Vipengele muhimu vya Mkataba wa Lisbon | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.09.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Vipengele muhimu vya Mkataba wa Lisbon

Mkataba wa Lisbon wa Umoja wa Ulaya ambao mustakbali wake utaamuliwa na wapiga kura wa Ireland hapo Ijumaa ni mpango mkubwa wa mageuzi wenye nia ya kuziboresha taasisi za umoja huo na kurahisisha utowaji wa maamuzi.

default

Bendera za nchi wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya.

Wale wenye mashaka na mkataba huo wanasema ni katiba iliojificha na hatua ya kuelekea katika serikali moja ya shirikisho ya Umoja wa Ulaya.

Mkataba huo uliosainiwa katika mji mkuu wa Ureno Lisbon hapo tarehe 13 Desemba mwaka 2007 na viongozi wa Umoja wa Ulaya lazima uridhiwe na mataifa yote wanachama 27 kabla ya kuanza kufanya kazi.

Wakati mataifa mengine yote yalitumia bunge kuupitisha mkataba huo Ireland inalazimika kikatiba kuitisha kura ya maoni na hii itakuwa ni ya pili kufuatia fadhaa ya kukataliwa hapo mwaka jana.

Kura ya ndio mara hii itaongeza shinikizo kwa marais wa Jamhuri ya Czech na Poland kusaini mkataba huo na kuondowa vikwazo vya mwisho kuuwezesha mkataba huo uanze kazi hapo mwakani.

Hivi ni baadhi ya vipengele vikuu vya mkataba huo:

Kwanza huu ni mkataba na sio katiba.

Jaribio la kuipatia Umoja wa Ulaya katiba yake ya kwanza kuchukuwa nafasi ya mikataba muhimu ule wa Rome wa mwaka 1957, wa Maastricht wa mwaka 1992,wa Amsterdam wa mwaka 1996 na wa Nice wa mwaka 2000 lilizimwa hapo mwaka 2005 wakati wapiga kura wa Ufaransa na Uholanzi walipoikataa katika kura zao za maoni za taifa.

Mkataba wa Lisbon utakuwa wa ziada na kurekebisha mikataba iliotangulia lakini haitochukuwa nafasi ya mikataba hiyo.

Haki mpya kwa raia wa Umoja wa Ulaya:

Mkataba huo unalazimisha kutekelezwa kwa Mkataba wa Umoja wa Ulaya wa Haki za Msingi juu ya kwamba Uingereza na Poland hazilazimiki kuuzingatia.

Raia milioni moja wa Umoja wa Ulaya wataweza kuialika Kamisheni ya Umoja wa Ulaya kuwasilisha pendekezo la kisheria katika eneo husika.

Nyadhifa za asasi:

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya lenye kuwakilisha nchi wanachama 27 atachaguliwa na viongozi kwa kipindi cha miaka miwili na nusu badala ya utaratibu mgumu uliopo hivi sasa wa mataifa kupokezana wadhifa wa urais kila baada ya miezi sita.

Rais ataandaa mikutano ya kilele na kuiwakilisha Umoja wa Ulaya katika jukwaa la dunia ambapo inatarajiwa bila ya kuingilia shughuli za Masuala ya Kigeni na Sera ya Usalama.

Wadhifa wa mambo ya nje utajumuisha pamoja dhima za hivi sasa za Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya wa Sera ya Pamoja ya Mambo ya nje na Usalama Javier Solana na Kamishna wa Uhusiano wa Kigeni Benita Ferrero Waldner.

Kamisheni ya Umoja wa Ulaya ambayo ni chombo cha utendaji wajumbe wake watapunguzwa kuanzia mwaka 2014 ili kuleta ufanisi zaidi.

Mkataba huo pia umeongeza nyanja za sera ambapo mabunge yaliochaguliwa ya Ulaya huidhinisha miswada ya sheria hususan katika fani nyeti za sheria,usalama na uhamiaji.

Mabunge ya taifa yatakuwa na sauti katika upangaji sera wa Umoja wa Ulaya.

Mkataba huo pia unaanzisha mfumo mpya wa upigaji kura.

Katika mfumo huo mpya wa kupiga kura wingi maradufu, asilimia 55 ya nchi wanachama kwa hivi sasa ni nchi 15 kati ya 27 zenye kuwakilisha angalau asilimia 65 ya idadi ya watu wa Umoja wa Ulaya lazima wapige kura kuunga mkono ili sheria iweze kupitishwa.

Mkataba huo unaweka uwezekano kwa nchi kujitowa katika Umoja wa Ulaya chini ya masharti yatakayojadiliwa na washirika wenzake.

Halikadhalika viongozi wa Umoja wa Ulaya wanahakikisha kwamba mkataba hautoingilia haki katika maisha na elimu. Wanahakikisha hautoupa umoja huo wenye makao yake makuu mjini Brussels madaraka mapya ya kuongeza kodi wala kuilazimisha serikali ya Ireland kushiriki katika operesheni za usalama za umoja huo kuathiri msimamo wake wa kijeshi wa kutopendelea upande wowote pamoja na kuleta taathira kwa majeshi yake ya ulinzi.

Mwandishi:Mohamed Dahman/ AFP

Mhariri: P.Martin

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com