1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya kibiashara kati ya Marekani na China vyapamba moto

Amina Mjahid
6 Julai 2018

Vita vya kibiashara kati ya Marekani na China inaonekana kuendelea kupamba moto, kufuatia ushuru mpya wa Marekani dhidi ya bidhaa za China ulioanza mapema leo, huku nayo China ikiapa kulipiza kisasi.

https://p.dw.com/p/30xkD
Symbolbild zur drohenden Zuspitzung des Handelskrieg s zwischen den Vereinigten Staaten von Amerika
Picha: imago/R. Peters

Usiku wa kuamkia leo, Marekani ilianza kupandisha asilimia 25 ya ushuru kwa bidhaa za China zilizo na thamani ya dola bilioni 34, miongoni mwao zikiwa bidhaa za elektroniki, teknolojia ya juu na vifaa vya kompyuta vya kuhifadhia data.

Nayo wizara ya mambo ya kigeni ya China ikasema hatua ya kulipiza kisasi imeanza kufanya kazi mara moja huku shirika la habari la kitaifa la Xinhua la china likithibitisha asilimia 25 ya ongezeko la ushuru kwa bidhaa za Marekani kama maharage, nyama ya nguruwe na magari ya kielektroniki zilizo na thamani sawa ya dola bilioni 34.

Germany G20
Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa China Xi Jinping Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Loeb

Hata hivyo, wachumi wameonya kwamba vita vya kibiashara vinavyoendelea kati ya Marekani na China huenda vikaathiri mfumo wa biashara na kusababisha mtikisiko mkubwa wa kiuchumi duniani kote.

Rais wa Marekani Donald Trump ameahidi kuipiga China kwa ushuru mkubwa zaidi kwa bidhaa zake zilizo na thamani ya dola bilioni 45 zinazoingia Marekani.

Hatua hii inakuja baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo kati ya mataifa hayo mawili kufeli, na Trump kutoa onyo masaa kadhaa kabla ya hatua ya ongezeko la ushuru kuanza rasmi, akisema kwamba Marekani iko tayari kuweka ushuru mkubwa kwa bidhaa za China zilizo na thamani ya mabilioni ya dola.

Raia wa China wana wasiwasi juu ya vita vya kibiashara vinavyoendelea kati ya taifa lao na Marekani

Serikali ya Trump imeishutumu China kwa kutumia mbinu za kujiimarisha kwa kuiba au kushinikiza makampuni au wawekezaji wa kigeni kutoa teknolojia yao. Maafisa wa Marekani wanahofia kwamba mipango ya China ya kuhodhi teknolojia katika viwanda vya maroboti, teknolojia za biolojia na utaalaamu mkubwa wa kompyuta, itaondoa ushindani katika uongozi wa Marekani kiviwanda.

China US-Produkte im Supermarkt
Raia wa China mjini Beijing akiwa dukani katika sehemu ya bidhaa za Marekani Picha: picture alliance/AP Photo/Andy Wong

Licha ya onyo linazotolewa na wachumi juu ya athari ya vita vya kibiashara kati ya China na Marekani, bado nchi hizo zinaamini zinaweza kuhimili msukosuko uliopo kwa sasa. China inaamini uchumi wake ukiwekeza zaidi juu ya mahitaji ya ndani ya kibiashara na kupunguza utegemezi mkubwa kwa bidhaa za nje inaweza kukabiliana na hali hiyo.

Hata hivyo, baadhi ya raia wa China wana wasiwasi juu ya vita hivi. Han Jie, muwekezaji aliye na miaka 38, anasema bila shaka watu wataathirika na vita vya kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Sera ya Trump ya Amerika Kwanza imewalenga pia washirika wengine wa kibiashara wa Marekani kama Umoja wa Ulaya, Japan, Mexico na hata Canada, kwa kuongeza ushuru wa bidhaa za chuma na bati kutoka mataifa hayo, huku nchi hizo nazo pia zikiongeza ushuru kwa bidhaa za Marekani.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Khelef