Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, anatayarisha mkutano juu ya amani ya Mashariki ya Kati. | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.10.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, anatayarisha mkutano juu ya amani ya Mashariki ya Kati.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Bibi Condoleezza Rice, yuko Mashariki ya Kati akijaribu kupata msimamo wa pamoja baina ya Wa-Israeli na Wapalastina utakaoweza kuwa msingi wa mashauriano katika mkutano mkubwa juu ya Mashariki ya Kati utakaofanywa mwaka huu huko Marekani. Hadi sasa matokeo sio mazuri.

Rais George Bush wa Marekani

Rais George Bush wa Marekani

Condoleezza Rice alikuwa na haki pale katika ziara yake ya mwishoni huko Mashariki ya Kati aliposema mtu ana mambo muhimu zaidi ya kufanya ikiwa tu hizo pande zinazogombana katika Mashariki ya Kati zitakwenda katika mkutano huo wa Marekani ili kupiga picha za wajumbe wao wakiwa pamoja. Pale mwisho wa mwezi Novemba utakapofanywa mkutano juu ya Mashariki ya Kati huko Annapolis, sio mbali na mji wa Washington, mkutano ambao umeitishwa na Rais Bush,basi itabidi kufanyike maendeleo ya kweli kuelekea lengo la kuutatua mzozo wa Mashariki ya Kati.

Hayo yote ni sawa. Lakini suala ni vipi jambo hilo litafanyika? Hapo ndipo watu wanatafautiana. Shetani yuko pale mtu anapokwenda katika undani wa kutafuta suluhu. Rais Mahmoud Abbas wa Wapalastina anataka mambo yawekwe wazi kabisa kuhusu masuala muhimu, juu ya hali ya baadae ya mji wa Jerusalem, suala la wakimbizi wa Kipalastina waliotimuliwa kutoka makwao, michoro ya mipaka ya siku za mbele na makaazi ya walowezi wa Ki-Israeli katika maeneo ya Wapalastina yaliotekwa na Israel. Lakini, Israel, haitaki kuhakikisha jambo lolote, na inataka kubakia tu kuizungumzia karatasi ya kimsingi ambayo itaelezea tu, kwa mara nyingine, misingi ya kuweko amani baina ya pande mbili; lakini katu haitaki kujiwajibisha na mambo Fulani.

Katika siku zilizopita, kumetolewa hadharani karatasi za aina hiyo, na karatasi hizo hazijawa na maana yeyote. Muhimu kabisa kati ya karatasi hizo ni Mapatano ya Oslo, ambayo matokeo yake ni kwamba wanasiasa wa Israel wameyavunja. Vivyo hivyo ni ile karatasi iliokuwa na kile kilichoitwa Ramani ya Njia ya Amani kwa ajili ya Mashariki ya Kati, na ambayo ilipendekezwa na Marekani, Umoja wa Mataifa, Russia na Umoja wa Ulaya. Wa-Israeli, kama vile Wapalastina, wanatoa miito ya kuchukuliwa hatua, lakini hazifikirii kuzichukuwa hatua zenyewe.

Huko Annapolis, mambo yatabidi yawe vingine. Hiyo ni nafasi ya mwisho kwa Rais George Bush kuushughulikia kikweli mzozo wa Mashariki ya Kati baada ya yeye kupata hasara zote za kisiasa katika eneo hilo. Angalau mara hii anajaribu ajipatie, naweza kusema, kijimafanikio. Anahitaji mafanikio ili aboreshe sura yake iliochafuka katika Ulimwengu wa Kiarabu, na amemwachia waziri wake wa mambo ya kigeni atangaze kwa sauti kubwa kile ambacho hakijawahi kusikika kutoka kwa George Bush. Nacho ni kwamba Marekani itafanya kila kitu inachoweza ili kuwezesha kuundwa dola ya Kipalastina.

Vipi ataweza kulitekeleza jambo hilo, bila ya kugongana na siasa za Israel, kinabaki kuwa kitandawili. Kwa muda mrefu George Bush, na pia watangulizi wake, wameiachia Israel ifanye inavotaka, kwa hivyo ni taabu sasa kwa yeye kuweza kuinyoshea Israel kidole na kuiambia Rejea Nyuma. Lakini Ehud Olmert, waziri mkuu wa Israel aliye katika hali dhaifu ya kisiasa, anatambua kwamba itambidi mahala Fulani amridhie Bush. Yeye amebanwa na wapinzani wake wa kisiasa ndani nchini mwake na pia marafiki wake wa zamani ndani ya chama chake. Ndio maana kwa ghafla Olmert akatamka kwamba Israel inaweza kuachilia sehemu Fulani za mji wa Jerusalem, na kusema kwamba kuingizwa sehemu hizo katika mji wa sasa kulikuwa ni kosa.

Hiyo ni hatua ndogo ya mwanzo, nyingine lazima zifuate. kama Ehud Olmert ana uwezo wa kufikia kule anakolenga na kuifuatiliza njia hiyo ni suala ambalo bado ni kizungumkuti. Hapo ndiko kunanin’ginia kufanikiwa au kutofanikwa mkutano wa Annapolis. Mkutano huo lazima ulete maendeleo ya kweli, na ikiwa utakuwa tu wa kupiga picha za pamoja, basi hiyo itakuwa kabisa ni kupoteza wakati.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com