Tillerson na Lavrov, watakutana Afrika kweli? | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.03.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Tillerson na Lavrov, watakutana Afrika kweli?

Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Urusi wako ziarani barani Afrika huku  kukiwa na  taarifa taarifa kwamba mawaziri hao Rex Tillerson wa Marekani na  Sergey Lavrov wa Urusi watakutana barani humo.

Lakini hakuna dalili kwamba hilo litafanyika licha ya kuwa viongozi hao walifikia  katika hoteli moja mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Wanadiplomasia hao wakuu wa Marekani na Urusi wanaonekana kuzungukana tu huko Afrika ambako wote wako kwenye ziara rasmi. Wakati ambapo nchi zao mbili zinalaumiana kuhusiana na mzozo wa Syria na Ukraine, serikali zao zinarushiana cheche kwenye mitandao ya kijamii kuhusu nani wa kulaumiwa kwa mawaziri hao wawili kutofanya kikao Addis Ababa.

Urusi imesema kwamba Tillerson na Lavrov wote wanakaa katika hoteli ya kifahari ya Sheraton mjini Addis Ababa  nchini Ethiopia ambapo Alhamis Tillerson atakuwa anakutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia anayeondoka madarakani pamoja na  na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya  Umoja wa Afrika.

Marekani haikupokea ombi la mkutano kutoka kwa serikali ya Urusi

Haijabainika mawaziri hao wawili walivyokosa kukutana huko Addis Ababa kwani Tillerson aliwasili Jumatano  mchana wakati ambapo Lavrov aliondoka mjini humo Jumatano usiku na kuwasili Zimbabwe kituo cha pili cha ziara yake.

Rex Tillerson (Picture-Alliance/AP Photo/I. Sekretarev)

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson

Pamoja na hayo Urusi inasema iliitisha mkutano na imeweka wazi kwamba ilituma ombi la kuwepo kwa mkutano hata kabla ya ziara hizo na imesisitiza kwamba ilituma ombi rasmi la kuweka miadi kwa Marekani ila inasema haikupokea jibu.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani Heather Nauert alisema wiki hii kwamba Marekani haijapokea ombi lolote la mkutano na Tillerson kutoka kwa serikali ya Urusi na kwamba haikuwa na tangazo lolote la mkutano.

Iwapo wangekutana kuna mengi ambayo wawakilishi hao wa nchi hizo mbili zenye nguvu duniani wangeyajadili. Nauert na Wizara ya Ulinzi ya Marekani wamekuwa wakiituhumu hadharani Urusi kwa vitendo vyake nchini Syria huku ikisema kwamba Urusi ndiyo inayowapiga raia kwa mabomu katika katika mji wa Ghouta mashariki ulioko karibu na Damascus.

Marekani na Urusi zashambuliana katika mitandao ya kijamii

"Mashambulizi huko Ghouta mashariki yanaonesha wazi kwamba Urusi haijali kabisa kuhusu mzozo wa kibinadamu ambao unaendelea kuongezeka," alisema Nauert, "raia bado wanashambuliwa kwa mabomu katika miji iliyoko nje ya Damascus," aliongeza msemaji huyo.

Schweiz russischer Außenminister Sergej Lawrow
auf der Sitzung des UN-Menschenrechtsrates in Genf (Getty Images/AFP/F. Coffrini
)

Sergey Lavrov, Waziri wa mambo ya nje wa Urusi

Ubalozi wa Urusi mjini Washington uliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook kwamba hii ingekuwa fursa nzuri ya kuzungumzia masuala muhimu ya kikanda na hata ya dunia nzima si kupitia vyombo vya habari bali kwa njia ya moja kwa moja. Urusi imeituhumu Marekani kwa kusambaza habari za uongo na kutoa taarifa zisizo za uhakika kuhusiana na uwezekano wa mkutano huo.

Nao ubalozi wa Urusi ukiilaumu  Marekani katika mtandao wa kijamii wa Facebook umesema kusisitiza kwa Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani kwamba Urusi haikuitisha mkutano ni jambo linaloonesha kwamba kuna kitu fulani ambacho hakiendi sawa katika wizara hiyo.

Kwa upande wake Waziri Tillerson mbali na kuizuru Kenya, atazitembelea pia Djibouti, Nigeria na Chad.

Mwandishi: Jacob Safari/APE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com