Iran mbioni kuepuka kurejeshewa vikwazo vya kiuchumi
19 Septemba 2025
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi, katika kujibu hatua hiyo ametoa pendekezo linalozingatia usawa kwa mataifa yenye nguvu ya Ulaya ili kuzuia nchi yake kurejeshwa kwenye vikwazo vya Umoja wa Mataifa.
Araghchi, amesema pendekezo hilo ni bunifu, la haki, na lenye uwiano linashughulikia maswala ya kweli na yenye manufaa kwa pande zote, lilitolewa jana Alhamisi kwa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani mataifa ambayo yanajulikana kama E3, pamoja na Umoja wa Ulaya.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi, amesisitiza kwamba kuligeuza wazo hili na kuwa vitendo ni hatua inayoweza kuharakisha kutatua mambo ya msingi ili kuepusha mgogoro, akihoji kwamba "Iran haiwezi kuwa mhusika pekee anayepaswa kuwajibika".
Kundi la E3, limedai kuwa Tehran imepuuza ahadi zake chini ya makubaliano ya nyuklia ya kihistoria yaliyotiwa saini mwaka 2015. Makubaliano hayo yaliwezesha kuondolewa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran kwa kubadilishana na mpango wake wa nyuklia.
Makubaliano hayo yalilenga kuizuia Iran kuunda silaha za nyuklia, lengo ambalo mataifa yenye nguvu ya Magharibi na Israel, hasimu mkubwa wa Iran, yamekuwa yakiituhumu Iran kwa muda mrefu kuwa inalenga kuwa na silaha za nyuklia, tuhuma ambazo Tehran imekuwa ikizikanusha vikali.
Makubaliano hayo ambayo yanajulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, au JCPOA, yamekuwa yakilegalega tangu Marekani ilipojiondoa kutoka kwenye mkataba huo mwaka 2018 katika muhula wa kwanza wa Donald Trump ambapo Marekani iliiwekea tena vikwazo Iran.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmail Baghaei amesema Iran iko chini ya shinikizo la nchi za Magharibi ikitakiwa kuwaruhusu wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kufika kwenye maeneo yake ya nyuklia yaliyoshambuliwa na Marekani na Israel mwezi Juni. Ametahadharisha kuwa endapo nchi yake itafanyiwa vitendo visivyo vya haki basi nayo itavunja makubaliano yake na shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya nyuklia IAEA.
Wiki iliyopita, Iran ilikubaliana kuhusu mfumo mpya wa kufanya kazi na shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) baada ya kusimamisha ushirikiano na shirika hilo kutokana na mashambulizi ya Israel na Marekani.
IAEA imeonya kuwa Iran ndiyo nchi pekee isiyo na silaha za nyuklia ambayo inarutubisha madini ya uranium hadi asilimia 60 kiwango ambacho kinavuka asilimia 3.67 kilichowekwa katika makubaliano ya mwaka 2015. IAEA imesema kiwango cha urutubishaji wa Uranium cha Iran kinakaribia kufikia asilimia 90 ya madini hayo kuweza kuunda silaha za nyuklia.
Katika hatua nyingine Iran imeondoa azimio iliyowasilisha la kupiga marufuku mashambulizi kwenye maeneo yake nyuklia.
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Reza Najafi amesema ametangaza hatua hiyo kutokana na nia njema ya Iran na ombi la nchi kadhaa wanachama. Najafi amesema yote hayo ni kwa ajili ya kutaka kujenga ushirikiano na kwamba rasimu hiyo imeahirishwa na nchi yake hadi kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wa mwaka ujao.
Vyanzo: AFP/AP