Al Gore ailaumu Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.12.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Al Gore ailaumu Marekani

Siku chache baada ya kutunukiwa tuzo la Nobel, makamu rais wa zamani wa Marekani Al Gore leo hii amewasili Bali kuhudhuria mkutano wa kimataifa kuhusu utunzaji wa hali ya hewa na amelaumu vikali serikali ya nchi yake.

Al Gore akihutubia mkutano wa Bali

Al Gore akihutubia mkutano wa Bali

Makamu rais wa zamani wa Marekani Al Gore amekaribishwa kwa mashangilio na wajumbe wa mkutano wa Bali kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa. Katika mwito kwa washirika wa mkutano Al Gore aliwashauri wafikie makubaliano hata bila ya kujali msimamo wa Marekani akilaumu serikali ya nchi yake kuzuia mazungumzo ya Bali. Wajumbe waachie tu nafasi fulani wazi katika makubaliano haya ambayo itajazwa na serikali mpya ya Marekani. Mimi si afisa wa serikali alisema Gore na aliongeza: “Nchi yangu, Marekani, kimsingi inabeba dhamana kwa kuzuia mafanikio hapa Bali. Sisi sote tunayajua haya. Lakini si nchi yangu peke ambayo inaweza kuchukua hatua kuhakikisha kwamba tutaendelea mbele kutoka hapa Bali kwa matumaini.”

Mabadiliko yanawezekana, alisema Gore akitaja juu ya serikali mpya Australia ambayo ilitia saini mkataba wa Kyoto kuhusu kupunguza utoaji wa gesi chafu zinazosababisha kuongezeka kwa joto duniani.

Waziri wa mambo ya mazingira na manaibu wao kutoka nchi zisizopungua 180 wana muda hadi kesho Ijumaa kuafikiana kuhusu ratiba mpya ya mazungumzo ambayo yanalenga kukubaliwa kwa mkataba mpya utakaofuata ule wa Kyoto ambao utaisha mwaka 2012.

Miongoni mwa watoaji wakubwa zaidi wa gesi duniani ni Marekani, nchi za Ulaya, Urusi, Canada, Australia, India na China. Waziri wa mazingira ya Ujerumani, Sigmar Gabriel, alisema China si shida, lakini huu unaweza kuwa mtego tu. Sigmar Gabriel: “China ni nchi ambayo hapa inajionyesha kwamba iko tayari kujitolea zaidi lakini wakati huo huo inadai kwamba Marekani pia ichangie. Kwa hivyo kuna hatari fulani ya kufanywa kwa mchezo wa kujificha, yaani kila mara mmoja anamlaumu mwingine akitumai kwamba huyu mwingine hatakubali kuchukua hatua ili yeye pia hatalazimishwa. Na bado hatukufanikiwa kumaliza mchezo huu.”

Bw Al Gore alisisitiza juu ya umuhimu wa mkutano wa Bali ulete matokeo ya maana. Alisema: “Kuna msemo wa Kiafrika usemao: Ukitaka kwenda mbio, nenda peke yako. Ukitaka kufika mbali, nenda kwa pamoja. Sisi inatubidi kwenda kwa mbiu na kufika mbali. Ili kufanya hivyo, tunahitaji tamko lililowazi hapa Bali.”

Baada ya hotuba yake ya dakika 45, Al Gore alipigiwa makofi kwa wingi, lakini kuna wasiwasi ikiwa maneno yake yatasaidia mkutano huu wa Bali umalizike kwa mafanikio. Kwa sasa, misimamo inatofautiana bado.

 • Tarehe 13.12.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CbL5
 • Tarehe 13.12.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CbL5
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com