1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya na Marekani kujadili utata wa mkataba wa Iran

John Juma
18 Februari 2021

Wanadiplomasia wakuu wa Ulaya na Marekani wanatarajiwa kufanya mazungumzo Alhamisi kuhusu namna ya kuufufua mkataba wa mwaka 2015 kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

https://p.dw.com/p/3pWo0
Brüssel Treffen EU Außenminister Maas und Le Drian
Picha: Reuters/S. Lecocq

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian atakuwa mwenyeji wa mkutano huo mjini Paris utakaohudhuriwa na mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani na Uingereza huku mwenzao wa Marekani Antony Blinken akitarajiwa kujiunga nao kwa njia ya video. Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa ilisema hayo jana Jumatano.

Kwenye taarifa, msemaji wa kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameeleza kwamba Merkel amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na rais wa Iran Hassan Rouhani kuzungumzia wasiwasi wake kwamba Iran inashindwa kutimiza ahadi zake kwa mujibu wa mkataba huo.

Soma pia: Iran yataka Umoja wa Ulaya usuluhishe mzozo wa nyuklia

Katika mazungumzo yake na Rouhani, Merkel alisema muda umewadia wa kuonyesha ishara chanya za kujenga uaminifu na kuzidisha nafasi za utatuzi wa kidiplomasia.

Wachambuzi wanahoji kwamba nafasi iliyosalia kuunusuru mkataba huo wa kimataifa ni ndogo. Mkataba huo ulipata pigo mwaka 2018 na nusura uvunjike kabisa wakati rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alipoiondioa nchi yake miongoni mwa washirika wa makubaliano hayo.

Rais wa Iran, Hassan Rouhani
Rais wa Iran, Hassan RouhaniPicha: Iranian Presidency/dpa/picture alliance

Marekani yataka kurudi kwenye mkataba wa nyuklia wa Iran

Utawala wa rais mpya wa Marekani Joe Biden, umesema umejiandaa kujiunga tena na mkataba huo na kuanza kuondoa vikwazo dhidi ya Iran, ikiwa Iran itaanza kutekeleza kikamilifu ahadi zake. Lakini Iran imepinga sharti hilo.

Usiku wa kuamkia leo kuelekea mkutano wa wanadiplomasia watakaojadili suala la mkataba huo, rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wamezungumza kwa njia ya simu na kujadili kitisho cha Iran pamoja na changamoto za kanda hiyo. Hayo ni kwa mujibu wa tarifa ya Ikulu ya Marekani, Whitehouse.

Kinachozidisha mvutano ni mipango ya Iran kuzuia shirika la nguvu za atomiki la Umoja wa Mataifa (IAEA) kufanya ukaguzi nchini mwake ikiwa Marekani haitaondoa vikwazo ilivyoiwekea Iran mwaka 2018, ifikapo Februari 21, kulingana na masharti ya muswada ulioidhinishwa na bunge la Iran mwezi Disemba.

Iran kuwazuia wakaguzi wa IAEA katika vinu vyake

IAEA: Kitisho cha Iran kitakuwa na athari kubwa

Mkuu wa shirika hilo la IAEA Rafael Grossi anatarajiwa kusafiri kuelekea Tehran siku ya Jumamosi kwa mazungumzo na maafisa wa Iran, kujaribu kupata suluhisho la ukaguzi unaoendelea nchini humo.

Shirika la IAEA limeonya kwamba kitisho cha Iran kitakuwa na athari kubwa dhidi ya juhudi zake za kukagua na kufuatilia shughuli zinazofanyika nchini humo kuhusiana na mipango ya nyuklia.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Ned Price amesema Iran inapaswa kushirikiana kikamilifu na kwa wakati ufaao na shirika hilo la IAEA.

Wachambuzi watilia shaka mkutano kuzaa matunda

Hata hivyo, afisa mmoja mkuu wa será kuhusu mahusiano ya kigeni katika Baraza la Ulaya Ellie Geranmayeh, ametilia shaka uwezekano wa mkutano wa Alhamisi kuzaa matunda kisiasa au kiuchumi kuzuia Iran kutekeleza kitisho chake.

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu nishati ya atomiki Rafael Mariano Grossi
Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu nishati ya atomiki Rafael Mariano GrossiPicha: Alex Halada/AFP/Getty Images

Ellie ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, tarehe ya mwisho iliyotolewa na Iran imekuwepo kwa miezi kadhaa, na endapo Iran haitapata ahueni kiuchumi, viongozi wake hawatakuwa na budi kutekeleza kitisho chao.

Wiki iliyopita, shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu nishati ya atomiki ilisema Iran imeanza kutengeneza vyuma vya urani, hivyo kukiuka mkataba, hatua iliyochochea nchi zenye nguvu za Ulaya kuonya kwamba Iran inahujumu juhudi za kidiplomasia ambazo zimefufuliwa upya.

(AFPE)