Timu 8 kileleni mwa timu 32 za kombe la dunia. | Michezo | DW | 02.12.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Timu 8 kileleni mwa timu 32 za kombe la dunia.

Ufaransa na Ureno hazimo.

Bafana-Bafana kileleni kundi 1.

Bafana-Bafana kileleni kundi 1.

Kura ya kuamua jinsi timu 32 za Kombe lijalo la dunia nchini Afrika Kusini,ikikaribia kupigwa keshokutwa ijumaa mjini Cape Town,Afrika Kusini, leo timu 8 zitakazoongoza makundi 8 ya duru za kwanza ilipigwa: Ujerumani,mabingwa mara 3 wa dunia, ni miongoni mwa timu hizo 8 zilizowekwa kileleni mwa kila kundi la timu 4:

Mabingwa wa dunia 1998,Ufaransa kama Ureno, hazimo katika safu hiyo. FIFA inadai kwa Ufaransa,hiyo haitokani na madhambi aliofanya nahodha wake Thierry Henry, ya kuunawa mpira kwa mkono kulikoongoza kutiwa lile bao lililoipiga kumbo Ireland nje ya Kombe hilo la dunia 2010.

Timu 8 zitakazo ongoza kileleni mwa makundi 8 ya timu nne-nne zilizotangazwa leo na FIFA mjini Cape Town ,Afrika Kusini kwa kura ya ijumaa hii, zimechaguliwa kwa muujibu wa orodha ya ngazi ya timu bora za FIFA. Ufaransa na Ureno ,kinyume na ilivyokua katika Kombe lililopita la dunia hapa Ujerumani 2006, mara hii hazimo kwenye orodha ya timu hizo kileleni.

Timu 8 zilizochaguliwa kwa muujibu wa nafasi zao hadi mwezi Oktoba mwaka huu katika orodha ya timu bora za dunia ni mabingwa wa dunia-Itali,Brazil,Ujerumani,Argentina, Uingereza na Holland. Kutoka kanda ya Afrika, ni wenyeji Afrika Kusini wamewekwa kileleni kuongoza chungu nambari 1.

Isitoshe, Afrika Kusini, ndio itakayofungua dimba hapo juni 11, mwakani katika Uwanja wa City Stadium, mjini Johannesberg.Mechi 63 zitakazofuatia mpambano huo wa ufunguzi, zitachezwa katika viwanja vya miji mbali mbali, kuanzia Polokwane huko kaskazini-mashariki hadi jiji la Cape Town uliopo kusini-magharibi mwa nchi hiyo.

Kilele kitakua Julai 11 ,2010 -siku ya finali mjini Pretoria.Ufaransa na Ureno safari hii zimeangukia chungu cha 4 pamoja na wenzao wa kanda ya UEFA ya ulaya-Denmark,Ugiriki,Serbia,Slovenia,Slovakia na Uswisi.

Hii ina maana zitapigiwa kura kutoka chungu kimoja hapo ijumaa jioni. Tafrija hiyo itachukua muda wa saa na nusu nzima ikiingiza mastadi wa dimba kama David Beckham wa Uingereza na mcheza-cinema wa kike Charlize Theron.

Kama desturi ,kila kura inayopigwa huzaa kundi moja la "kufa-kupona" kama kuzitia kundi moja na mapema Ufaransa na Brazil na labda, Australia na Mexico na Chile au Paraguay. Ikitokea hivyo, bila ya shaka, itakua kuangukia ajali hiyo ya kundi la kufa-kupona.Utakumbuka katika Kombe lililopita la dunia 2006,Tembo wa Ivory Coast,wakiongozwa na nahodha wao Didier Drogba, waliangukia kundi kama hilo liloingiza Argentina,Holland na Serbia.Rahisi hapo kukata roho na mapema.

Holland,mara hii , ilitamba katika mapambano yake ya kufuzu kwa Kombe lijalo la dunia kama ilivyotamba Spain, mabingwa wa Ulaya Haikushindwa hata mara moja.Hizi ndizo timu za kwanza kushinda mechi zao zote.Kwa sababu hiyo Holland, imetumbukizwa chungu nambari 1.

Katibu mkuu wa FIFA Jerome Valcke, amekanusha uvumi kuwa mabingwa wa dunia 1998,Ufaransa, wameshushwa hadhi kutojumuishwa katika kundi hilo la timu 8 kutokana na madhambi ya nahodha wao Thierry Henry ,alieunawa mpira kwa mkono na kuipiga kumbo Ireland nje ya kombe hili la dunia.Jaribio la Ireland,kuvunjwa miko ili ya FIFA na kuwa timu ya 33 badala ya 32 lilizimwa na FIFA.

Chungu cha 3 kinajumuisha Simba wa nyika-Kamerun,Super Eagles,Nigeria,Tembo -Ivory Coast,Black Stars -Ghana,kanda ya Afrika na ile ya Amerika Kusini, ni Chile,Paraguay na Uruguay,mabingwa wakwanza kabisa wa dunia, 1930 lilipoazishwa Kombe hili mjini Montevideo.

Mwandishi: Ramadhan Ali /AFPE

Uhariri: Abdul-Rahman