1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza,Canada na Australia zaitambua Palestina kama Taifa

21 Septemba 2025

Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema hatua yake inalenga kuleta amani mashariki ya kati na sio kuizawadia Hamas kama inavyodai Israel

https://p.dw.com/p/50pvC
Waziri mkuu Keir Starmer
Waziri mkuu Keir Starmer Picha: 10 Downing Street/PA Media/dpa/picture alliance

Uingereza,Canada na Australia zimetangaza rasmi leo Jumapili kulitambua taifa la Palestina  licha ya Israel na Marekani kupinga vikali hatua hiyo kuchukuliwa.

Waziri mkuu wa Uingereza Keir Stamer amethibitisha kwamba sasa ni rasmi Uingereza inayatambua Mamlaka ya Wapalestina kama Taifa.

Tangazo la Starmer limeonekana kama ni hatua ya pamoja ya ushirikiano na Canada na Australia ambayo ni mataifa wanachama wa jumuiya ya madola.

Kiongozi huyo wa Uingereza ambaye amekabiliwa kwa muda na shinikizo kutoka ndani ya chama chake cha Labour la kumtaka achukue msimamo mkali dhidi ya Israelamesema hatua yake inalenga kufufua matumaini ya amani kwa Wapalestina na Waisrael na sio hatua ya kulizawadia kundi la Hamas.

Amesisitiza bwana Starmer kwamba Hamas hawatokuwa na dhima yoyote ya uongozi wa hapo baadae wa Wapalestina mjini Ramallah.

Rais wa Mamlaka ya Wapalestina  Mahmoud Abbas
Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud AbbasPicha: Anthony Behar/Sipa USA/picture alliance

Ujumbe wa Mahmoud Abbas

Rais Mahmoud Abbas ameiitaja hatua ya Uingereza ya kulitambua taifa la Palestina kuwa muhimu iliyohitajika kuelekea amani ya kudumu kwenye kanda hiyo.

Japo hatua ya kuitambua Palestina kuwa taifa huru kwa sehemu kubwa ni alama tu, ni kitendo cha kihistoria na hasa kwakuwa Uingereza ndiyo iliyoweka msingi wa kuundwa kwa dola la Israel wakati nchi hiyo ilipokuwa ikidhibiti kile kilichofahamika kama Palestina mnamo mwaka 1917.

Tangazo la Uingereza lilitarajiwa baada ya Starmer kuweka wazi mwezi Julai kwamba nchi hiyo itaitambua Palestina kama taifa ikiwa Israel haitokubali kusitisha vita Gaza na kuruhusu Umoja wa Mataifa kupeleka msaada na kuchukua hatua nyingine za kuelekea amani ya kudumu.

Zaidi ya nchi 140 za ulimwengu tayari zimeshaitambua Palestina kama taifa na nyingine zaidi zinatarajiwa kuchukua hatua hiyo katika mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa wiki hii, ikiwemo Ufaransa.

Israel yakasirishwa na hatua ya Uingereza

Hasira zimeshaanza kujitokeza Israel ambako Mawaziri wawili wa wanaofuata  siasa kali za mrengo wa kulia wametoa wito wa kunyakuliwa kwa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel kujibu tangazo la Uingereza, Canada na Australia kulitambua taifa la Palestina.

Israel na Marekani zinapinga vikali hatua ya kuitambuwa Palestina kama Taifa huru
Israel na Marekani zinapinga vikali hatua ya kuitambuwa Palestina kama Taifa huruPicha: Nathan Howard/AFP/Getty Images

Waziri wa usalama wa taifa Itamar Ben Gvir, amesema leo kwamba tangazo la Uingereza, Canada, na Australia kulitambua taifa la Palestina, linahitaji hatua za haraka za kukabiliana na hali hiyo.

Miongoni mwa hatua za haraka alizopendekeza ni kupititishwa kwa mamlaka ya kujitawala huko Yudea na Samaria na kuvunjwa kabisa kwa Mamlaka ya Palestina.

Waziri huyo anakusudia kuwasilisha pendekezo la kupitishwa mamlaka ya kujitawala katika mkutano ujao wa baraza la mawaziri.

Naye waziri wa fedha Bezalel Smotrich, ambaye mara kadhaa ametaka Ukingo wa Magharibi kunyakuliwa, naye alitoa kauli kama hiyo.