Umoja wa Nchi za Bahari ya Mediterrenean | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Nchi za Bahari ya Mediterrenean

Jana nchi za Umoja wa Ulaya pamoja na zile za Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya Kati ziliunda mjini Paris Umoja wa nchi za Bahari ya Mediterrenean.

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa(kushoto) na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa(kushoto) na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani


Umoja huo umetokana na fikra ya Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa, ambaye hivi sasa anashikilia urais wa Baraza la Umoja wa Ulaya. Nini kinachotarajiwa kutokana na Umoja huo?

Ulikuwa mkutano wa kilele wa mbwembwe nyingi, maneno mengi na makubwa, ahadi na ishara kubwa kubwa. Katika jengo ambalo limekuwa la maonyesho ya dunia tangu mwaka 1900, jengo la kuvutia ambalo haliko mbali na fukwe za Mto Seine, walikaa pamoja katika meza moja wakuu wa nchi na serekali 27 kutoka Umoja wa Ulaya pamoja na nchi nyingine zinazopakana na Bahari ya Mediterrenean. Hilo peke yake ni fanikio kubwa kwa Nicolas Sarkozy.

Kumetolewa mapendekezo mengi huko Paris: kwanza, Bahari ya Mediterrenean iwe safi zaidi, nishati ya juwa inayopatikana katika nchi zilizo kusini mwa bahari hiyo itumiwe kwa nguvu zaidi, na kuweko utaratibu mzuri zaidi wa misafara ya meli katika bahari hiyo. Na bila ya shaka, kutokana na kuimarika ushirikiano baina ya nchi zinazopakana na bahari hiyo, Rais Nicolas Sarkozy anatumai uhamiaji haramu wa watu kuoka Afrika Kaskazini kwendea Ulaya utapungua.

Nicolas Sarkozy wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita mwaka jana huko Ufaransa aliitangaza fikra yake hiyo ya kuunda Umoja wa Nchi za Bahari ya Mediterrenean. Kutoka ile ndoto yake ya zamani ya kuwa tu na Umoja wa nchi za Bahari ya Mediterrenean hakujabakia mengi. Hasa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, alikuwa na wasiwasi na umoja kama huo. Kansela alifanikiwa kuyashikilia maoni yake kwamba Umoja wa Nachi za Bahari ya Mediterrenean unaweza tu kuweko chini ya kivuli cha taasisi za sasa za Umoja wa Ulaya. Hiyo ina maana kwamba mwishowe huko Paris fikra hiyo ya mwanzo ya Rais Sarkozy iliingizwa katika ule ushirika ulioundwa mwaka 1995 baina ya Umoja wa Ulaya na nchi za Bahari ya Mediterrenean. Sasa ushirika huo unatakiwa kupigwa jeki na kupewa hadhi ya juu zaidi. Hilo lilikuwa ni pigo chungu kwa rais huyo wa Ufaransa.

Lakini Nicolas Sarkozy aligundua njia mpya kuupa mkutano huo wa kilele umuhimu wa kisiasa. Alilitumia jukwaa hilo kuupiga jeki mwenedo wa amani wa Mashariki ya Kati. Hata kabla ya kuanza mkutano huo wa kilele, alikutana na Rais Bashar al-Assad wa Syria na rais mpya wa Lebanon, Michel Suleiman. Mwisho wa mazungumzo yao, marais hao wa Kiarabu walitangaza kwamba nchi zao zitabadilishana mabalozi na kufungua balozi katika mji mkuu wa kila nchi, yaani Damascuss na Beirut. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa nchi hizo kufanya hivyo tangu zilipopata uhuru katika miaka ya arbaini. Na jana Nicolas Sarkozy aliweza kwa fahari kutoka hadharani na waziri mkuu wa Israel na rais wa Wapalastina na kuwatia mori wasonge mbele na juhudi zao za kutafuta amani baina ya nchi zao. Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, alisisitiza kwamba Israel haijawahi kuwa karibu na kufikia mapatano ya amani na Wapalastina kama ilivo sasa. Nicolas Sarkozy naye aliitumia nafasi hiyo ya jana kuweka wazi kwamba yeye, akiwa rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, atatumia juhudi zaidi kuliko kuwa mwanasiasa tu kuupeleka mbele mwenendo huo wa kutafuta amani ya Mashariki yaq Kati.

Naam, kwa uchache mkutano huo wa Paris ulikuwa wa kupongezana na kila mmoja akatangaza nia yake njema. Kilichobaki tu ni kungoja kipi ambacho kitatekelezwa. Hii itakuwa sio mara ya kwanza kwa mkutano wa mbwembewe kama huo kutofuatilizwa na vitendo.
 • Tarehe 14.07.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EcPo
 • Tarehe 14.07.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EcPo
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com