1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Venezuela: Hugo Chavez mshindi wa kura ya maoni

Miraji Othman17 Februari 2009

Wanavenezuela wanakubali Chavez apiganie tena uchaguzi wa urais

https://p.dw.com/p/Gw2p
Rais Hugo Chavez wa VenezuelaPicha: AP

Rais Hugo Chavez wa Venezuela ameshinda katika kura ya maoni iliofanywa nchini mwake jumapili iliopita, hivyo sasa anaruhusiwa kubakia madarakani kwa muda wote pindi tu atawashinda wapinzani wake katika uchaguzi. Hiyo ina maana kwamba nchi hiyo ya Amerika ya Kati itabaki kuwa chini ya uongozi wa siasa za kijamaa na mapambano dhidi ya Marekani. Hugo Chavez ameshakuwa madarakani kwa miaka 10 sasa na kura hiyo ya maoni imesaidia kumfagulia njia ya kulifikia lile lengo lake la kutaka kutawala kwa miongo ijayo, japokuwa mgogoro wa sasa wa kiuchumi duniani utamzuwia kutumia fedha nyingi alizokuwa akizipata kutoka viwanda vya mafuta alivovitaifisha, fedha zilizomwezesha kupanuwa ushawishi wake katika nchi za nje.

Asili mia 54 ya wapiga kura waliyakubali mageuzi ya katiba, na asilimia 45 kupinga, hivyo kuondosha vikwazo vilivowekwa kwake yeye kuchaguliwa tena. Watu milioni 11 walikwenda kupiga kura kati ya milioni 17 walio na haki ya kufanya hivyo katika uchaguzi uliofanyika kwa utulivu. Mhula wa Hugo Chavez sasa kutawala unamalizika mwaka 2012, na kwa hivyo ataweza kuwa mtetezi wa muhula mwengine wa urais hadi mwaka 2019. Alisema hivi ulipotangazwa ushindi wake:

" Mwanajeshi huyu yuko tayari kuwa mtetezi wa Jamhuri ya Venezuela kwa kipindi cha baina ya mwaka 2013 na 2019."

Yaishi Mapinduzi, alisema Chavez akiwa amesimama katika dirisha la sebule la kasri yake, huku akiwa amevaa shati jekundu, alama ya chama chake cha kisiasa anachokiongoza. Lakini mara hii, kinyume na wakati anapotoa hotuba za ushindi, alijiepusha kutangaza siasa mpya, na huenda, kutokana na mzozo wa kiuchumi uliosambaa duniani. Badala yake aliahidi kupambana na uhalifu na rushwa na mwaka huu kuuendeleza mpango wake wa kijamaa. Alisema pindi yale yaliokwishafanywa yataimarishwa, basi kuanzia mwakani wananchi wa Venezuela watakuwa katika hali ilio bora ya kuufungua mustakbali mpya. Wafuasi wake walimshangilia wakisema CHAVEZ hatokwenda. Kuhusu kura hii ya maoni. alisema:

"Pale tunapotaka hata kufanya mabadiliko madogo ya katiba, basi wananchi lazima wafanye hivyo. Hamna nukuta au koma ibadilishwe bila ya kuitishwa kura ya maoni."

Mtu mmoja alisema:

" Ni rahisi, ni kusema Ndio au Sio, unatia alama vile unavofikiri, na mambo yanakwisha."

Lakini sio kwamba Hugo Chavez anawaamini kabisa wananchi wake. Wakati wa kura hiyo ya maoni, maelfu ya wanajeshi waliwekwa tayari kukandamiza fujo zozote kama zilizotokea wiki zilizopita. Wakati huo wanafunzi walimlaumu Rais kwa kutumia vibaya madaraka yake. Mtawala huyo kabla ya uchaguzi alisema;

" Sisi serekalini, sisi wanamapinduzi, tutaheshimu matokeo, bila ya kujali yatakavokuwa."

