1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mariupol: Umoja wa Mataifa watakiwa usimamie njia salama.

Zainab Aziz Mhariri: Babu Abdalla
25 Aprili 2022

Ukraine imeutaka Umoja wa Mataifa kusimamia zoezi la kuwaondoa raia waliozingirwa kwenye eneo la kiwanda cha chuma katika mji wa Mariupol ambalo ni ngome ya mwisho ya wanajeshi wa Ukraine katika mji huo wa bandari.

https://p.dw.com/p/4APqz
Ukraine Krieg | Mariupol
Picha: Musienko Vladislav/Ukrainian News/IMAGO

Wizara ya ulinzi ya Urusi leo Jumatatu imetangaza hatua ya kusitisha mapigano karibu na kiwanda cha chuma cha Azovstal katika mji wa Mariupol ili kuruhusu zoezi la kuwahamisha raia kutoka kwenye eneo la viwanda ambako majeshi ya Urusi yamekuwa yakikabiliana na upinzani katika mji huo wa bandari. 

Msafara wa magari ya kivita ya Urusi katika mji wa pwani wa Mariupol
Msafara wa magari ya kivita ya Urusi katika mji wa pwani wa MariupolPicha: Chingis Kondarov/REUTERS

Wizara ya ulinzi ya Urusi katika taarifa yake imesema kuanzia mwendo wa saa tano asubuhi saa za ulaya ya kati leo hii, vikosi vyake vilianza kutekeleza hatua ya kusimamisha mapigano na kuanza kusogea katika umbali ulio salama na kuhakikisha kuwa raia wanaondolewa na kupelekwa popote ambapo wamechagua.

Urusi imesema Ukraine pia inapaswa kuonyesha utayari wa kuanza zoezi la kuwaondoa watu kwa kutungika bendera nyeupe katika kiwanda cha Azovstal. Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema taarifa hii itawasilishwa kwa walio ndani ya kiwanda hicho kwa njia ya redio kila dakika 30.

Soma:Urusi yaonyesha utayari wa mazungumzo

Ukraine imeutaka Umoja wa Mataifa kusimamia zoezi hilo la kuwaokoa raia waliozingirwa kwenye eneo la kiwanda cha chuma katika mji wa Mariupol ambayo ni ngome ya mwisho ya wanajeshi wa Ukraine katika mji huo wa bandari.

Rais wa Urusi Vladmir Putin
Rais wa Urusi Vladmir PutinPicha: Alexander Nemenov/AFP/Getty Images

Wakati huo huo msemaji wa serikali ya Ujerumani amesema nchi hiyo inapanga kuamua hivi karibuni ikiwa itaidhinisha kupelekwa nchini Ukraine magari ya kivita yapatayo 100 katika hatua ambayo itakuwa ya kwanza kwa Ujerumani kupeleka nchini Ukraine shehena ya silaha nzito.

Kampuni ya silaha ya Ujerumani Rheinmetall imeomba idhini ya kupeleka nje magari hayo ya kivita kwa Ukraine, ikilenga kwanza kuyakarabati magari hayo katika miezi ijayo kabla ya kuyasafirisha.

Soma:Marekani: Yaahidi msaada zaidi wa kijeshi kwa Ukraine

Hatua hiyo ya kampuni ya Rheinmetall inatazamiwa kumlazimisha kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kuchukua msimamo wa wazi kuhusiana na uwezekano wa serikali yake kupeleka silaha nzito moja kwa moja kutoka Ujerumani hadi Ukraine kwa sababu mpango huo unahitaji idhini kutoka kwa baraza la usalama la taifa, ambalo linaongozwa na kansela Scholz. Scholz anakosolewa ndani na nje ya nchi kutokana na kusita kwake kutoa silaha nzito kama vile vifaru kwa ajili ya kuisaidia Ukraine kupambana na Urusi.

Ujerumani imeonekana kujikokota katika suala la kupiga marufuku mafuta ya Urusi, na pia kusita linapokuja suala la kupeleka silaha nzito nchini Ukraine. Baadhi ya wanachama wa NATO wa eneo la mashariki, ambao wanahofia kuwa wanaweza kuwa walengwa watakaofuata wa uvamizi wa Urusi, wangependa Ujerumani ifanye zaidi.

Waziri Mkuu wa Estonia Kaja Kallas amesema wanachotarajia kwa uhakika ni kwamba Ujerumani iwe inaunga mkono maamuzi yote wanayofanya pamoja na pia kuonyesha uongozi kuhusiana na maamuzi hayo.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Ronaldo Schemidt/AFP/Getty Images

Katika ziara yao ya kwanza nchini Ukraine tangu Urusi ilipoivamia nchi hiyo miezi miwili iliyopita, waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na mwenzake wa Mambo ya Nje Antony Blinken wameahidi msaada wa ziada wa kijeshi kwa Ukraine pamoja na silaha za hali ya juu. Maombi ya Ukraine ya kutaka silaha nzito yameongezeka tangu Urusi ilipohamishia mashambulizi yake katika eneo la mashariki la Donbas.

Vyanzo:AFP/DPA/RTRE/AP