1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yoweri Museveni aapishwa rais wa Uganda

12 Mei 2011

Hii leo Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameapishwa rais kwa awamu yake ya nne, katika sherehe iliyohudhuriwa na viongozi kadhaa wa Kiafrika katika mji mkuu wa Uganda Kampala.

https://p.dw.com/p/RNQl
Präsident Museveni hält eine Rede auf der Wahlkampfveranstaltung in Museveni. Foto: DW/Simone Schlindwein 16.2.2011 Wo wurde das Bild aufgenommen?: Kampala
Rais wa Uganda, Yoweri MuseveniPicha: AP

"Nitabakia rais milele" hiyo ilikuwa kauli mbiu ya Museveni katika kampeni yake ya uchaguzi. Hata madikteta wengine katika nchi za Afrika Kaskazini walitamka hivyo na wakajirundikia mali ya serikali kwa miongo kadhaa. Hatimae wakatimuliwa madarakani.

Rais Museveni wa Uganda anangángánia madaraka tangu miaka 25 iliyopita. Kiongozi huyo anatuhumiwa na wengi kuwa ameshinda uchaguzi uliopita kwa kuwapa wapiga kura zawadi ya fedha, katika kampeni iliyogharimu serikali fedha nyingi sana. Museveni ni mmojawapo wa viongozi wa Kiafrika waliopigania haki za wananchi, lakini sasa nguvu na madaraka yanaonekana kumlevya na hivyo kuingia katika kundi la viongozi mafisadi kinyume na malengo yake ya hapo mwanzoni.

Kipi kilichoikumba "Lulu ya Afrika"

Tangu uchaguzi uliofanyika mwezi wa Februari, serikali inatumia mabavu na vitisho dhidi ya waandamanaji na wapinzani wanaoandamana kwa amani. Vikosi vya polisi vinatuhumiwa na mashirika ya haki za binaadamu kutumia mabavu, kufanya ukatili na kuwakamata watu kinyume na sheria. Hata vyombo vya habari vinazidi kubanwa.

Ugandan's burn tires to block the road as they demonstrate against the high cost of fuel and food in the capital Kampala Monday April 18, 2011. Police in Uganda have arrested the country's top opposition leader Kizza Besigye for the third time in a week. Besigye has been trying to walk to work to protest the high cost of gas and food. Last week violence broke out during his second attempt to walk to work and he was shot in the hand by police. (Foto:Stephen Wandera/AP/dapd)
Waandamanaji wakipinga kuongezeka kwa bei za vyakula na mafutaPicha: dapd

Je, kipi kilichoikumba nchi iliyokuwa ikijulikana kama "Lulu ya Afrika"? Je, inaelekea wapi chini ya uongozi wa rais aliechaguliwa upya? Kwanini anangángánia madaraka na anatumia mabavu kuyakandamiza maandamano ya amani yanayopinga kuongezeka kwa bei za vyakula? Labda yeye pia kama viongozi wenzake katika Kaskazini mwa Afrika, hajui hali halisi inayowakabili wananchi katika maisha yao ya kila siku. Hafahamu jinsi ilivyokuwa vigumu kwa familia nyingi za Uganda kupata hata mlo mmoja wa siku.

Utajiri wa mafuta neema au mkosi

Wakati huo huo, kuna uvumi kuwa kiongozi huyo anataka kujitajirisha kwa mafuta yanayotegemewa kuchimbuliwa nchini Uganda. Wataalamu wanatathmini kuwa akiba ya mafuta inafikia mapipa bilioni kadhaa. Tayari inaripotiwa kuwa watu wanahamishwa kwa nguvu kutoka maeneo yenye utajiri wa mafuta. Mafuta hayo yataweza kusaidia kuwatoa wananchi kutoka maisha yao ya dhiki, ikiwa wao pia wataruhusiwa kufaidika. Kwani katika nchi zingine kama vile Nigeria na Chad, utajiri wa mafuta umedhihirika kuwa kama mkosi kwa wananchi na mazingira.

Ndoto ya Museveni ni kubakia rais kwa milele. Lakini, hilo ni jinamizi kwa vijana wengi wa Uganda, wasiomjua rais mwengine isipokuwa Museveni, tangu walipozaliwa.

Mwandishi:Andrea Schmidt/ ZPR(DW-Kiswahili)

Mhariri: Yusuf Saumu