Al-Nusra Front washambulia makundi ya waasi Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Al-Nusra Front washambulia makundi ya waasi Syria

Kundi la wanamgambo ambalo awali lilikuwa na mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda limefanya mashambulizi dhidi ya makundi mengine ya wanamgambo ya Jeshi Huru la Syria, FSA, wanaoungwa mkono na nchi za Magharibi.

Kundi hilo la wanamgambo linalojulikana kama Levant Conquest Front na ambalo awali lilikuwa likijulikana kama Al-Nusra Front, jana lilifanya mashambulizi kadhaa kaskazini magharibi mwa Syria, eneo ambalo ni moja ya maeneo yanayoendesha mapambano dhidi ya Rais wa Syria, Bashar al-Assad.

Kundi hilo ambalo pia linajulikana kama Jabhat Fateh al-Sham, limeeleza katika taarifa yake kwamba limelazimika kufanya mashambulizi hayo kwa lengo la kuzuia njama zinazoendelea dhidi yake. Kundi hilo limesema mazungumzo na mikutano ilikuwa inajaribu kugeuza mwenendo mzima wa mapinduzi kuelekea maridhiano na serikali ya jinai ya Assad.

Kundi hilo lilikuwa likimaanisha mazungumzo ya amani ya Syria yaliyofanyika kwenye mji mkuu wa Kazakhstan, Astana.

Syrien Präsident Bashar al-Assad (picture alliance/AP Photo)

Rais wa Syria, Bashar al-Assad

Kundi la Levant Conquest Front halikualikwa katika mazungumzo hayo ambayo yalidhaminiwa na mshirika wa Rais Assad, Urusi pamoja na Uturuki na yaliungwa mkono na kundi la wanamgambo wa Jeshi Huru la Syria, FSA, ambalo linachukuliwa kama kundi kubwa la upinzani lenye msimamo wa wastani.

Likichukuliwa kama moja ya makundi ya waasi yenye nguvu nchini Syria, mwaka uliopita Al-Nusra Front lilitangaza kwamba limesitisha uhusiano wake na Al-Qaeda, licha ya kutokuwepo mabadiliko katika uongozi wake pamoja na muundo wote kwa ujumla. Kundi hilo kisha likabadili jina lake na kuanza kujiita Levant Conquest Front.

Makundi yalijiandaa kuungana

Kabla ya mashambulizi ya wiki hii magharibi ya Aleppo, makundi ya FSA, yalilikuwa yamejiandaa kuunganisha nguvu zao pamoja na Ahrar al-Sham, kundi jingine lenye itikadi kali za Kiislamu linalopambana katika jimbo la Idlib.

Hata hivyo, kundi la Ahrar al-Sham limelionya kundi la Levant Conquest Front kuhusu mashambulizi yake dhidi ya makundi pinzani kwenye eneo hilo, likilituhumu kwa kukakataa juhudi za upatanishi zenye lengo la kuyapatanisha makundi ya FSA na kundi lililokuwa na mafungamano na Al-Qaeda.

Syrien syrische Soldaten nach der Zurückeroberung von Aleppo (Getty Images/AFP/G. Ourfalian)

Eneo la Sukkari, Aleppo, linaloshikiliwa na waasi

Kundi la Ahrar al-Sham ambalo linajitambulisha lenyewe kama kundi lenye itikadi kali za Kiislamu kutoka madhehebu ya Sunni, linachukuliwa kama kundi la kigaidi na Urusi. Mashambulizi ya Fateh al-Sham yametishia kuyaondoa makundi ya FSA, ambayo yamekuwa yakiungwa mkono na nchi zinazoipinga serikali ya Assad kama vile Uturuki, Marekani na Ghuba ya Kiarabu.

Mkuu wa Ahrar al-Sham, Abu Ammar al-Omar, amesema iwapo mapigano yataendelea na kama upande mmoja utaendelea kufanya dhulma kwa mwingine, basi hawatoruhusu hilo lipite, bila ya kujali gharama yake, hata kama wakiwa wahanga wa jambo hilo.

Tangu mwaka 2011, makundi ya upinzani ya Syria, yaligawanyika kulingana na misimamo yao ya kiitikadi, huku upande mmoja ukichukuliwa kama wazalendo na upande mwingine kama unaofuata zaidi itikadi kali za Kiislamu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/Reuters, DW http://bit.ly/2k3pi1R
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com