1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi lazima ichague suluhu katika mzozo na Ukraine

Tatu Karema
10 Februari 2022

Katibu mkuu wa jumuiya  ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg, amesema kuwa Urusi lazima ichague kati ya suluhu ya kidiplomasia katika mzozo na Ukraine ama ikabiliwe na vikwazo vya kiuchumi kutoka mataifa ya Magharibi.

https://p.dw.com/p/46ohu
NATO-Russland Rat tagt in Brüssel
Picha: Alexey Vitvitsky/Sputnik/picture alliance/dpa

Stoltenberg amesema iwapo Urusi itachagua njia ya kidiplomasia, jumuiya hiyo iko tayari kukaa nayo chini  katika mazungumzo na iwapo itachagua hatua ya makabiliano, itakabiliwa na vikwazo vikali zaidi na pia kuongezeka kwa uwepo wa vikosi vyake vya  kijeshi katika eneo la Mashariki mwa jumuiya hiyo akisisitiza kwamba Uingereza ni mdau muhimu katika suala hilo.

Stoltenberg amesema haya Alhamisi ( 10.02.2022) wakati wa mkutano wa pamoja wa wanahabari na waziri mkuu wa Uingereza Borris Johnson mjini Brussels: Pia ameongeza kuwa wanafuatilia kwa karibu kupelekwa kwa vikosi vya kijeshi vya Urusi nchini Belarus ambavyo ni vingi mno tangu kumalizika kwa vita baridi na kwamba huu ni wakati hatari kwa usalama wa bara Ulaya. Stoltenberg amesema idadi ya vikosi vya Urusi inaongezeka na muda wa tahadhari kwa uwezekano wa mashambulizi unayoyoma.

Russland Moskau | Pressekonferenz Außenministerin Annalena Baerbock und Sergej Lawrow
Sergey Lavrov - Waziri mkuu wa UrusiPicha: SNA/imago images

Wakati huo huo, wakati wa mazungumzo kati ya mawaziri wa nje wa Uingereza Liz Truss na mwenzake wa Urusi Sergey Lavrov ambayo ni ya kwanza kwa mkutano wa wajumbe wakuu wa mataifa hayo mawili katika muda wa zaidi ya miaka minne, Truss ameihimiza Urusi kuondoa hofu kuhusiana na Ukraine na kuzingatia demokrasia hata baada ya maelfu ya wanajeshi wa Urusi kushiriki katika luteka ya kijeshi nchini Belarus karibu na mpaka na Ukraine hali iliyoibua wasiwasi katika mataifa ya Magharibi kuhusu uwezekano wa uvamizi.

Truss asisitiza kuhusu athari mbaya kwa Urusi iwapo itaishambulia Ukraine

Kwa mara nyingine tena, Truss aliionya Urusi kwamba kushambulia taifa hilo jirani kutakuwa na athari mbaya huku akiihimiza kuzingatia makubaliano ya kimataifa yanayoihitaji kuheshimu uhuru wa Ukraine. Katika kujibu, Lavrov amesisitiza kuwa Urusi haitakubali kukemewa na mataifa ya Magharibi. Lavrov ameongeza kuwa mitazamo ya itikadi na kauli za vitisho ni njia isiyoelekea popote. Lavrov pia alikataa ombi la Truss la kuondoa vikosi vya kijeshi vya nchi hiyo katika eneo hilo la mpaka na Ukraine na kusema ombi hilo halistahili na kutaja kuongezeka kwa wanajeshi wa Uingereza na NATO katika eneo la Mashariki mwa Ulaya. Lavrov amesema kuwa hawataki kumtishia mtu yeyote na kwamba wao ndio wanaokabiliwa na vitisho. Waziri huyo mkuu amedai kuwa wanasiasa wa mataifa ya Magharibi wanachochea hofu kuhusiana na Ukraine kwa sababu za kisiasa.