1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yawaondoa wanajeshi wake wote Afghanistan

Amina Mjahid
30 Juni 2021

Ujerumani imewaondoa wanajeshi wake wa mwisho kutoka Afghanistan na kuhitimisha operesheni zake, baada ya kutumikia nchini humo kwa takriban miaka 20

https://p.dw.com/p/3voho
Afghanistaneinsatz der Bundeswehr endet
Picha: Torsten Kraatz/Bundeswehr/dpa/picture alliance

Jeshi la anga la Ujerumani liliwasafirisha wanajeshi hao waliokuwa sehemu ya ujumbe wa Jumuiya ya kujihami NATO kutoka kambi ya Mazar-i-Sharif, na kuwarejesha nyumbani.

Katika ndege hiyo iliyowabeba wanajeshi hao, kilikuwepo pia kikosi maalum cha wanajeshi KSK kilichopelekwa upande wa kaskazini mwa Afghanistan kuilinda kambi ya Mazar i Sharif. Wanajeshi wote wanatarajiwa kuwasili katika kambi ya kijeshi ya Wunstorf katika jimbo la Lower Saxony nchini Ujerumani.

Waziri wa ulinzi wa ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer amesema baada ya miaka 20 hatimaye wanajeshi wa ujerumani wameondoka afghanistan walikopambana na kudhihirisha umahiri wao katika vita vya Afghanistan. Kulingana na jeshi la Ujerumani Bundeswehr, wanajeshi 59 waliuwawa katika operesheni yao nchini humo wakiwemo 35 waliouwawa katika mashambulizi na mapambano makali.

soma zaidi: Biden akutana na Ghani, Abdullah kuhusu Afghanistan

Kramp-Karrenbauer alitangaza pia msaada kwa wanajeshi wa Afghanstan walioshirikiana na wanajeshi wake katika operesheni yao. Kwa mfano, wakalimani walioshirikiana nao, sasa wanaweza kupata kibali cha kuishi ujerumani. Amesema baadhi yao wapo njiani kuelekea Ujerumani huku wengine wakiamua kusubiri kwanza kabla ya kuanza safari yao.

Ujerumani iliharakisha mchako wa kuwaondoa wanajeshi wake baada ya utawala wa Marekani chini ya rais Joe Biden kutangaza pia kuwaondoa wanajeshi wake huko.

Wanasiasa wa Afghanistan wakosoa hatua ya kuondolewa wanajeshi wa kigeni

Wanajeshi wa mwisho wa Ujerumani nchini Afghanistan warejea

Kama mchangiaji mkubwa wa wanajeshi Afghanistan, Marekani ilijipanga kukiondoa kikosi chake  ifikapo septembe 11, tarehe ya kuadhimisha mashambulizi ya kigaidi yaliotokea nchini humo miaka 20 iliyopita, yanayodaiwa kufanywa na kundi la al qaida, lakini kwa sasa imesema wanajeshi hao wataondoka Julai 4 ambayo ndiyo siku kuu ya mapumziko ya kitaifa.

Ujerumani ilikuwa na wanajeshi 1,100 Afghanistan. Wanajeshi hao wanaondoka huku wakiacha hali isiyothabiti na hatua ya kuondoka kwao ikikosolewa vikali na wanasiasa nchini humo.

Soma zaidi: Kundi la Taliban latoa onyo kali kwa wanajeshi wa Marekani

Fawzia Hamidi mbunge wa Afghanistan amesema wanajeshi wa ujerumani walikuwa wanatoa msaada mkubwa kwa jeshi lao pamoja na watu wake, na kuondoka kwao kunawafanya wengi kuhisi ni kana kwamba wameachwa peke yao huku hali ikigeuka na kuwa mbaya zaidi kiusalama.

Fawzia ameliambia shirika la habari la dpa kwamba tayari kundi la taliban lilidhibiti wilaya ya kaldar katika mkoa wa balkh wakati wanajeshi wa Ujerumani walipokuwa wanaondoka kutoka kambi yao ya kijeshi.

Kwa ujumla tangu kuanza kuondoka kwa wanajeshi wa kigeni mnamo Mei mosi wanamgambo wa kundi la Taliban wamefanikiwa kudhibiti wilaya 90 kati ya 400 za Afghanistan.

Chanzo: afp/dpa

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi