Iran, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kukutana
23 Septemba 2025Duru zinaeleza kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa Iran, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, watakutana Jumanne pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kujadiliana kuhusu mzozo wa malengo ya nyuklia ya Iran huku kukiwa na vitisho vya kuwekewa vikwazo.
Nchi hizo tatu zinazojulikana kama E3, zilianzisha mchakato wa siku 30 mnamo Agosti 28, wa kurudisha vikwazo vya Umoja wa Mataifa, zikiishutumu Iran kwa kushindwa kutii makubaliano ya mwaka 2015 kati yake na mataifa yenye nguvu duniani, yaliyolenga kuizuia kutengeneza silaha za nyuklia.
Septemba 9, Shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia, IAEA na Iran zilifikia makubaliano ya kuanza tena ukaguzi katika vinu vya nyuklia.
Tanbihi ya Mhariri: Makala hii awali ilijumuisha picha kutoka shirika la SalamPix. Iliondolewa tarehe 12 Machi 2026 baada ya Picture Alliance na Imago kutuarifu kuwa walikuwa wanaondoa picha za SalamPix kutokana na wasiwasi kuhusu chanzo chake na uwezekano wa kuwa zimehaririwa.