Utata sera ya silaha ya Ujerumani | Magazetini | DW | 25.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Utata sera ya silaha ya Ujerumani

Wahariri wanahoji ikiwa sera ya Ujerumani ya silaha kuelekea maeneo yenye migogoro inakiukwa katika wakati ambapo Umoja wa Ulaya umeyaruhusu mataifa wanachama kulisaidia jeshi la Pashmerga, Iraq.

Wanajeshi wa kikosi cha Peshmerga kaskazini mwa Iraq.

Wanajeshi wa kikosi cha Peshmerga kaskazini mwa Iraq.

Gazeti la Rheinische Post linazungumzia mkanganyiko uliopo baina ya hatua ya kuwafikishia silaha wapiganaji wa serikali nchini Iraq na sera ya silaha ya Ujerumani kuelekea maeneo yenye migogoro.

Utata huo umeibuliwa na Waziri wa Kazi, Andrea Nahles kutokea chama cha SPD, ambaye amesema hatua hii kwa hakika inavunja miiko ya Ujerumani, lakini kwa maneno yake: “kwanza, hali iliyopo kaskazini mwa Iraq hivi sasa ni tafauti, maana kuna watu huko wanaoteseka na wanaohitaji msaada, na pili ni uamuzi wa Umoja wa Ulaya ambayo Ujerumani ni sehemu yake". Lakini pia anaonya Waziri huyo kwamba hili lisije likageuzwa kuwa ndicho kigezo cha kufuatwa kwa kila mahala.

Obama baina ya Iraq na Syria

Mhariri wa Mittelbayerische Zeitung analizungumzia pia suala hilo hilo la Iraq lakini kwa kuangazia sera ya Rais Barack Obama wa Marekani katika mzozo huu uliovuuka mpaka kutokea Syria. Mhariri anasema Rais Obama anapaswa kuziangalia Iraq na Syria katika uhalisia wake.

Rais Barack Obama wa Marekani.

Rais Barack Obama wa Marekani.

Mashambulizi ya anga dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, yakisaidiwa na kuongezwa nguvu kwa vikosi vya ardhini Iraq, anahoji mhariri huyo, yanaweza tu kuleta mafanikio ya kitambo, kama vile kulichukuwa tena bwawa la Mosul, na yumkini kuwazuia wanamgambo hao kusonga mbele, lakini si zaidi ya hapo.

Hakuna anayeujuwa ukweli zaidi kuliko mkuu wa majeshi wa Marekani, Martin Dempsey, kwamba suluhisho la kudumu dhidi ya Dola la Kiislamu haliko tu kwenye viunga vya kaskazini mwa Iraq, bali liko lilikoanzia, kaskazini mashariki mwa Syria.

Mhariri anahoji kwamba kama alivyokuwa Saddam Hussein wa Iraq, ndivyo alivyo sasa Bashar al-Assad wa Syria. Wote ni dhidi ya demokrasia, wote ni dhidi ya siasa kali za kidini. George Bush alimuondosha mmoja. Mmoja bado yupo madarakani, lakini amepoteza udhibiti wa baadhi ya maeneo ambayo pengo lake limejazwa na waasi wa Dola la Kiislamu.

Merkel akosolewa kuhusu Urusi

Tumalizie kwa maoni ya mhariri wa gazeti la Neue Westfälische ambaye anamnukuu aliyekuwa mshauri wa sera za nje wa Kansela Helmut Kohl, Horst Teltschik, akimkosoa Kansela wa sasa, Angela Merkel, kwa sera zake kuelekea Urusi.

Teltschik haamini kwamba vikwazo dhidi ya Urusi vinafanya kazi. Kwa maneno yake, Warusi hawaadhibiki kwa vikwazo maana wamezowea mateso.

"Jambo pekee linaloweza kusaidia, anasema mwanasiasa huyo mkongwe, ni majadiliano ya kisiasa na mashirikiano," alisisitiza Teltschik.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Vyanzo: Rheinische Post, Neue Westfälische, Osnabrücker Zeitung
Mhariri: Josephat Charo