Urusi yaonyesha utayari wa mazungumzo | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.04.2022
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Urusi yaonyesha utayari wa mazungumzo

Ikulu ya Kremlin imesema kwamba Moscow bado inasubiri majibu kutoka kwa Ukraine kuhusiana na pendekezo la maandishi la hivi karibuni juu ya mazungumzo ya amani baina ya pande hizo mbili.

Ikulu ya Kremlin aidha imehoji kulikoni rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy hana taarifa na waraka huo baada ya Jumatano hii, Zelenskyy kudai kwamba hajaona wala kusikia chochote kuhusu mapendekezo hayo ya Urusi. 

Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amenukuliwa akiyarejea matamshi yake kwa mara nyingine kwamba mapendekezo yao ya karibuni yaliwasilishwa kwa wapinzani wao kupitia kwa ujumbe wa wasuluhishi kutoka Ukraine. 

Peskov amewaambia waandishi wa habari kwamba Kremlin iliyasikia matamshi ya Zelensky ambayo amesema yaliibua maswali kadhaa ya kwamba, kulikoni hakuna yoyote aliyemuwasilishia rais huyo mapendekezo hayo ya kimaandishi.

Ikumbukwe Aprili 12, rais Vladimir Putin wa Urusi alisema kwamba mazungumzo hayo ya amani yalifikia mwisho, huku mkuu wa ujumbe wa mazungumzo kutoka Ukraine akisema siku ya Jumanne kwamba ilikuwa ni vigumu kutabiri muda wa kurejea kwenye majadiliano hayo na hasa kutokana na uvamizi wa Urusi kwenye jiji la Mariupol na kile alichosema matamanio ya Moscow ya kujiimarisha zaidi kwa kuanzisha mashambulizi mapya ya kijeshi.

Soma Zaidi: Ukraine: Urusi inaendeleza mashambulizi baada ya kuahidi kusitisha mapigano

China yaikosoa Marekani.

Huko China, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa nchi hiyo Wang Wenbin ameiambia Marekani kuacha kusambaza taarifa za uongo za kuikashifu China na badala yake ijiwajibishe yenyewe kuhusiana na mzozo unaoendelea nchini Ukraine.   

"Marekani inapaswa kuacha kueneza habari potofu zinazoikashifu China, itafakari wajibu wake kuhusiana na migogoro kati ya Urusi na Ukraine, na kufanya kazi pamoja na jumuiya ya kimataifa kuendeleza suluhu ya kisiasa ya mgogoro huo. Marekani inapaswa kuacha kuifanya Ulaya na dunia kulipa bei ya juu kwa maslahi yake ya ubinafsi." amesema Wenbin.

Ukraine | Krieg | Pedro Sanchez und Mette Frederiksen in Kiew

Rais wa ukraine Volodymyr Zelensky(katikati) akiwa na waziri mkuu wa Uhispani pedro Sanchez(kushoto) na mette Frederiksen wa Denmark walipozuru Ukraine hii leo kuonyesha kuunga mkono Ukraine.

Nchini Ukraine katika mji wa Kyiv, waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez amesema Uhispania imepeleka tani 200 za vifaa vya kijeshi nchini humo, ikiwa ni pamoja na magari ya kusafirisha vitu vizito na risasi. Amewaambia waandishi wa habari katika mkutano wa pamoja na rais Volodymyr Zelensky kwamba huo ni msaada mkubwa zaidi kupelekwa na Uhispania hadi sasa, ambao ni mara mbili ya ule ambao tayari umetolewa. Waziri mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, pia alikuwepo kwenye mkutano huo.

Soma Zaidi: Mataifa ya Magharibi yatoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine

Aidha, Ukraine imesema imepokea watumishi 19 wa kijeshi na raia waliokamatwa Urusi, katika tukio la kubadilishana wafungwa, baada ya miezi miwili ya mapigano, naibu waziri mkuu wa Ukraine, Iryna Vereshchuk amesema amearifu. Mabadilishano haya ni ya karibuni zaidi, hii ikiwa ni kulingana na Kyiv, ingawa Urusi haijazungumzia chochote kuhusiana na hatua hiyo ama ni wafungwa wangapi waliohusika.

Kutoka Berlin shirika la wahamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM limearifu leo kwamba idadi ya wakimbizi wa ndani nchini Ukraine tangu uvamizi wa Urusi imeongezeka hadi milioni 7.7. Shirika hilo lenye makao yake mjini Geneva limesema leo kwamba zaidi ya wakimbizi wengine 600,000 waliyakimbia makazi yao ndani ya nchi hiyo katika kipindi cha siku 17 za mwezi huu wa Aprili. Idadi hii ya IOM inatolewa siku moja baada ya shirika la wakimbizi la Umoja huo, UNHCR kuarifu kwamba idadi ya wakimbizi kutoka Ukraine imepindukia milioni 5.

Mashirika: RTRE/AFPE/APE