1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukosefu wa fedha ni changamoto kwa bunge la Afrika Mashariki

19 Desemba 2018

Wabunge wa bunge la Afrika mashariki wamelaumu nchi wanachama wa mtengamano huo kwa kushindwa kutoa michango ya kuendesha jumuiya hiyo.

https://p.dw.com/p/3ANn0
Ostafrikanische Gemeinschaft Kenyatta, Museveni und Maguful
Picha: DW/C. Ngereza

Wabunge wa bunge la Afrika mashariki wamelaumu nchi wanachama wa mtengamano huo kwa kushindwa kutoa michango ya kuendesha jumuiya hiyo na kusababisha sekretarieti ya jumuiya hiyo pamoja na bunge kushindwa kufanya kazi zake kutokana na ukosefu wa fedha huku baaadhi ya miradi ikikwama na kuzua hofu juu ya mustakabali wa jumuiya hiyo yenye sita wanachama.

Wakizungumza katika mjadala mkali katika bunge hilo wabunge hao wamesema nchi hizo zinakikuka mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ambao unaeleza wazi kuwa kila nchi inapaswa kutoa mchango wake ndani ya wakati ili kusaidia uendeshwaji wa miradi na mambo muhimu ndani ya jumuiya hiyo.
 

Alikuwa ni mbunge wa Uganda, Suzan Nakauchi, ambaye aliwasilisha hoja maalum ya kujadiliwa kwa hali ya mambo ndani ya jumuiya hiyo kutokana na watumishi wa sektarieti ya jumuiya na wabunge kukosa mishahara na posho mbalimbali hali ambayo imesababisha hali ya sintofahamu katika mwelekeo wa mambo ndani ya jumuiya hiyo.
 

Hoja hiyo iliungwa mkono na bunge hilo ambapo Mbunge kutoka Tanzania Abdullah Makame alisema, suala la kuchangia michango kwa nchi wanachama ni muhimu na lipo katika itifaki ya mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo na hivyo nchi wanachama wanapswa kuheshimu na kutekeleza wajibu huo.

East African Community Gipfel Tansania Arusha
Picha: picture-alliance/dpa/Xinhua

Naye Kenedy Musyoka mbunge kutoka Kenya alisema hatua ya nchi wanachama kuchelewesha michango au kutotoa michango hiyo haivumilki na kuzitaka nchi wanachama wa jumuiya hiyo kutoa michango yao ili kuweka mambo sawa katika jumuiya hiyo.

Hadi kufikia jana nchi Kenya ilikuwa tayari imetoa asilimia 80 ya mchango wake ,Uganda ikiwa imetoa asilimia 53 na Tanzania ikiwa imetoa asilimia 52 huku Rwanda ikiwa imetoa asilimia 25 huku nchi za Sudan kusini na Burundi zikiwa zimetoa asilimia sifuri.
 

Katika hatua nyingine mbunge wa bunge hilo George Steven Odongo aliwasilisha hoja ya kutaka bunge hilo kujadili hali ya mambo katika jumuiya hiyo kutokana na mizozozo miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo huku akitaja tukio la wanamichezo waliozuiwa kuingia nchini Burundi hapo juzi kuwa linaashiria kudorora kwa mahusiano miongoni mwa nchi wanachama.
 

Hatua hiyo inakuja wakati baadhi ya wakuu wa nchi wanachama na mawaziri wa nje wakiwemo wa nchi za Rwanda na Burundi wakisema wazi kuwa baadhi ya nchi wanachama zinazozana na kushutumiana na hivyo kuna haja ya matatizo hayo kutafutiwa ufumbuzi.

Mwandishi: CHARLES NGEREZA/DW ARUSHA

Mhariri: Mohammed Khelef