Juhudi za kidiplomasia za kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza, zinaendelea. | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Juhudi za kidiplomasia za kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza, zinaendelea.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo linatarajia kurudi katika majadiliano kuhusu wito wa mataifa ya Kiarabu kutaka kusitishwa mapigano mara moja Gaza, huku Misri ikitoa pendekezo la kuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo

default

Rais wa Misri, Hosni Mubarak, (kulia), akifanya mazungumzo na Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy katika mji wa Sharm el-Sheik, Misri.


Baraza hilo lenye wajumbe 15 linatarajia kukutana baadaye leo katika ngazi ya mawaziri na kupima muswada wa azimio la Libya lililowasilishwa kwa niaba ya mataifa ya Kiarabu. Mawaziri wa mambo ya nje wa Libya Abdel-Rahman Shalgam na mwenzake wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Saudi Al-Faisal, walisema baraza la usalama la umoja wa mataifa lina jukumu kubwa la kumaliza mizozo mbalimbali haraka iwezekenavyo, na mzozo wa sasa wa Gaza lazima utatuliwe.


Lakini wanadiplomasia wameelezea wasiwasi wao kuhusu muswada huo, ambao unapingwa na Israel, kuwa utapata uungwaji mkono kutoka mataifa muhimu ya Magharibi yenye kura ya veto, hususan Marekani.


Ufaransa ambayo ni mwenyekiti wa baraza la usalama la umoja wa mataifa kwa mwezi huu, imekuwa ikishirikiana na mataifa ya Kiarabu kuafikiana kuhusu muswada huo unaoitaka Israel kusitisha mapigano dhidi ya kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya watu 660, tangu yalipoanza Desemba 27, mwaka uliopita.


Kwa upande wake Misri imesema inazialika Israel na Palestina kwa mazungumzo ya dharura kujadili hali ya usalama katika mpaka wa Misri na Gaza. Kauli hiyo imetolewa na Rais wa nchi hiyo, Hosni Mubarak, mara baada ya kukutana na Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy jana huko Sharm el-Sheikh. Naye Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Bernard Kouchner amesema wito huo wa Misri unazitaka Israel na Palestina kukutana hii leo mjini Cairo.


Aidha, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Condoleezza Rice aliliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa wamefurahishwa na wito wa Rais Mubarak na kuahidi kufuatilia hatua zaidi za majadiliano hayo.


Naye Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, David Miliband pia ameunga mkono suala hilo akilitaka baraza la usalama kuwa wazi katika kanuni na kufanyia vitendo hitimisho la kuimarisha na kuzitia nguvu juhudi hizo.


Kwa upande mwingine mkuu wa sera za mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya (EU), Javier Solana, ameeleza matumaini yake kuwa huenda mkutano huo wa Misri ukaleta mafanikio.


Wakati huo huo, Mexico pia imeungana na mataifa ya Amerika ya Kusini yanayotaka kusitishwa kwa mapigano hayo katika Ukanda wa Gaza kwa kupendekeza kufanyika mazungumzo ya amani baina ya Israel na Palestina, yenye lengo la kumaliza mapigano hayo.
 • Tarehe 07.01.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GTS2
 • Tarehe 07.01.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GTS2
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com