Tony Blair afanya ziara katika nchi tatu za Afrika | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.05.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Tony Blair afanya ziara katika nchi tatu za Afrika

Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair amewasili nchini Sierra Leone ikiwa ni mkondo wa pili wa ziara yake katika nchi tatu za Afrika.

Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair

Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair

Waziri mkuu wa Uingereza anaeondoka Tony Blair amepokelewa kwa shangwe na nderemo katika mji wa Lungi ulio karibu na mji mkuu wa Free Town nchini Sierra Leone akitokea nchini Libya.

Huku akiwa ameandamana na mkewe Bi Cherie waziri mkuu wa Uingereza anafanya ziara ya kuaga kabla ya kung’atuka madarakani mwishoni mwa mwezi ujao wa Juni.

Taarifa kutoka wizara ya mambo ya nje mjini Free Town zinaarifu kuwa rais Ahmad Tejan Kabbah wa Sierra Leone amepanga maandalizi kabambe ya sherehe za kumuaga waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair.

Bwana Blair atatunukiwa uchifu wa heshima katika sherehe ya kitamaduni na pia atatunukiwa shahada ya heshima na chuo kikuu cha Sierra Leone kwa mchango wake alioutowa katika kuleta amani baada ya vita vya miaka kumi nchini Sierra Leone.

Waziri mkuu wa Uingereza baadae atafanya mazungumzo na rais Kabbah na kisha atakutana na rais Ellen Johson Sirleaf wa Liberia ambae pia yuko nchini Sierra Leone kwa ajili ya kufanya mazungumzo na waziri mkuu huyo anaeondoka.

Mazungumzo kati ya waziri mkuu wa Uingereza na viongozi hao yatazingatia maswala ya maendeleo, vita dhidi ya umasikini,elimu,afya na maswala yanayohusu ajira.

Waziri wa mambo ya nje wa Sierra Leone Momodu Koroma ameeleza kuwa ziara ya bwana Tony Blair nchini mwake kuwa ni ishara ya uhusiano mzuri baina ya nchi zao.

Waziri mkuu Tony Blair atakuwepo nchini Sierra Leone kwa muda wa saa tisa kabla ya kuelekea nchini Afrika Kusini kukamilisha mkondo wa tatu wa ziara yake barani Afrika.

Kwa mujibu wa wasaidizi wa bwana Blair ni kwamba ziara ya kiongozi huyo inalenga kutafuta kuungwa mkono juhudi za kusimamisha machafuko katika jimbo la Darfur nchini Sudan na pia kutafuta mbinu za kumaliza mzozo wa kisiasa na kiuchumi unaoikabili Zimbabwe.

Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair, amesema kwamba ana matarajio kuwa ziara yake hii itahamasisha mkazo juu ya bara la Afrika kuhusu swala la mabadiliko ya hali ya hewa katika mkutano wa viongozi wa nchi za G8 utakaofanyika nchini Ujerumani katika siku chache zijazo.

Bwana Tony Blair pia ameeleza kwamba mazungumzo yake na rais Muammar Gadaffi wa Libya yalikuwa yenye mafanikio makubwa na kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeimarika zaidi hasa baada ya Libya kutelekeza nia yake ya kutaka kuwa na silaha za kinyuklia.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com