1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani iko tayari kuridhia mageuzi ya uombaji hifadhi

Amina Mjahid
29 Septemba 2023

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Nancy Faeser, amesema Berlin iko tayari kukubaliana na pendekezo jipya la maelewano juu ya namna ya kudhibiti uhamiaji katika Umoja wa Ulaya wakati wa mzozo.

https://p.dw.com/p/4WvZg
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Nancy Faeser
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Nancy FaeserPicha: Michael Bahlo/dpa/picture alliance

Waziri Faeser ametoa kauli hiyo katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya wanaokutana hii leo mjini Brussels kujadili vipengele vinavyozusha mabishano kwenye mageuzi ya sera ya uhamiaji.

Hatua hizo zenye utata ni muhimu katika mageuzi makubwa ya uhamiaji, yanayolenga kupunguza uhamiaji katika jumuiya hiyo, ambazo zimekuwa zikifanyiwa kazi kwa miaka mingi. Ujerumani ilikuwa imekataa pendekezo la hapo awali.

Waziri Faeser amewaambia wenzake wa Umoja wa Ulaya kwamba Berlin sasa iko tayari kupiga kura kuunga mkono maelewano hayo, licha ya wasiwasi uliokuwepo. Ujerumani mara kwa mara imetoa wito wa ulinzi bora wa familia chini ya kipengele cha mzozo.

Mwaziri wa Uhamiaji wakutana Brussels kujadili mustakabali wa waomba hifadhi

Hata hivyo, Waziri Faeser alielezea masikitiko yake kwamba hakuna uungwaji mkono mkubwa wa sera hiyo ndani ya Umoja wa Ulaya kwa sasa.

Waziri wa Uhamiaji wa Luxembourg, Jean Asselborn, amesema nchi yake inaunga mkono wito wa Ujerumani wa kuwepo kwa hatua bora zaidi kuzilinda familia, hatua zinazopigiwa chapuo pia na Ireland na Ureno.

Sheria hiyo ya ushughulikiaji wa wahamiaji wakati wa mgogoro itakuwa inafanya kazi wakati Ulaya ikiwa inakabiliwa na wimbi kubwa la wahamiaji kama ilivyo sasa, lakini Ujerumani ilikuwa inataka kila nchi iwekewe masharti makali ya vipi inaweza kutangaza mgogoro wa wahamiaji na kuweza kutumia kanuni hizo maalum.

Waomba hifadhi watalazimika kukaa vituoni kwa zaidi ya wiki 12.

Italien | Migranten auf Lampedusa
Boti la polisi Italia katika kisiwa cha Lampedusa likiwa na wahamiaji waliookolewa Picha: Cecilia Fabiano/AP Photo/picture alliance

Kifungu kinachohusika na mageuzi hayo kinatowa muda mrefu zaidi kwa usajili wa maombi ya wahamiaji kwenye mipaka ya nje ya Umoja wa Ulaya, na pia uwezekano wa kushusha viwango vya makaazi na huduma wanazopatiwa wahamiaji hao.

Vile vile, waomba hifadhi sasa wanaweza kulazimika kukaa kwenye vituo vya kuwapokelea mipakani kwa zaidi ya wiki 12.

Ujerumani ilikuwa inapingana na mpango huo ikihoji kuwa viwango vya huduma kwa waomba hifadhi vingeshushwa kupita kiasi.

Kanuni hizo za dharura zinaweza kuzifanya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ambako wahamiaji walifikia awali kuwaruhusu kuingia Ujerumani na nchi nyengine za Umoja huo zilizoendelea zaidi, na hivyo kuipa mzigo mkubwa zaidi Berlin.

Mataifa yanayopinga kupokea wahamiaji barani Ulaya, yakiwemo Poland na Hungary, yamekuwa yakipigania hatua kali zaidi ya hizi.

Ujerumani kuongeza doria mpaka wa Poland na Jamhuri ya Czech

Ikiwa idadi kubwa ya mataifa ya Umoja huo yataunga mkono kanuni hizo mpya, zitawasilishwa haraka mbele ya Bunge la Ulaya kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa, huku wakati ukiwa unapita kwa kasi kutokana na wimbi la wahamiaji kuzidi katika miezi ya hivi karibuni.

Ikiwa majadiliano juu ya rasimu ya kanuni hizo yatachelewa kwenye kiwango cha serikali za mataifa ya Ulaya na hatimaye kuchelewa kuingia bungeni, huenda kusiwe na sheria yoyote itakayotangazwa hadi baada ya chaguzi za bunge la Ulaya kukamilika.

Chanzo: dpa