1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Darfur waafikiana kwa pamoja kushiriki katika mpango wa amani ya Darfur

6 Agosti 2007

Makundi ya waasi wa eneo la mzozo la Darfur nchini Sudan wanakamilisha mkutano ulioanza mwishoni mwa wiki jana.Kikao hicho kililenga kufikia muafaka na serikali ya Sudan na kufadhiliwa na Umoja wa mataifa na Afrika.

https://p.dw.com/p/CB2B
Majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika,AMIS
Majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika,AMISPicha: AP

Hatua hiyo ilifanyika baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kuidhinisha hatua ya kupeleka kikosi kilichoimarishwa cha kulinda amani katika eneo la Darfur.Ghasia katika eneo la Darfur zimesababisha vifo vya takriban watu laki mbili na wengine yapata milioni 2 kuachwa bila makao.

Kikao hicho cha siku 3 kililenga kujadilia kundi litakalowakilisha waasi ili kufikia muafaka na serikali ya Khartoum.Kwa mujibu wa mjumbe wa maalum wa Umoja wa Afrika Dr Salim Ahmed Salim, mkutano kati yao na serikali huenda ukafanyika katika kipindi cha miezi miwili ijayo.

Suala jengine muhimu lililojadiliwa ni siku na mahala pa kufanyia mazungumzo yenyewe.Viongozi wa makundi mawili muhimu ya waasi walisusia kikao hicho.Mwanzilishi wa vuguvugu la Darfur Abdel Wahid Mohammed Nur aliye uhamishoni mjini Paris,Ufaransa alisusia kikao hicho kwa madai kuwa makundi yaliyohudhuria hawakuwa halali na mazungumzo hayo yangefanyika baada ya makubaliano ya kusitisha vita kufikiwa.Abdelwahid al Nur ni mwenyekiti wa Kundi la waasi la Sudan Liberation Movement SLM

''Hatuendi… na kundi la SLM halitashiriki katika mazungumzo hayo ya Arusha.Kila siku mauaji yanatokea na mamia ya watu wa Darfur wanauawa.Mauaji hayo yanasababishwa na kundi la Janjaweed wakiungwa mkono na serikali.Tunatoa wito kwa jamii ya kimataifa kuwa tunataka kuhakikishiwa usalama kwa watu wetu na mauaji yasitishwe.''

Suleiman Jamous Muasi mwengine anayedhaniwa kuwa mpatanishi muhimu anazuiliwa bna serikali katika hospitali moja nchini Sudan hata baada ya wito wa kuachiwa kwake kutolewa.

Makubaliano ya amani kati ya waasi na serikali ya Sudan yalifikiwa mwezi mei mwaka jana mjini Abuja nchini Nigeria japo kuidhinishwa na kundi moja tu la waasi.Jambo hilo lilisababisha ghasia kuanza upya katika eneo hilo.Hata hivyo Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika mazungumzo hayo Jan Eliasson ana matumaini kuwa hatua zitapigwa na la msingi ni kutafakari matatizo yanayowakabili wakazi wa eneo hilo.

''Hapa tulipo tunapaswa kutafakari matatizo yanayowakabili wanawake na watoto.Tukumbuke sura ya wanawake…watoto..na wanaume walioko kwenye kambi na vijiji na matatizo yanayowakabili tunapojadiliana. ''

Hata hivyo waashiriki wa mkutano huo wa Arusha wana imani kuwa waasi hao wataafikiana.Kulingana na Jerome Tubiana mtaalam wa masuala ya Darfur aliyeandaa ripoti kuhusu waasi hao mwezi jana anaeleza kwamba tatizo ni vita binafsi kati yao wala sio masuala ya msingi.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa mataifa vita na ukame katika eneo la Darfur vimesababisha vifo vya takriban watu laki mbili na wengine milioni 2 kuachwa bila makao.