Assad azilaumu Uturuki,Saudia,na Qatar | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.04.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Assad azilaumu Uturuki,Saudia,na Qatar

Rais wa Syria Bashar al Assad amezilaumu Uturuki,Saudi Arabia na nchi nyingine za Mashariki ya kati kwa kuchangia kuyasaidia makundi ya itikadi kali nchini Syria na kusababisha makundi hayo kupata nguvu.

Wapinzani wa serikali ya Assad wakishikilia bendera ya kundi la al Nusra Front ambalo ni tawi la IS,Idlib

Wapinzani wa serikali ya Assad wakishikilia bendera ya kundi la al Nusra Front ambalo ni tawi la IS,Idlib

Katika mahojiano yaliyochapishwa Ijumaa(17.04.15) na gazeti moja la Sweden rais Assad amesema kudhibiti kwa mji mkuu wa mkoa wa kaskazini magharibi wa Idlib mwishoni mwa mwezi Marchi kumetokana hatua ya Uturuki kuwasaidia waasi kwa njia za kijeshi na kiusafiri pamoja na msaada wa hata wa kifedha uliotoka nchi za Saudi Arabia na Qatar.

''Ikiwa tunataka kuuangalia mgogoro wa Syria kama mgogoro tu wa ndani kati ya makundi ndani ya Syria huo utakuwa sio ukweli halisi na hiyo siyo haki.Kwa hakika tatizo sio gumu hivyo lakini linakuwa gumu kwasababu ya mgogoro huu umeingiliwa na watu kutoka nje.''

Rais Bashar al Assad

Rais Bashar al Assad

Rais Assad ameongeza kusema katika vita vya aina yoyote ile hapana budi jeshi linaweza kuzidiwa nguvu hata likiwa na uwezo kiasi gani lakini katika mgogoro wa nchi yake kudhibitiwa kwa mji wa Idlib na waasi kumetokana na nguvu za nje.Hata hivyo msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Uturuki Tanju Bilgic akijibu Tuhuma hiyo amesema hakuna ukweli wowote juu ya madai kwamba jeshi la Uturuki limewasaidia waasi kuutwaa mji huo wa Idlib.

Mgogoro wa Syria unakadiriwa kusababisha vifo vya watu 220,000 huku rais Assad akipoteza udhibiti wa sehemu kubwa ya kaskazini na mashariki na kubakia na nguvu kwenye miji mikubwa ya magharibi kwa msaada wa washirika wake ikiwemo Iran na kundi la Hezbollah.

Pamoja na hayo wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa walijawa na majonzi na wengine kufikia kububujikwa machozi jana wakati shahidi wa kwanza akisimulia kwa kuonyesha picha kuhusu watoto waliokufa kufuatia mashambulizi ya silaha za sumu yaliyofanywa dhidi ya raia nchini Syria.Shahidi huyo ambaye ni Daktari wa Syria,Mohammed Tenari alihusika kuwatibu katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita wahanga waliojeruhiwa kufuatia shambulio la silaha za sumu linalodiwa kufanywa na serikali ya Assad.

Katika ushahidi wake alionyesha mkanda wa Video wa shambulio linalotuhumiwa kuwa la silaha za kemikali ya Chlorine lililofanywa Marchi 16 katika mji anakotokea wa Sarmin mkoa wa Idlib ambapo ilionyesha watoto watatu wenye umri wa kati ya mwaka na miaka 3 wakikata roho licha ya kufanyika juhudi za kuokoa maisha yao.

Samantha Power Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa

Samantha Power Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa

Video hiyo ilimuonyesha mmoja kati ya watoto hao watoto akiwa amefariki akiwa juu ya kifua cha bibi yake.Tenari atakutana leo na ujumbe wa Urusikatika Umoja wa Mataifa katika wakati ambapo Marekani na wanachama wengine wa baraza la usalama wanajaribu kuwashawishi washirika hao wakubwa wa serikali ya Syria kutotumia kura ya Turufu dhidi ya hatua zinazopangwa kuchukuliwa katika mgogoro huo wa miaka minne.

Pamoja na hayo lakini inatajwa kwamba kuanzia mwezi ujao mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria,Staffan De Mistura anapanga kushauriana na pande zinazohusika kwenye mgogoro huu kuhusu duru nyingine ya amazungumzo ya amani ingawa hatua hii mara zote imekuwa ikishindwa kupiga hatua tangu vita vilipoanza.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com