Viongozi wa Umoja wa Ulaya waonyesha mshikamano kuhusu mgogoro wa kiuchumi | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.03.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa Umoja wa Ulaya waonyesha mshikamano kuhusu mgogoro wa kiuchumi

Viongozi wako tayari kufanya mashauriano

Umoja wa Ulaya umeshikamana pamoja wakati huu unapokabiliwa na mgogoro wa kiuchumi na umeonyesha uko tayari kufanya mashauriano. Huo ndiyo ujumbe muhimu uliojitokeza kwenye mkutano maalum wa Umoja wa Mataifa uliofanyika siku ya Jumapili mjini Brussels Ubelgiji.

Mgogoro wa masoko ya fedha na wa kiuchumi unaenea kwa kasi isiyo mithili. Umetufunza somo moja kwamba kanuni za kisiasa ambazo katika majuma machache yaliyopita zilionekana kuwa imara sasa haziwezi tena kumudu matatizo haya ya kiuchumi. Na hakuna awezaye kusema kwa ujasiri ni kitu gani kinachoweza kufaa katika majuma yajayo ili kuweza kuzuia migogoro kutokea.

Hali hiyo pia inaweza kuenda sambamba na jibu wazi la hapana kwa mpango wa kuuokoa uchumi wa nchi za mashariki mwa Ulaya. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na mwenyekiti wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Mirek Topolanek, wamepinga mpango wa kuufua uchumi wa Hungary, Latvia, Romania, Bulgaria na mataifa mengine.

Je waziri mkuu wa Hungary Ferenc Gyurcsany anaonekana kuwa mdhaifu anapozungumzia mahitaji ya kiwango cha yuro bilioni 190 kwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya mashariki mwa bara la Ulaya? Au inawezekana kuwa katika majuma kadhaa yajayo mgogoro wa mabenki utazitishia nchi za Umoja wa Ulaya kwa sababu kwa nchi hizi gharama inaweza kuwa kubwa kukopesha fedha katika masoko ya fedha? Mwezi Disemba mwaka jana serikali nyingi zilisisitiza hazikuwa zikikabiliwa na mgogoro wa kifedha. Sasa ziko katika mporomoko mkubwa.

Ni kweli kuwa maendeleo haya yamefanyika haraka. Tayari kunazo dalili kwamba mgogoro huu wa kiuchumi unaweza kuidhoofisha sarafu ya yuro inayotumiwa katika nchi 16 wanachama wa Umoja wa Ulaya. Jamhuri ya Ireland, Ugiriki, Uhispania na Italy zinakabiliwa na matatizo makubwa kuweza kulipa madeni yao ya kitaifa.

Sarafu ya yuro tayari inakabiliwa na shinikizo kubwa katika masoko ya hisa. Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na maswala ya sarafu Joaquín Almunia ameonya juu ya kuongezeka kwa ushindani kutoka kwa sarafu nyingine. Viongozi wa Umoja wa Ulaya kwenye mkutano wao wa dharura hawakufaulu kupata jibu la vitisho hivi.

Ujerumani kama nchi mojawapo ya Umoja wa Ulaya iliyo na uchumi imara, inasita kuzisaidia nchi nyengine ili kuzuia uwezekano wa hiyo yenyewe kukabiliwa na hasara katika mikopo yake.

Sasa inategemewa kwamba viongozi wa Umoja wa Ulaya watakuwa wakakamavu kwenye majadiliano yatakayofanyika katika mkutano wa nchi 20 zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani utakaofanyika Aprili 2 mjini London Uingereza, kwa kuwa ikilinganishwa na matatizo mengine duniani, nchi kadhaa za Ulaya zimeanza tena kupata afueni. Bara la Ulaya linapaswa kubakia katika mashindano pamoja na maeneo mengine ulimwenguni.

Mkutano wa mjini Brussels ulioitishwa kwa dharura umedhihirisha kuwa nchi ndogo wanachama wa Umoja wa Ulaya hazitaki kuchukuliwa kuwa nchi za tabaka la pili. Hazitaki kulambishwa siagi iliyopakwa kwenye mkate na kunyimwa utamu wa mkate wenyewe.

Mkutano mzima wa Brussels ulikuwa kinyume cha mkutano uliofanyika mjini Berlin juma moja lilipita uliolenga kufanya maandalizi ya mkutano wa nchi 20 zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, ambapo nchi kubwa pekee za Umoja wa Ulaya zitashiriki. Hata hivyo huu si wakati wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuvutana. Mgogoro huu wa kiuchumi ni mkubwa mno kuliko kile mtu anachoweza kufanya kukabiliana nao.

 • Tarehe 02.03.2009
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/H3tI
 • Tarehe 02.03.2009
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/H3tI
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com