Al-Maliki wa Iraq akasirishwa na matamshi ya waziri wa nje wa Ufaransa | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 27.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Al-Maliki wa Iraq akasirishwa na matamshi ya waziri wa nje wa Ufaransa

Bw Kouchner asema ameeleweka vibaya,lakini akitakiwa kuomba radhi atafanya hivyo kwamoyo mkunjufu.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Beranard Kouchner.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Beranard Kouchner.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Bernard Kouchner amesema leo kwamba atakua tayari kuomba radhi iwapo Waziri mkuu wa Iraq Nouri Al-Maliki anahisi ameingilia mambo ya ndani ya nchi yake. Wakati alipokuwa ziarani mjini Baghdad wiki iliopita. Bw Al-Maliki amemlaumu vikali Waziri huyo wa kigeni wa Ufaransa baada ya kutamka kwamba “serikali ya Irak haifanyi kazi na kuunga mkono maoni yanayotolewa na baadhi ya wanasiasa wan chi za magharibi kwamba, ingekua vyema kama Bw Al-Maliki

Katika mahojiano na Redio RTL ya Ufaransa Waziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi hiyo Bernard Kouchner alisema kwamba anahisi ameeleweka vibaya, au pengine hakuweza kufafanua vya kutosha, kwamba alikua akidokeza juu ya maoni anayoyasikia kutoka kwa Wairaki juu ya hali ya mambo ilivyo. Mbali na kusema kwamba serikali ya Irak haiwajibiki na kwamba ingekua vyema kama waziri mkuu Nouri Al-Maliki atan´gatuka, Bw Kouchner pia amenukuliwa kuwa alimwambia Waziri mwenzake wa Marekani Bibi Condoleeza Rice kwamba wazo hilo linaungwa mkono na wengi nchini Irak.

Sasa Bw Kouchner anasema kama Waziri mkuu Al-maliki atamtaka aombe aradhi, basi atafanya hivyo kwa moyo mkunjufu. Kouchner alikuweko mjini Baghdad kwa siku tatu wiki iliopita, akijaribu kuirudisha Ufaransa katika mjadala juu ya mustakbali wa Irak na pia kuboresha uhusiano na Marekani ulioingia dosari baada ya uvamizi wake 2003.

Katika ukurasa wa maoni yaliochapishwa toleo la leo la gazeti la International Herald Tribune, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa aliandika kwamba Ufaransa iko katika nafasi nzuri ya kusaidia kuleta hali mpya nchini Irak na kusisitiza kwamba hapana budi paundwe serikali pana zaidi ya umoja wa kitaifa na nchi yake iko tayari kuwa mpatanishi katika kufikia lengo hilo,

Kwa upande mwengine rais wa Ufaransa Nikolas Sarkozy naye ametoa wito wa pawekwe ratiba maalum ya kuondoka wanajeshi cwa kigeni nchini Irak. Katika hotuba yake ya kwanza kuhusu sera ya kigeni tangu aingie madarakani mwezi Mei, Sarkozy alisema hakuna suluhisho zaidi ya lile la kisiasa na hapana budi pawekwe ratiba ilio wazi juu ya kuondoka kwa majeshi ya kigeni. Akizungumza na mabalozi wa Ufaransa mjini Paris, Rais Sarkozy alisema ni uamuzi juu ya swala hilo la kuondoka majeshi ya kigeni, utakaowalazimisha wahusika ndani ya Irak kutathimini wajibu wao na kujipanga ipasavyo kusaka suluhisho.

Wakati hayo yakiendelea, viongozi wa makundi ya kisiasa nchini Irak leo walifikia makubaliano ya kushirikiana pamoja kuyatatua maswala ya msingi yanayozusha mvutano, huku wanasiasa wa Marekani wakizidi kutoa matamshi ya kushinikiza hatua zaidi aya maendeleo katika kuleta upatanishi wa kitaifa.

Viongozi hao wamekubaliana kulainisha misimamo yao kupinga wanachama wa chama tawala cha Baath cha kiongozi wa zamani Saddam Hussein kushika nyadhifa za serikali. Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Rais Jalal Talabani, viongozi hao wa makundi ya kisiasa pia wamekubaliana kuandaa chaguzi za mikoa ambalo ni takwa kuu la Marekani, na kuyasaidia majeshi ya usalama kuzuwia umwagaji damu.

Hali nchini Irak bado inazidi kuwa tete. Leo jeshi la Marekani liliriopoti kuuawa kwa wanajeshi wake wengine wanne, wawili leo hii katika mkoa wa Anbar baada ya mmoja kuwawa Jumamosi na mwengine hapo jana katika mapigano huko Samara. Kadhalika gavana wa mkoa wa Salahuddin ,Hamad Hamoud Shagtti ,amenusurika katika shambulio la bomu lililotegwa kandoni mwa barabara, wakati safari wake ulipokua ukipita kuelekea chuo kikuu kimoja mkoani humo.

 • Tarehe 27.08.2007
 • Mwandishi Mohammed AbdulRahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB1i
 • Tarehe 27.08.2007
 • Mwandishi Mohammed AbdulRahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB1i

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com