1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi: Marekani iliagiza Kremlin ishambuliwe kwa droni

4 Mei 2023

Urusi Alhamis imeituhumu Marekani kwa kuhusika katika shambulizi la droni lililonuiwa kumuua Rais Vladimir Putin katika ikulu ya Kremlin.

https://p.dw.com/p/4Qudm
Moskau Kreml angebliche Drohnen-Attacke
Picha: Ostorozhno Novosti/REUTERS

Lakini Marekani kupitia msemaji wa baraza la kitaifa la usalama la White House John Kirby, imekanusha hayo.

Siku moja baada ya kuilaumu Ukraine kwa kile ilichokiita shambulizi la kigaidi, Kremlin sasa imeigeukia Marekani na kuinyoshea kidole cha lawama bila kutoa ushahidi wowote.

Msemaji wa Rais Vladimir Putin, Dmitry Peskov amesema Marekani bila shaka ilihusika na tukio hilo.

"Tunajua kwamba mara nyingi maeneo yanayolengwa na mashambulizi hayachaguliwi na Kyiv, yanachaguliwa Washington kisha Kyiv inapewa taarifa ili ifanye mashambulizi. Kyiv haina haki ya kuchagua jinsi shambulizi litakavyofanywa, hilo pia linafanyika nje. Tunajua hili vyema kabisa," alisema Peskov.

Russland | Dmitri Peskow
Dmitry Peskov msemaji wa Rais Vladimir PutinPicha: Valery Sharifulin/TASS/dpa/picture alliance

Wakati wa Zelenskiy kuangamizwa

Lakini katika mahojiano na kituo cha habari cha Marekani cha MSNBC, msemaji wa baraza la kitaifa la usalama la White House John Kirby amesema, Marekani haihusiki kivyovyote na kwamba Peskov anasema uongo. Kirby amesema kuwa Marekani haiungi mkono Ukraine kufanya mashambulizi nje ya mipaka yake.

Lakini Urusi imesema ina haki ya kulipiza kisasi na watu walio na misimamo mikali nchini humo akiwemo rais wa zamani Dmitry Medvedev, wamesema sasa Urusi inastahili "kumuangamiza" Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy. Ila Peskov amekataa kusema iwapo Zelenskiy ni mtu wanayemlenga katika mashambulizi yao.

Hayo yakiarifiwa, Rais Zelenskiy katika ziara yake nchini Uholanzi Alhamis, amesema, ana uhakika kwamba Rais Putin atafikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu, Ukraine itakapovishinda vita hivyo ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Katika hotuba iliyopewa kichwa, "Hakuna amani bila haki kwa Ukraine" aliyoitoa mjini The Hague, mji ulio na mahakama ya ICC, Zelenskiy amesema Putin anastahili kuhukumiwa kwa uhalifu wake katika mahakama hiyo.

"Na nashukuru kwamba mji wa The Hague unaohusishwa na sheria ya kimataifa duniani, unakuwa mji wa haki. Haki kwa wale wote walioteseka kutokana na uchokozi na uhalifu mwengine wa kimataifa. Huu ndio mwaka wa ushirikiano wetu na nyinyi," alisema Zelenskiy.

Niederlande l Premierminister Mark Rutte empfängt den ukrainischen Präsidenten Selenski
Volodymyr Zelenskiy akiamkuana na Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark RuttePicha: Yves Herman/REUTERS

Kuvujishwa kwa ziara ya Zelenskiy Ujerumani

Hotuba ya Zelenskiy ilikuwa ni wito wa kutaka kufunguliwa kikamilifu kwa mashtaka ya uchokozi katika kikao maalum. Lakini kisheria mahakama ya ICC haiwezi kufungua mashtaka ya uchokozi wa kuanzisha vita.

Kwengineko polisi ya Ujerumani katika taarifa imesema itaanzisha uchunguzi baada ya taarifa kuhusiana na ziara ya Rais Zelenskiy nchini Ujerumani, kuvujishwa katika vyombo vya habari.

Gazeti moja nchini humo liliripoti kwamba polisi ya Ujerumani inajiandaa kwa ziara ya Zelenskiy mjini Berlin katikati ya mwezi Mei. Tovuti ya habari ya Ujerumani ya T-Online imeripoti kwamba maafisa wa Ukraine wamevunjwa moyo na hatua ya kuvujishwa kwa taarifa hizo.

Vyanzo: AFP/AP/Reuters