1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelenskiy akosoa matokeo ya mkutano wa Geneva

19 Februari 2026

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amekosoa matokeo ya mazungumzo ya siku mbili mjini Geneva kati ya wawakilishi wa Ukraine na Urusi, akisema hayakufikia matarajio.

https://p.dw.com/p/590bU
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskiyPicha: Kuba Stezycki/REUTERS

Rais huyo wa Ukraine alikuwa anataka mazungumzo hayo miongoni mwa mambo mengine yaangazie uwezekano wa kufanyika kwa mkutano kati yake na Rais Vladimir Putin.

Putin amesema mazungumzo kama hayo yanawezakufanyika ila mjini Moscow tu, jambo ambalo Zelenskiy amelipinga.

Matokeo hayatoshi

Zaidi ya hayo Zelenskiy anasema alikuwa ameyatakamazungumzo hayo ya Geneva yajikite katika kuangazia masuala ya kiutu kama ubadilishanaji wa wafungwa na raia.

Mkuu wa utumishi wa umma wa Ukraine Andrii Hnatov akitoka kwenye hoteli ilikofanyika mkutano Geneva
Mkuu wa utumishi wa umma wa Ukraine Andrii Hnatov akitoka kwenye hoteli ilikofanyika mkutano GenevaPicha: Pierre Albouy/REUTERS

"Kufikia leo hatuwezi kusema kuwa matokeo yanatosha. Jeshi lilijadili baadhi ya masuala kwa kina. Mambo nyeti ya kisiasa, uwezekano wa maelewano na umuhimu wa mkutano wa viongozi ni mambo ambayo hayajaangaziwa vizuri. Tunatarajia mkutano ujao, na itakuwa vyema kuufanya Februari," alisema Zelenskiy.

Awali upande wa Urusi uliashiria kuwa mazungumzo yajayo yatafanyika karibuni. Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov lakini amesema tarehe au sehemu itakakofanyika mkutano huo ni mambo ambayo hayajaamuliwa.

Marekani kupitia msemaji wa ikulu ya White House Karoline Leavitt kwa upande wake imesema kumekuwa na hatua muhimu zilizopigwa kwenye mazungumzo hayo, huku kukiwekwa ahadi za ushirikiano katika kupata makubaliano ya amani.

Ukraine imeyachukua kutoka kwa Urusi maeneo makubwa

Kwa ujumla Urusi inakalia takriban asilimia 20 ya ardhi ya kitaifa ya Ukraine ikiwemo Crimea iliyozingirwa na kutekwa mwaka 2014.

Mshauri wa Rais Vladimir Putin, Vladimir Medinski akiwa Geneva
Mshauri wa Rais Vladimir Putin, Vladimir Medinski akiwa GenevaPicha: Alexander Ryumin/TASS/ZUMA/picture alliance

Lakini uchambuzi mpya wa data kutoka Taasisi ya Masomo ya Vita, ISW, uliofanywa na shirika la habari la Ufaransa AFP unaonesha kuwa Ukraine imeyachukua kutoka kwa Urusi jumla ya maeneo yenye ukubwa wa kilomita 63 za mraba kati ya Jumatano na Jumapili wiki iliyopita.

Uchunguzi huo unaonesha kuwa Ukraine imeteka kilomita 91 za mraba ikiwemo kilomita 86 za mraba katika eneo moja lililoko karibu kilomita 80 mashariki mwa mji wa Zaporizhzhia, ambapo vikosi vya Urusi vimepiga hatua tangu katikati ya mwaka jana 2025.

Ukraine ilikuwa haijawahi kuchukua tena kutoka kwa Urusi eneo kubwa kama hilo tangu Juni 2023.

Uchunguzi huo vilevile unaonesha kuwa jeshi la Urusi limeteka kilomita 28 za mraba katika maeneo mengine ya Ukraine.

Vyanzo: DPA/Reuters/AFP