1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaongezewa shinikizo la kuondoa wanajeshi wake

14 Februari 2022

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amezidi kuishinikiza Urusi kupunguza kitisho cha uvamizi kwa Ukraine na kuonya tena kwamba itakabiliwa na adhabu kali iwapo itamvamia jirani yake huyo.

https://p.dw.com/p/46ys9
Wahl des Bundespräsidenten | Bundeskanzler Olaf Scholz
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Mvutano kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi juu ya madai ya kitisho cha uvamizi wa Urusi nchini Ukraine unazidi kushika kasi. Hii leo Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amezidi kuishinikiza Urusi kupunguza kitisho hicho kwa Ukraine na kurejea tena onyo lililotolewa na magharibi mara kadhaa kwamba itakabiliwa na adhabu kali iwapo itamvamia jirani yake huyo. Anasema hayo wakati Marekani ikisisitiza uvamizi huo uko karibu mno. 

Wakati anaanza safari yake kuelekea Moscow kwa mazungumzo na rais Vladimir Putin ili kuangazia suluhu ya kidiplomasia, kansela Olaf Scholz ameandika kupitia ukurasa wake wa twitter, akiishinikiza Urusi kuashiria kuwaondoa wanajeshi wake kwenye mipaka ya Ukraine. Scholz anataraji kukutana na Putin hapo kesho katika ikulu ya Kremlin.

Hapo jana kansela Scholz alionya kuhusu vikwazo vikali dhidi ya Urusi iwapo itaivamia Ukraine. Ingawa afisa mmoja amesema jana mjini Berlin kwamba hawatarajii kitu chochote kikubwa kufikiwa, lakini amesema Ujerumani bado inaamini diplomasia ina umuhimu mkubwa kwenye mvutano huu.

Soma Zaidi: Ujerumani, Ufaransa na Poland zaazimia kuepusha vita Ulaya

Katika hatua nyingine, Ukraine imeomba mkutano wa dharura na Urusi na mataifa kadhaa ya Ulaya ili kuelezea hatua ya Moscow ya kuwaweka wanajeshi wake kwenye mipaka yake. Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dymitro Kuleba ameandika kupitia ukurasa wake wa Facebook jana usiku kwamba Urusi ilipuuza ombi lake rasmi la kuitaka kuelezea kuhusiana na hatua ya kuwarundika wanajeshi wake na hata kuongeza silaha mipakani mwake.

Außenministerin Baerbock in der Ukraine | PK mit Außenminister Dmytro Kuleba
Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dymitro Kuleba(Kulia) akiwa na waziri wa mambo na nje wa Ujerumani Annalena Baerbock.Picha: Gleb Garanich/Reuters/AP/dpa/picture alliance

Ukraine inataka kufanyika kwa mkutano hao katika kipindi cha masaa 48. Hata hivyo Moscow haikupatikana mara moja kuzungumzia ombi hilo la Kuleba wakati wasiwasi ukiongezeka kuhusiana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Marekani yasisitiza Urusi itaivamia Ukraine hivi karibuni.

Huko Washington, mshauri wa masuala ya usalama wa rais Joe Biden Jake Sullivan, yeye anasisitiza kwamba Urusi itaivamia Ukraine siku yoyote kuanzia sasa, ingawa bado anasema hawajajua bado ni lini hasa. Alikuwa akizungumza na kituo cha utangazaji cha CNN. Maafisa wengine wa Marekani walisema bado hawawezi kuthibitisha ripoti kwamba taarifa za kiintelijensia za taifa hilo zinaashiria kwamba Urusi ilipanga kuivamia Ukriane siku ya Jumatano.

Soma Zaidi: Biden aiapiza Urusi hatua kali na za haraka ikiivamia Ukraine

Uingereza inayokubaliana na Marekani kuhusiana na uvamizi wa Urusi, imesema kupitia msemaji wake kwamba inashughulikia namna ya kuisaidia Ukraine kijeshi na kiuchumi na itatangaza msaada huo siku chache zijazo, wakati waziri mkuu Boris Johnson akijiandaa kuzuru Ulaya baadae wiki hii kuongeza nguvu za kumaliza mvutano uliopo na Urusi.

Taarifa za muda mfupi uliopita zimesema, Ujerumani inapeleka wanajeshi zaidi nchini Lithuania, wakati kitisho cha uvamizi kikiimarika. Malori mengi yaliyokuwa na wanajeshi wa ziada yameondoka mjini Münster mapema leo, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la DPA. Inasemekana kwamba Ujerumani inapeleka wanajeshi takriban 350 zaidi na magari karibu 100, kusaidia wanajeshi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO walioko Lithuania

Mashirika: AFPE/RTRE