1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vance aelekea Pakistan kwa mazungumzo ya amani na Iran

10 Aprili 2026

Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance ameionya Iran isicheze michezo na Marekani, wakati akielekea Pakistan kwa ajili ya mazungumzo na Iran yanayolenga kumaliza vita kati ya pande hizo mbili.

https://p.dw.com/p/5C0Cu
Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance kabla ya kuelekea Pakistan
Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance kabla ya kuelekea PakistanPicha: Jonathan Ernst/AP Photo/picture alliance

Rais wa Marekani Donald Trump amempa jukumu kiongozi huyo, mwandani wake ambaye ameonekana kuwa mwenye kusitasita zaidi kuunga mkono vita hivyo vya wiki sita dhidi ya Iran, kutafuta suluhu ya mgogoro huo na kuzuia kile kilichoelezwa kuwa tishio la rais huyo la kuufuta "ustaarabu mzima” wa Iran.

Vance, ambaye kwa muda mrefu amekuwa mpinzani wa uingiliaji wa kijeshi wa Marekani nje ya nchi na mkosoaji wa wazo la kutuma wanajeshi kwenye migogoro isiyo na kikomo cha muda, alianza safari leo hii kwenda kuongoza mazungumzo yaliyoratibiwa na wapatanishi na Iran mjini Islamabad, mji mkuu wa Pakistan.

JD Vance: Nadhani yatakuwa mazungumzo mazuri

Zaidi Vance anaeleza "Nadhani yatakuwa mazungumzo mazuri, lakini bila shaka tutaona yatakavyoendelea. Kama Rais wa Marekani alivyosema, ikiwa Wairani wako tayari kujadiliana kwa nia njema, sisi bila shaka tuko tayari kuonyesha dhamira njema kwa mazungumzo. Lakini ikiwa watajaribu kutuchezea, basi watagundua kwamba timu ya mazungumzo haitakuwa tayari kupokea hilo. Kwa hiyo tutajaribu kufanya mazungumzo yenye mwelekeo chanya. Rais ametupa miongozo iliyo wazi kabisa, na tutaona yatakakokuwa.”

Kiongozi Mkuu mpya wa Iran, Mojtaba Khamenei.
Kiongozi Mkuu mpya wa Iran, Mojtaba Khamenei.Picha: Hamed Jafarnejad/ISNA/WANA/REUTERS

Ziara ya Vance inafanyika wakati ambapo makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano yanaonekana kuwa hatarini kuvunjika.

Wigo wa pengo la madai ya Iran na Marekani

Pengo kati ya madai ya Iran liko wazi na yale ya Marekani pamoja na mshirika wake, Israel, linaonekana kuwa gumu kuzibwa. Wakati huo huo, nchini Marekani ambako Vance anaweza kuwaomba wapiga kura baada ya miaka miwili wamchague kuwa rais ajaye kuna shinikizo linaloongezeka kisiasa na kiuchumi kumaliza mgogoro huo haraka.

Vance ameandamana na mjumbe maalum wa Trump, Steve Witkoff, pamoja na mkwe wa rais, Jared Kushner, ambaye awali alishiriki katika duru tatu za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na wajumbe wa Iran. Mazungumzo hayo yalilenga kushughulikia wasiwasi wa Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, makombora ya masafa marefu, na msaada wake kwa makundi yenye silaha Mashariki ya Kati, kabla ya Trump na Israel kuanzisha vita dhidi ya Iran Februari 28 mwaka huu.

Starmer: Marekani iniihitaji NATO

Na katika hatua nyingine Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesisitiza Ijumaa kwamba uwepo wa jumuiya imara ya NATO ni katika maslahi ya Marekani, alipokuwa akihitimisha ziara ya siku tatu katika eneo la Ghuba kujadili namna ya kuimarisha makubaliano tete ya kusitisha mapigano Mashariki ya Kati.

Zaidi Starmer anaeleza "Maslahi ya Marekani, yapo pia katika maslahi ya Ulaya. Unajua, NATO ni muungano wa kujilinda ambao kwa miongo mingi umetufanya tuwe salama zaidi kuliko ambavyo tungekuwa kabla. Kwa hiyo sisi ni waungaji mkono thabiti wa NATO, na tutabaki kuwa waungaji mkono thabiti zaidi wa NATO daima.

Kauli ya Starmer inatokana na  mashambulizi mapya ya wiki hii kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump dhidi ya muungano huo wa kijeshi wa mataifa ya Magharibi, pamoja na vitisho vyake vya kujitoa NATO, baada ya washirika wa NATO kukataa kujiunga na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.