1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

160108 Kenia EU

Riegert / Dreyer17 Januari 2008

Katika mwsada wa pamoja, wabunge wa bunge la Ulaya jana jioni waliutaka Umoja wa Ulaya kusitisha kwa muda malipo ya misaada kwa serikali ya Kenya. Kamishna wa masuala ya mendeleo, Louis Michel, aliunga mkono dai hilo.

https://p.dw.com/p/Ct3e
Umoja wa Ulaya yataka vurugu zimalize KenyaPicha: AP

Katika mjadala wao wa jana kuhusu suala la Kenya, wabunge wa Umoja wa Ulaya walisema matokeo ya uchaguzi hayaaminiki na walitaka urudiwe upya ikiwa haitawezekana kuhesabu tena kura kwa njia sawa. Mswada huu ulitaka pia msaada kwa serikali ya Kenya usimamishwe. Mbunge Glenys Kinnock wa Uingereza anawakilisha maoni ya wengi akisema: "Lazima Umoja wa Ulaya usitishe msaada wake kwa bajeti ya Kenya hadi suluhisho la kisiasa litakapopatikana. Kwa maoni yangu tunapaswa kuweka wazi kwamba uongozi bora ni sharti ya kutolewa misaada kama inavyokubaliwa katika mikataba ya ushirikiano. Nafikiri hatukutia maanani vya kutosha madai mengi ya rushwa katika nchi hiyo."
Mbungu huyu Kinnock pamoja na wabunge wengine pia waliukosoa Umoja wa Ulaya kwa kulipa Euro Millioni 40.6 kama msaada siku moja tu baada ya uchaguzi. Lakini kamishna wa masuala ya maendeleo, Louis Michel, alikanusha lawama hizo. Alisema malipo yalisitishwa hadi baada ya uchaguzi kufanyika, ili kutoingilia kati wakati wa kampeni. Lakini shaka kuhusu matokeo ya uchaguzi zilisikika tu baada ya kutuma fedha hizo. Michel alikumbusha kwamba matumizi ya fedha hizo ambazo ni sehemu tu ya Euro 380 zinazotarajiwa kulipwa hadi mwaka wa 2013 yatadhibitiwa.
Kamishna Louis Michel, ambaye tayari mwanzoni mwa wiki hii alisema Umoja wa Ulaya utafikiria kuiwekea vikwazo Kenya kuhusiana na malipo ya misaada ikiwa suluhisho la kisiasa halitapatikana, alirudia tishio hilo mbele ya bunge la Ulaya, lakini pia alifutilia mbali uwezekano wa kusitisha misaada mara moja kwani hatua hiyo ingeweza kuwaathiri watu wa kawaida.
Hata hivyo, Louis Michel alirudia pia mwito wake kwa wanasiasa wa Kenya: "Ni wazi kwamba tunahitaji kila pande iwe tayari kwa suluhisho la kisiasa. Bila ya hayo, Umoja wa Ulaya bila shaka unalazimishwa kufikiria upya uhusiano wake na Kenya ambao ulikuwa mzuri sana hadi sasa. Kenya iliangaliwa kuwa nchi iliyopita kiwango cha wastani kuhusu haki za binadamu na utawala bora."
Kamishna Michel aliongeza kusema kwamba Umoja wa Ulaya uko tayari pia kupatanisha katika mzozo nchini Kenya. Mwakilishi wa masuala ya nje yuko tayari kusafiri kwenda Kenya, lakini kwanza ni juu ya watapanisha wa Kiafrika. Kwa mujibu wa kamishna Michel, tatizo la Kiafrika linapaswa kutatuliwa na Waafrika na Umoja wa Afrika.
Waziri wa Ujerumani anayehusika na masuala ya maendeleo na ushirikiano wa uchumi, Bi Heidemarie Wieczorek-Zeul, pia alitaka shinikizo dhidi ya serikali ya Mwai Kibaki liongezwe. Kenya imevunja ahadi zake za kuheshimu demokrasia na sheria katika udanganyifu wa zoezi la kupiga kura, alisema waziri huyu, na alidai lazima Umoja wa Ulaya uchukue hatua na kusitisha malipo ya misaada kwa muda.