Amerika Kusini yaongoza juhudi za kuyafikia malengo ya milenia ya Umoja wa Mataifa | Masuala ya Jamii | DW | 04.07.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Amerika Kusini yaongoza juhudi za kuyafikia malengo ya milenia ya Umoja wa Mataifa

Kwa mujibu wa ripito ya Umoja wa Mataifa, Amerika Kusini inaongoza nchi zinazoendelea kuhusiana na takwimu zinazonyesha maendeleo katika kuyafikia malengo ya milenia ya Umoja wa Mataifa. Hata hivyo eneo hilo linafeli katika lengo moja muhimu la kupunguza kwa asilimia hamsini idadi ya watu wanaoishi katika umasikini uliokithiri.

Mama na mtoto wake wakiishi katika hali ngumu ya umaskini

Mama na mtoto wake wakiishi katika hali ngumu ya umaskini

Idadi ya watu wanaoishi chini ya dola moja ya kimarekani kwa siku katika Amerika Kusini ilishuka kutoka asilimia 10.3 hadi asilimia 8.7 kati ya mwaka wa 1990 na mwaka wa 2004. Kiwango hiki ni kidogo mno kuliwezesha eneo hilo kuwa katika njia ya kuelekea kulifikia lengo la milenia la Umoja wa Mataifa la kupunguza umaskini kufikia mwaka wa 2015.

Kuhusu kugawa utajiri hali pia si nzuri kwa sababu kiwango cha utajiri kinachowafikia watu walio maskini kilishuka kutoka asilimia 2.8 hadi asilimia 2.7.

Haya ni baadhi ya matokeo ya ripoti juu ya malengo ya milenia ya Umoja wa Mataifa ya mwaka huu wa 2007 iliyotolewa Jumatatu wiki hii na Umoja wa Mataifa. Ripoti hiyo inahusu takwimu za mwaka wa 2004 zilizokusanywa na mashirika zaidi ya 20 ndani na nje ya Umoja wa Mataifa.

Takwimu za mwaka jana zilizokusanywa na waandishi wa habari wa shirika la habari la IPS katika nchi kadhaa, zinaonyesha kuwa Amerika Kusini inaendelea kuvuta mkia katika juhudi za kupambana na umaskini. Pamoja na hayo wataalamu waliohojiwa walielezea wasiwasi wao kuhusu data zinazoonyesha ufanisi kidogo na kutilia shaka utendaji wa serikali katika mipango ya kupunguza umaskini.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa idadi ya watu wanaoishi chini ya kiwango cha dola moja kwa siku katika nchi zinazoendelea ilipungua kwa asilimia 11.7 kutoka asilimia 31.6 hadi asilimia 19.9. kati ya mwaka wa 1990 hadi mwaka 2004.

Na ingawa Amerika Kusini na eneo la Karibik zina idadi ndogo ya watu maskini kuliko maeneo mengine yanayoendelea duniani, kupungua kwa idadi ya watu wanaoishi katika umaskini ilikuwa asilimia 1.6.

Lengo la kwanza miongoni mwa malengo manane ya milenia yaliyoidhinishwa na jamii ya kimataifa mnamo mwaka wa 2000, ni kupunguza kwa nusu idadi ya watu wanaoteseka na umaskini na njaa kufikia mwaka wa 2015 kutoka kwa viwango vya mwaka wa 1990.

Malengo mengine ni kuhakikisha elimu ya msingi, kuendeleza usawa wa kijinsia na afya ya uzazi, kupunguza vifo vya watoto, kupambana na ugonjwa wa ukimwi, malaria na magonjwa mengine, kuhakikisha mazingira yanalindwa na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo.

Idadi ya watoto wanaokwenda shule katika Amerika Kusini na eneo la Karibik iliongezeka kutoka asilimia 87 hadi asilimia 97 kati ya mwaka wa 1990 na 2005 huku idadi ya wanawake walioajiriwa katika sekta nyengine mbali na kilimo ikaongezeka kutoka asilimia 37 hadi asilimia 42 katika kipindi hicho.

Ripoti hiyo inasema wanawake walipiga hatua katika maswala ya kisiasa, huku idadi ya wanawake wanaoshikilia viti bungeni ikiongezeka kufikia asilimia 20 mwaka huu kutoka asilimia 12 mnamo mwaka wa 1990.

Katika sekta ya afya ripoti hiyo ilisema nchi za Amerika Kusini zilipiga hatua kubwa mbele kupunguza idadi ya vifo vya watoto kutoka vifo 54 katika kila watoto 1,000 waliozaliwa mwaka wa 1991 hadi vifo 31 kufikia mwaka wa 2005.

Kumekuwa pia na maendeleo mazuri katika utoaji wa huduma za matibabu kwa akina mama wajawazito ingawa bado kuna baadhi ya nchi masikini katika eneo hilo hasa Amerika ya Kati ambako huduma za matibabu bado ni mbaya.

Umoja wa Mataifa umeipongeza Amerika Kusini kwa ufanisi huo lakini umeonya kuwa juhudi za kuungamiza umaskini zinafanyika kwa mwendo wa kinyonga na kwamba kutokuwepo usawa bado ni tatizo kubwa Amerika Kusini, eneo la Karibik na barani Afrika ambako asilimia 20 ya watu maskini wanatumia asilimia tatu pekee ya pato zima la kitaifa.

 • Tarehe 04.07.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHkK
 • Tarehe 04.07.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHkK
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com