1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, Brazil zawasilisha azimio la udukuzi

8 Novemba 2013

Ujerumani na Brazil zimewasilisha rasimu ya azimio la kupinga udukuzi katika baraza kuu la umoja wa Mataifa hapo jana kwa hoja kwamba faragha katika mawasiliano ni haki ya msingi ya kibinadaamu na msingi wa demokrasia

https://p.dw.com/p/1ADzE
Picha: picture-alliance/dpa

Azimio hilo lililowasilisha na nchi hizo mbili linafuatia ufichuzi kuwa shirika la kitaifa la Ujasusi Marekani lilidukua mawasiliano ya Ujerumani,Brazil na mataifa mengine mengi duniani.Rasimu hiyo inasema baraza kuu la umoja wa Mataifa linapaswa kutilia msisitizo haki zinazopewa watu wasiotumia mitandao pia zinastahili kwa wanaoitumia ya kujieleza kwa uhuru.

Balozi wa Ujerumani katika umoja wa Mataifa Peter Wittig akiwasilisha azimio hilo,alisema anatumai azimio hilo litachochea mazungumzo yenye manufaa na kusaidia kuhakikisha kuwepo kwa haki ya kuwa na faragha kwa wanaoutumia mitandao na kuongeza kuwa udukuzi huo wa mawasiliano ya kibinafsi umezua hali ya taharuki miongoni mwa watu kote duniani.

Balozi wa Brazil Antonio de Aguiar Patriota amesema azimio hilo linataka kusitishwa kwa udukuzi na ukusanyaji wa data za kibinafsi na serikali zinazohusika na kuongeza kulindwa kwa haki ya faragha za watu ili kuwalinda dhidi ya matumizi mabaya ya mamlaka kwani ukosefu wa haki ya kuwa na faragha unawanyima watu uhuru wa kweli wa kujieleza.

Brazil inaamini ni muhimu kwa jumuiya ya kimataifa kulijadili kwa kina suala la kulinda haki za binadaamu hata kati enzi hii ya dijitali, ikihusisha pia mchakato wa kushughulikia usalama wa kitaifa na kufuatilia vitendo vya kihalifu.

Rais wa Brazil Dilma Rouseff (Kushoto) na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Rais wa Brazil Dilma Rouseff (Kushoto) na Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Chris Ratcliffe-Pool/Getty Images

Mifumo huru kuundwa kuepusha udukuzi

Azimio hilo lililowasilishwa kwa kamati inayoshughulikia masuala ya haki za binadamu katika umoja wa mataifa pia linataka kuundwa kwa mifumo huru ya usimamizi katika kila nchi kuepusha visa vya serikali kufanya udukuzi na kuzitaka nchi wanachama wa umoja huo kuchukua hatua za kukomesha ukiukaji wa haki hizo ikiwemo kuhakikisha kuwa sheria za nchi husika zinaheshimu sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu.

Azimio hilo haliinyoshei nchi yoyote kidole cha lawama wazi wazi lakini Marekani imejipata ikishutumiwa vikali kufuatia ufichuzi uliofanywa na mfichua siri za kijasusi Edward Snowden.

Marekani imekuwa ikishutumiwa kwa udukuzi

Brazil na Ujerumani zimekuwa katika msitari wa mbele katika kushutumu udukuzi tangu sakata hiyo ya ufichuzi wa taarifa za kijasusi miezi michache iliyopita inayodai kuwa Marekani imekuwa ikidukua mawasiliano ya mamilioni ya watu duniani yakiwemo hata ya kibinafsi ya viongozi wa nchi akiwemo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Brazil Dilma Rouseff.

Mfichua siri za Marekani Edward Snowden
Mfichua siri za Marekani Edward SnowdenPicha: Reuters

Marekani imekanusha madai kuwa inachunguza mawasiliano ya kibinafsi ya Kansela Merkel na kusema haitafanya hivyo hata siku za usoni lakini imekataa kutamka chochote kuhusu iwapo ilifanya hivyo kipindi cha nyuma.

Kufuatia kuwasilishwa kwa azimio hilo,nchi kumi ikiwemo Korea kaskazini zimekubali kuliunga mkono na idadi ya nchi zinazounga mkono azimio la Ujerumani na Brazil inatarajiwa kuongezeka kabla ya kupigiwa kura katika kamati hiyo baadaye mwezi huu na iwapo itafanikiwa kuungwa mkono katika kura hiyo,itawasilishwa kwa baraza kuu la umoja wa Mataifa kupigiwa kura ya kuidhinishwa mwezi ujao.

Mwandishi:Caro Robi/dpa/Reuters/Dw.English

Mhariri: Gakuba Daniel