1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Urusi inaweza kuivamia Ukraine muda wowote

Grace Kabogo
12 Februari 2022

Marekani imeonya kuwa Urusi inaweza kuivamia kijeshi Ukraine muda wowote. Mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani, Jake Sullivan amesema uvamizi huo unaweza ukaanza kwa makombora na mashambulizi ya anga.

https://p.dw.com/p/46uaN
Belarus | Militärmanöver mit Russland
Picha: Viktor Tolochko/Sputnik/dpa/picture alliance

Tangazo la Marekani linatokana na taarifa mpya za kijasusi kuhusu kuongezeka kwa wanajeshi wa Urusi kwenye mipaka ya Ukraine katika wiki moja iliyopita.

Akizumgumza na waandishi habari katika Ikulu ya Marekani, Sullivan amesema huo ni ujumbe wa dharura kwa sababu wako katika hali ya dharura. Amesema Urusi ina majeshi yote inayohitaji kufanya mashambulizi makubwa ya kijeshi na nchi hiyo inaweza kuchagua ndani ya kipindi kifupi kuanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Ukraine. Amesema uvamizi kama huo unaweza ukaanzia kwa kuushambulia mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.

Huku wasiwasi ukiongezeka, Rais wa Marekani, Joe Biden Jumamosi anatarajiwa kuzungumza kwa njia ya simu na Rais wa Urusi, Vladmir Putin kuhusu kuongezeka kwa mzozo huo. Mazungumzo kati ya Putin na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron pia yanatarajiwa kufanyika.

Bildkombo Biden und Putin
Rais wa Marekani, Joe Biden na Rais wa Urusi, Vladimir Putin Picha: Jim WATSON/Grigory DUKOR/AFP

Hata hivyo, Urusi imerudia kukanusha mipango yoyote ya kuivamia Ukraine. Licha ya kukanusha huko, nchi kadhaa ikiwemo Marekani, Uingereza, Australia, Canada, Norway, Denmark, New Zealand, Japan na nchi nyingine za Ulaya zimewataka raia wake kuondoka Ukraine mara moja.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jen Psaki amewaambia waandishi habari kwamba wanatambua Rais Putin anafanya uamuzi wa kuivamia Ukraine, hivyo kutakuwa na mazingira magumu kwa raia wa Marekani walioko Ukraine. ''Tunataka kuweka wazi hatari iliyopo kwa raia wetu, kwa raia yeyote ambaye atabakia ndani ya Ukraine,, alifafanua Psaki.

Marekani yaihakikishia Ukraine kuhusu uhuru wake

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken amesema vikosi vya Urusi vinaweza kuivamia Ukraine muda wowote. Akizungumza kwa njia ya simu na waziri mwenzake wa Ukraine, Dmytro Kuleba, Blinken amemuhakikishia kwamba Marekani itaendelea kuiunga mkono uhuru na uadilifu wa Ukraine.

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amezungumza kwa njia ya simu na Blinken, Macron pamoja na Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau, huku viongozi hao wakithibitisha umuhimu wa kuweka vikwazo vikali na vya haraka iwapo Urusi itaivamia Ukraine.

Deutschland | Bundeskanzler Scholz trifft Spitzen der drei baltischen Länder
Kansela wa Ujerumani, Olaf ScholzPicha: Christophe Gateau/AFP

Serikali ya Ujerumani imesema juhudi zote za kidiplomasia ni kuishawishi Urusi kupunguza mvutano, huku lengo kuu likiwa kuzuia vita barani Ulaya. Scholz anatarajia kuelekea Ukraine siku ya Jumatatu kujadiliana hatua za pamoja na madhubuti kukabiliana na vitisho.

Katibu Mkuu wa Jumuia ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg amesema muungano huo umejiandaa kwa hali yoyote ile. Ijumaa, wizara ya ulinzi ya Marekani ilisema Rais Biden ameamuru kupelekwa wanajeshi zaidi 3,000 nchini Poland mbali na 1,700 ambao tayari wako nchini humo, ili kuimarisha vikosi vya NATO vilivyoko huko.

Wanajeshi walioko Ujerumani pia kuhamishwa

Jeshi la Marekani pia linawahamisha wanajeshi 1,000 kutoka Ujerumani kwenda Romania, ambayo kama ilivyo Poland inapakana na Ukraine.

Mkuu wa Majeshi, Jenerali Mark Milley Ijumaa alizungumza kwa simu na mwenzake wa Urusi, Jenerali Valery Gerasimov. Ofisi ya Milley haikutoa maelezo zaidi kusuhu kilichozungumzwa zaidi ya kusema makamanda hao wawili walijadiliana masuala kadhaa yanayohusiana na usalama.

Jenerali Milley alizugumza pia kwa njia ya simu na wenzake kutoka nchi za NATO, ikiwemo Canada, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Italia, Poland na Romania.

(AFP, DPA, AP, Reuters)