Xi azitaka nchi zaidi kujiunga na mradi wa miundombinu | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.04.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Xi azitaka nchi zaidi kujiunga na mradi wa miundombinu

Rais wa China Xi Jinping amezitaka nchi zaidi duniani zijiunge na mradi wa nchi yake wa ujenzi wa miundombinu, mpango ambao Marekani inahofia unajenga ushawishi mkubwa zaidi wa kimkakati kwa manufaa ya China.

Rais Xi ameutoa wito huo leo Jumamosi katika mkutano wa kilele wa pili kuhusu mradi wa China wa ujenzi wa miundombinu ya kuyaunganisha mabara unaofanyika mjini Beijing, ambao viongozi wengine wameelezea hatua yao ya kuunga mkono mradi huo.

Rais wa Urusi, Vladmir Putin na viongozi wengine wa ulimwengu wameupongeza mradi huo, hatua inayoonekana kama pigo kwa utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump ambao unajaribu kuzikatisha tamaa nchi nyingine zishiriki katika mpango huo.

Jana wakati akiufungua mkutano huo, Xi alijaribu kuondoa wasiwasi wa baadhi ya watu kwamba mradi huo wa China utaziingiza nchi mbalimbali katika mtego wa madeni. Aidha, amekanusha madai kwamba mradi huo hauziendelezi nchi za Afrika na za barani Asia ambazo zimejenga bandari na njia za reli kwa mikopo kutoka China.

Faida kwa wote

Katika hotuba yake Xi aliahidi kuwa nchi yake inadhamiria kuleta faida kwa wote. ''Tunahitaji kuhimiza kuhusu ushiriki kamili wa nchi zaidi pamoja na makampuni,'' alisema kiongozi huyo wa China katika mkutano huo wa kilele unaofanyika katika ukumbi wa mikutano wa serikali na kuhudhuriwa na viongozi wa nchi zaidi ya 40, wakiwemo wa kutoka nchi za Afrika.

Hayo yanajiri wakati ambapo Rais Xi Jinping amesema mikataba yenye thamani ya Dola bilioni 64 imesainiwa leo Jumamosi ambayo ni siku ya pili katika mkutano huo.

China Peking Belt and Road Forum (Getty Images/J. Lee)

Viongozi wanaohudhuria mkutano wa mradi wa miundombinu wa China

Akizungumza wakati akiufunga mkutano huo, rais huyo wa China amerudia kusema kuwa mradi huo mkubwa wa matrilioni ya Dola unaohusisha ujenzi wa barabara, madaraja, mabomba na bandari, utazingatia uwazi na maendeleo ya mazingira safi na pande zote zitashiriki katika msingi wa haki sawa.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na viongozi wanaohudhuria mkutano huo imeelezea kufurahishwa na ''fursa muhimu'' zilizoanzishwa kupitia mradi wa ujenzi wa miundombinu na wamesema unasaidia katika kupatikana kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Washiriki hao ni pamoja na maraisa wa Ufilipino, Kenya na Misri, waziri mkuu wa Italia, Ugiriki na Pakistan pamoja na maafisa wengine wa serikali kutoka Indonesia, Ujerumani na nchi nyingine.

Kenya yakopa milioni ya Dola

Kenya kwa upande wake imejipatia mkopo wa Dola milioni 666 kutoka China kwa ajili ya kujenga mji utakaokuwa na teknolojia ya kisasa utakaoitwa Konza nje kidogo ya mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Ofisi ya Rais Uhuru Kenyatta imeeleza kuwa mkopo huo mpya utakuwa wa viwango vya chini vya riba pamoja na ushirikiano wa kampuni binafsi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kampuni ya mawasiliano ya China, Huawei itausimamia mradi huo wa Konza kwa gharama ya Shilingi bilioni 17.5 za Kenya.

Kenia Uhuru Kenyatta (imago/i Images)

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta

Shilingi bilioni 50 za Kenya zilizobakia, zitaelekezwa katika ujenzi wa barabara ya kisasa itayounganisha uwanja mkubwa wa ndege pamoja na vitongoji vya jiji la Nairobi na utasimamiwa na kampuni ya China ianyoshughulika na ujenzi wa barabara na Madaraja kwa gharama ya Shilingi bilioni 51 za Kenya.

Wakosoaji wanailaumu serikali ya Kenyatta kwa kuvitumbukiza vizazi vijavyo katika mzigo wa madeni makubwa kutokana na kukopa fedha zaidi kutoka China. Hata hivyo, serikali imesema hatua yake ya kukopa fedha hizo, itachochea katika kukuza maendeleo ya kiuchumi nchini Kenya.

Hata hivyo, wakosoaji wanalalamika kwamba kazi kubwa inayofanywa inakwenda katika makampuni yanayomilikiwa na serikali ya China na mradi huo unaweza ukasababisha rushwa na uharibifu wa mazingira. Marekani, Urusi, Japan na India zina wasiwasi kwamba China inajenga ushawishi mkubwa wa kimkakati.

Vita vya kibiashara kati ya China na Marekani

Wakati huo huo, vita vya kibiashara baina ya Marekani na China vinauthiri pia uchumi wa Ujerumani na Ulaya kwa jumla.

«Seidenstraßen»-Gipfel in Peking (picture-alliance/dpa/O. Geibel)

Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Peter Altmaier na makamu wa Waziri Mkuu wa China, Liu He

Hayo yameelezwa na Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Peter Altmaier pembezoni mwa mkutano wa kilele kuhusu mradi wa China wa ujenzi wa miundombinu unaofanyika mjini Beijing.

Waziri Altmaier amekutana na makamu wa Waziri Mkuu wa China, Liu He anayeiwakilisha nchi yake kwenye mazungumzo na Marekani juu ya kuutatua mgogoro huo wa kibiashara.

Altmaier pia amesema mgogoro huo wa mataifa makubwa kabisa mawili unazuia kasi ya ustawi wa uchumi wa dunia. Mazungumzo mengine kati ya China na Marekani yamepangwa kuendelea Jumanne ijayo katika mji wa Beijing.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com