Uturuki yaishambulia IS ndani ya Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.07.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Uturuki yaishambulia IS ndani ya Syria

Ndege za Uturuki zimezishambulia ngome za kundi linalojiita Dola la Kiislamu, au IS ndani ya Syria kulipiza kisasi shambulizi la jana kwenye kituo cha jeshi la Uturuki lililomuuwa mwanajeshi mmoja

Ndege chapa F-16 zinazotumiwa na Uturuki kuiadhibu IS.

Ndege chapa F-16 zinazotumiwa na Uturuki kuiadhibu IS.

Hatua hii ya mashambulizi dhidi ya IS inaashiria mabadiliko makubwa ya kimkakati kwa Uturuki, ambayo siku za nyuma ilikuwa inasitasita kujiunga na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani dhidi ya kundi lijiitalo Dola la Kiisamu.

Afisa wa serikali ya Uturuki amesema ndege tatu chapa F-16 zimeondoka katika kituo cha Diyarbakir kusini mashariki mwa nchi mapema leo, na kutumia kile alichokiita 'mabomu safi' kulenga vituo vitatu vya IS. Afisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema miongoni mwa vituo vya IS vilivyoshambuliwa, viwili ni vya kuratibu mapigano, na cha tatu ni cha mapokezi kwa ajili ya watu wanaojiunga na kundi hilo lenye itikadi kali.

Ingawa hakuna tamko rasmi kutoka upande wa serikali kuthibitisha mahali vilipo vituo vya IS vilivyoshambuliwa, vyombo vya habari nchini Uturuki vimesema vipo katika kijiji cha Havar nchini Syria, karibu na mpaka baina ya nchi mbili.

Wanamgambo wauawa

Shambulizi la kujitoa muhanga la IS katika mji wa Suruc limeivuta Uturuki ndani ya mzozo

Shambulizi la kujitoa muhanga la IS katika mji wa Suruc limeivuta Uturuki ndani ya mzozo

Shirika binafsi la habari la Dogan limeripoti kuwa wapiganaji 35 wa IS wameuawa katika mashambulizi hayo, lakini halikutaja chanzo cha taarifa hizo.

Tangazo la serikali mjini Ankara limesema uamuzi wa kufanya mashambulizi hayo ulifikiwa katika mkutano wa kiusalama uliofanyika jana Alhamis, baada ya wanamgambo watano wa IS kufanya mashambulizi ya bunduki kutoka upande wa Syria, na kumuuwa mwanajeshi wa Uturuki.

Uturuki yavutwa ndani ya mzozo

Mapema wiki hii, Uturuki iliiruhusu Marekani kutumia uwanja wake wa ndege wa Incirlik karibu na mpaka wa Syria, kufanya mashambulizi dhidi ya IS, hii ikiwa ni kwa mujibu wa afisa wa ngazi ya juu wa Marekani.

Hivi karibuni Uturuki imejikuta ikibururwa katika mzozo unaoihusha IS. Mwanzoni mwa juma hili, mshambuliaji wa kujitoa mhanga wa kundi hilo aliwauwa watu 32 katika mji ulio karibu na mpaka wa Syria. Maafisa wa nchi hiyo wanaamini kuwa mashambulizi hayo ni jibu la IS kwa operesheni ambayo Uturuki imeianzisha dhidi ya wafuasi wa kundi hilo kwenye ardhi yake.

Taarifa za hivi punde zimeeleza kuwa msako mkali ulioendeshwa leo katika mikoa 13 ya Uturuki, umewakamata wanamgambo wa kiislamu na kikurdi wapatao 250.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com