1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajumbe wa Marekani wawasili Sharm El-Sheikh

8 Oktoba 2025

Wapatanishi wakuu wa Marekani Jumatano wamejiunga na mazungumzo yanayolenga kuvimaliza vita vya Gaza.

https://p.dw.com/p/51gEt
Waandamanaji katika mji wa Sharm El-Sheikh wakati wa mazungumzo ya amani ya Gaza
Waandamanaji katika mji wa Sharm El-Sheikh wakati wa mazungumzo ya amani ya GazaPicha: Ahmad Gharabli/AFP

Rais wa Misri ambaye ndiye mwenyeji wa mazungumzo hayo Abdel Fattah al-Sisi, ameelezea matumaini kuhusiana na mazungumzo hayo ambayo si ya moja kwa moja kati ya Hamas na Israel.

Vyombo vya habari nchini Misri vimemuonesha mjumbe wa Mashariki ya Kati wa Rais Donald Trump, Steve Witkoff na Jared Kushner wakiwasili katika mazungumzo hayo huko Sharm El-Sheikh.

Afisa mkuu wa HamasTaher al-Nunu ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa, AFP kwamba wapatanishi wanafanya juhudi kuondoa vikwazo vyovyote katika utekelezaji wa mpango wa kusitisha vita.

Haya yanafanyika wakati ambapo jeshi la Israel Jumatano limezuia msafara wa kundi la boti tisa unaopeleka msaada Gaza katika Bahari ya Mediterenia.

Ripoti zinaarifu kuwa wanaharakati 145 wanaoripotiwa kuwa katika hali nzuri ya kiafya wamekamatwa na wanapelekwa katika ufukwe wa Israel kwa ajili ya kurudishwa makwao.