Kura hiyo ya maoni haijamhusu Chavez peke yake

Upande wa upinzani umekiri kushindwa, ambako ni kukubwa zaidi kuliko vile ilivotarajiwa kabla ya kura kupigwa. Ulidai kwamba Hugo Chavez alitumia fedha za serekali kufanya mikutano ya hadhara na kuwasafirisha wapiga kura hadi kwenye vituo vya uchaguzi. Chavez analaumiwa anatawala kiimla, akishikilia kutaka kuibadilisha Venezuela iwe sawa na Cuba ya kikoministi. Upande wa upinzani ulidhani utafaidika na manunguniko ya wananchi juu ya uhalifu uliotapakaa nchini, ufisadi wa kiuchumi na rushwa, lakini haukufua dafu. Chavez mwenyewe hajaweka siri juu ya uchu wake wa madaraka, anataka kubakia katika usukani wa uongozi wa nchi hiyo, kama anavosema mwenyewe, ili kuuimarisha ujamaa wake wa karne ya 21. Aliwaambia wafuasi wake kwamba hamna mtu anayeweza kudumu milele, ni Mwenyezi Mungu ndio aliye daima, na nchi yake lazima idumu. Alijisifu kwamba yeye ni mwanajeshi wa umma na kwamba amejitolea kuwa chombo cha kuifanya nchi yake ikamilishe ile mipango alioianzisha tangu alipokamata urais mwaka 1999. Alisema Venezuela ama itabaki kuwa ya kijamaa ama sivyo haitadumu. Lakini watu wengi wanautilia wasiwasi uhalali wa urais wake. Hajaonesha hamu yeyote ya kufikia muwafaka na masikilizano na wapinzani wake. Japokuwa alikiri kushindwa katika kura ya maoni ya kwanza ya Disemba mwaka 2007 iliotaka kuondosha vikwazo vya mihula ya kutawala, si zaidi ya mwaka mmoja baadae ameitisha kura nyingine ya maoni kama ile ya kwanza, na mara hii ameshinda. Ametumia madaraka kamili ya dola, mara nyingine bila ya kujali, ili kuendeleza ajenda yake. Upinzani umeonya juu ya kuchomoza udikteta mpya katika Venezuela. Na katika miaka kumi ya utawala wake amezibadilisha taasisi za nchi, kupitia katiba mpya, na kutumia madaraka makubwa aliyokuwa nayo rais.

Zamani Hugo Chavez alikuwa mwanajeshi wa miavuli aliyeongoza jaribio la mapinduzi lililoshindwa hapo mwaka 1992. Baada kukaa gerezani kwa miaka miwili, alijiingiza katika siasa, akiungwa mkono na wananchi wa Venezuela waliochoshwa na vyama vya kisiasa vya kiasilia katika nchi hiyo iliokuwa moja wapo yenye utawala wa kidemokrasia wa zamani kabisa. Baada ya hapo alikamata madaraka kwa kupitia uchaguzi. Aliweza kunusurika kupinduliwa kutoka madarakani na migomo mikuu miwili dhidi ya utawala wake, na yote ni kwa sababu ya utiifu mkubwa anaoupata kutoka kwa Wanavenezuela walio maskini.

Hugo Chavez alichukuwa madaraka mwaka 1999, akila kiapo kuwaondosha maafisa mafisadi na amepata umaarufu kutokana na mipango yake ya kutumia fedha za serekali kujengea zahanati, shule na kuwapa vyakula maskini. Akimuita rais wa zamani wa Cuba, Fidel Castro, kama baba yake wa kisiasa, Chavez sasa amegeuka kuwa mshika bendera wa mapambano dhidi ya ubwana wa Marekani katika Amerika ya Kusini, akitumia utajiri wa mafuta ya nchi yake kuwasaidia washirika na kuupinga ushawishi wa Kimarekani katika eneo hilo. Fidel Castro alikuwa wa mwanzo kumpongeza Chavez aliyejibu kwamba ushindi huu pia ni wa Castro, watu wa Cuba na wa Amerika ya Kusini.

Jee Chavez anaweza kuvaa kiatu kikubwa cha Fidel wa Cuba, nilimuuliza Ali Sultan, ambaye aliwahi kuwa waziri katika serekali ya mapinduzi ya Zanzibar, na mtu aliyekuwa anafuata sana harakati za kimapinduzi katika Amerika ya Kusini:

Mkuu huyo wa Venezuela ameimarisha maingiliano ya nchi yake na Iran pamoja na Russia, na pia na nchi za karibu, kama vile Ecuador na Bolivia, ambazo zimebadilisha sheria kuzidisha ushawishi wa dola katika uchumi.

Vipi wa-Irani wanavomtathmini Hugo Chavez unapokuja usuhuba wao katika siasa za bei ya mafuta, mwandishi wa habari aliyoko Tehran, Abdul Fattah Musa, aliniambia hivi:

Matokeo haya ya kura ya maoni ya majuzi ni pigo kubwa kwa upinzani katika Venezuela ambao ulishinda katika miji kwenye uchaguzi wa mikoa wa mwaka jana. Katika chaguzi za hapo kabla, upinzani ulidai kwamba kulikuweko udanganyifu.

Wawekezaji wana hofu kwamba Chavez atazimaliza fedha ilizokuwa nazo nchi yake katika kuendeleza miradi yake ya kijamii, licha ya kwamba nchi hiyo sasa inapungukiwa na fedha zinazotokana na mauzo ya mafuta na kwamba thamani ya sarafu ya Venezuela itakwenda chini. Thamani hiyo tangu hapo karibuni imepata pigo kutokana na matumaini kwamba Chavez atabakia madarakani kwa muda mrefu ujao. Wachunguzi wanasema kwamba kila pale Venezuela itakapopungikiwa na mapato ya mafuta, ndipo bashasha ya Chavez mbele ya wananchi wake itakapopungua. Kama Chavez atamfikia Fidel Castro wa Cuba kwa kuitawala nchi yake karibu miaka hamsini ni jambo lisilofikiriwa. Wazi ni kwamba bado ana ushawishi mkubwa huko Venezuela na anazidi kuwavutia walala hoi wa Amerika ya Kusini, kama vile alivokuwa Fidel Castro wakati fulani.