″Ufaransa na Umoja wa Ulaya zibadilishe sera zake″ | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.02.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

"Ufaransa na Umoja wa Ulaya zibadilishe sera zake"

Kwa mujibu wa mwandishi wetu Thomas Mösch, mzozo huu unaonyesha wazi kosa la sera za Ulaya barani Afrika. Ili hali iboreke lazima Ufaransa na Umoja wa Ulaya zibadilishe sera zake.

default

Jeshi la Ufaransa mjini N'Djamena


Nchini Chad waziri wa ulinzi wa Ufaransa amewasili katika mji mkuu N'Djamena kuonyesha kwamba wa Ufaransa inaiunga mkono serikali hiyo ya koloni yake ya zamani. Lakini waasi  walitoa taarifa kwamba watapiga ili kujihami ikiwa Wafaransa wataingilia kati kijeshi. Wakati huo huo, hali ya wakimbizi inaendelea kuwa tete, baadhi yao sasa wamefika Nigeria baada ya kupita Cameroon.
Kwa mara nyingine tena, nchi za Ulaya, na hasa Ufaransa, zinajikuta zikizipa kisogo sera zao barani Afrika. Kinachotokea nchini Chad hivi sasa ni cha kushangaza na kitatokea tena wakati serikali ya nchi hiyo inatumika tu kutekeleza maslahi ya makundi fulani na nchi nyingine.
Kwa kweli, Chad haijapata uhuru wake kutoka kwa Ufaransa na Umoja wa Ulaya haujajali Ufaransa inachofanya katika koloni zake za zamani za Afrika, si juu ya maadili ya demokrasia wala haki za binadamu. Na mradi anasaidia kuendeleza maslahi ya Ufaransa, rais Idriss Déby atabakia madarakani. Lakini kwa Wachadi wengi hata mabadiliko madarakani yanayopiganiwa kwa nguvu hayatawasaidia kwa sababu mzozo huu ni kati ya watu hao hao wa tabaka la juu ambao kwa miaka mingi sasa wanatawala nchi hii na kuzipora mali zake.
Mfano unaofaa kabisa kuonyesha sera mbaya za Ufaransa ni juu ya rais huyu Idriss Déby mwenyewe. Mwaka 1990 aliingia madarakani kwa njia hiyo hiyo inayotumika sasa na wapinzani wake kumwangusha, yaani mapigano. Baadaye na baada ya kuzungumza na serikali ya Ufaransa, Idriss Déby akajifanyia kama kiongozi wa kidemokrasi. Lakini yule ambaye bado aliamini kwamba Déby ni mwanasiasa bora alifahamu ukweli pale Déby alipobadilisha katiba miaka mitatu iliyopita ili aweze kupewa muhula mwingine kupitia uchaguzi wa udanganyifu.
Chad iliyoko katikati mwa bara la Afrika na ni muhimu sana kwa Ufaransa yenye kituo chake kikubwa cha kijeshi humo Chad. Juu ya hayo, nchi hii maskini ilijiunga na kundi la nchi zinazozalisha mafuta mengi duniani. Licha ya upinzani mwingi, Déby aliweza kuzishawishi nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani kwamba yeye anaweza kutegemewa katika biashara ya mafuta. Mikataba na benki ya dunia ambayo ililenga kuhakikisha kwamba wananchi wanufaike kutokana na utariji wa mafuta haitekelezwi kama ilivyopangwa.
Pia vita vya Darfur vilimsaidia Déby kuimarisha mamlaka wake. Huenda yeye mwenyewe alisaidia kuuzidishia mzozo huu. Chad sasa inahitajika kuwahudumia mamia ya wakimbizi. Kutumwa kikosi cha jeshi la Ulaya cha kulinda amani karibu na mpaka na Sudan bila shaka kungeuimarisha zaidi uongozi wa Idriss Déby. Kwa hivyo, ni hatua ya kushangaza kwamba waasi ambao wanasemekana wanaungwa mkono na Sudan wanajaribu kuangusha serikali wakati huu.
Bila shaka, ni sawa kwa Umoja wa Afrika na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusisitiza kwamba mapinduzi ya serikali kwa kutumia nguvu hayatakubaliwa. Lakini inabidi pia serikali za jumuiya ya kimataifa hususan za Ufaransa na nchi za Umoja wa Ulaya zitambue kwamba usalama nchini Chad utapatikana tu ikiwa makundi yote muhimu yatashirikishwa katika serikali. La sivyo, watu wa kawaida watalazimika kuendelea kuyavumilia majaribio ya makundi ya wanamgambo kupigania uongozi kwa kutumia nguvu.
 • Tarehe 06.02.2008
 • Mwandishi Mösch, Thomas
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/D3U1
 • Tarehe 06.02.2008
 • Mwandishi Mösch, Thomas
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/D3U1

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com