala cha ANC wanakutana siku ya Jumapili kwenye mkutano unaolenga kusawazisha tofauti zilizopo kati ya Rais Thabo Mbeki na aliyekuwa makamu wake Jacob Zuma ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa chama tawala.

Askofu Tutu aliyekuwa mstari wa mbele kupiga vita ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, hafurahishwi na misimamo ya wanasiasa hao wawili, yaani Rais Thabo Mbeki na Jacob Zuma kwa kuwa wamebeba dhamana ya wananchi.

Desmond Tutu amekaririwa akisema kwamba anaongea akiwa ni mtu wa kawaida asiye na mwelekeo wowote kwa chama cha ANC, na pia akaongeza kuwa kashfa iliyokuwa ikimkabili Jacob Zuma ya ubakaji ni kitendo cha fedheha na kinachodhalilisha.

Tutu amefafanua kuwa kashfa hiyo ya Zuma inaleta maswali mengi, kwa wachambuzi wa mambo na kunaweza kuleta athari kubwa, katika chama cha ANC na serikali kwa ujumla.

Akimgeukia Rais Thabo Mbeki, Askofu Desmond Tutu, amesema kiongozi huyo amekuwa na msimamo wa kutokubali kupingwa kwa namna yoyote, na pale anapopingwa anakuwa mkali.

Akikumbushia enzi za ubaguzi wa rangi Askofu Tutu, amesema wakati huo hapakuwa na mtu wa kusema kitu au kunyosha kidole dhidi ya utawala wa kidhalimu wa makaburu, lakini sasa wakati huu ni wa demokrasia na kila mtu ana haki ya kutoa mawazo yake bila kuvunja sheria za nchi.

Desmond Tutu aliyewahi kuwa Askofu wa Jimbo la Cape Town amewataka viongozi wote wa siasa kufuata nyendo za Rais wa kwanza wa Afrika Kusini Huru Mzee Nelson Mandela, kwa kuwa aliifanya demokrasia kuwa haki ya kila raia.

Pamoja na kashfa zote zilizokuwa zikimkabili Jacob Zuma, wiki hii anatarajia kuchukua uanyekiti wa chama cha African National Congress na ikiwa mambo yatamwendea vizuri, ataweza kujinga katika kinyang’anyiro cha urais baada ya Rais Thabo Mbeki kumaliza kipindi chake hapo mwaka 2009.

Watu wengi hasa masikini nchini Afrika Kusini wameweka matumaini yao kwa Zuma kwa madai kwamba amekuwa karibu na wananchi siku zote, licha ya kashfa za hapa na pale, kitu wanachokieleza kuwa moja ya udhaifu wa kila binadamu.

Ikiwa Zuma atakuwa mwenyekiti kamili wa chama cha ANC, atakuwa kiongozi wa kwanza kugombea nafasi ya urais akiwa na umri mdogo wa miaka 65.

Jacob Zuma alijiunga na chama cha ANC, ambapo mwaka 1963 alifungwa katika gereza lililoko kwenye kisiwa cha Robben, baada ya kuratibu mapinduzi dhidi ya serikali ya kibaguzi.

Baada ya miaka 10 gerezani Zuma, alikwenda kuishi uhamishoni, katika nchi za Msumbiji, Swaziland na Zambia kwa kipindi cha miaka 12 akiwa mkuu wa masuala ya usalama wa chama cha ANC.

Mwaka 1990, Jacob Zuma alirejea nchini Afrika Kusini baada ya kukomesha ubaguzi wa rangi, na akawa miongoni mwa maofisa waliokuwa wakipanga mkakati wa kuunda umoja wa kitaifa miongoni mwa weusi na wazungu walowezi.

Katika serikali ya Rais Nelson Mandela, Jacob Zuma alipewa nafasi ya uwaziri wa uchumi akiwakilisha jimbo la KwaZulu Natal, kabla ya kuwa Makamu wa Rais mwaka 1999 na kuondolewa madarakani mwaka 2005.