Spika Mbazaa ndiye rais wa muda Tunisia | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 15.01.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Spika Mbazaa ndiye rais wa muda Tunisia

Baraza la Katiba nchini Tunisia lamtangaza Foued Mbazaa, ambaye ndiye Spika wa Bunge la Taifa, kama mtu anayefaa kushikilia nafasi ya urais katika kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi ndani ya kipindi cha siku 60 zijazo.

Waziri Mkuu wa Tunisia, Mohamed Ghannouchi

Waziri Mkuu wa Tunisia, Mohamed Ghannouchi

Nchini Tunisia bado hali ni tete. Mapema mchana wa leo (15 Januari 2011), chombo kikuu kinachosimamia masuala yote ya sheria na katiba nchini Tunisia, Baraza la Katiba, limetangaza kwamba, mtu anayepaswa kushika wadhifa wa urais katika kipindi hiki cha mpito ni spika wa bunge la taifa, Foued Mbazaa.

Akitoa tamko hilo kupitia televisheni ya taifa, Rais wa Baraza hilo, Fat-hi Abd Ennather, alisema hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha 57 na kuongeza kuwa uchaguzi wa rais unapaswa kuitishwa katika muda usiozidi siku 60 kuanzia sasa.

Jana Waziri Mkuu Muhammad Ghannouchi alitangaza kuwa anachukua nafasi ya urais kwa sababu Rais Zain al-Abidin Ben Ali, alikuwa hawezi kutekeleza majukumu yake ya urais. Ben Ali anaripotiwa kuikimbia nchi na kukimbilia Saudi Arabia kufuatia maandamano ya umma.

Hadi sasa, Ghannouchi, hajasema chochote kuhusiana na tangazo hili la Baraza la Katiba na hivyo bado haiko wazi nani hasa atakayeshikilia uongozi wa nchi.

Rais wa Tunisia aliyekimbilia uhamishoni nchini Saudi Arabia, Zain al-Abidin Ben Ali

Rais wa Tunisia aliyekimbilia uhamishoni nchini Saudi Arabia, Zain al-Abidin Ben Ali

Lakini kuna hofu kuwa ikiwa Ghannouchi hataheshimu uamuzi wa Baraza la Katiba, kuna uwezekano wa kukabiliwa na hatima ile ile ya Ben Ali, kwani tangu hapo jana alipotangaza kushikilia wadhifa huo, mamia ya waandamanaji wameendelea kumiminika mitaani wakimtaka awachie madaraka na ampishe Spika Mbazaa kama yalivyo matakwa ya katiba.

Awali akizungumza mjini Paris Ufaransa ambako kuna jamii kubwa ya Watunisia, kiongozi wa Vuguvugu la Wazalendo linalojulikana kama Bysra, lenye makao makuu yake mjini humo, Salim bin Hassan, amekiambia kituo cha redio cha Europe One, na hapa namnukuu:

"Ghannouchi amekuwa waziri mkuu kwa miaka kumi mfululizo. Kama kweli alikuwa na nia njema, basi angeliyafanya haya tangu zamani."

Maandamano ya Umma yaliyomng'oa madarakani kiongozi wa Tunisia, Zain al-Abidin Ben Ali

Maandamano ya Umma yaliyomng'oa madarakani kiongozi wa Tunisia, Zain al-Abidin Ben Ali

Katika ulimwengu wakiarabu Serikali ya Qatar imesema kwamba itaheshimu uamuzi wa Watunisia kufuatia kuondoshwa madarakani kwa Ben Ali kwa maandamano ya umma. Taarifa iliyotolewa jana na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, inasema kwamba Qatar itaendeleza ushirikiano wake na watu wa Tunisia kwa maslahi ya pande zote mbili, huku ikiahidi kuwa serikali inafuatilia kwa makini mambo yanavyoendelea nchini Tunisia.

Kauli kama hii pia imetolewa leo na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Arab Leaguze imewataka Watunisia kuwa watulivu na wamoja, huku taasisi husika za nchi hiyo zikiandaa taratibu za kuumaliza mgogoro uliopo kwa njia za amani.

Nje ya Ulimwengu wa Kiarabu, miito imekuwa ikitolewa kwa uongozi utakaochukuwa madaraka nchini Tunisia kusimamia demokrasia na haki za binaadamu. Hapa nchini Ujerumani,Kansela Angela Merkel ameutaka uongozi huo kuitumia fursa hii ya kihistoria kuanza mwanzo mpya.

Huko Ufaransa, nchi ambayo ilikuwa na himaya yake Tunisia, Rais Nikolas Sarkuzy ameitisha kikao maalum na baraza lake la mawaziri kuijadili hali ya mambo ya Tunisia.Jana Ufaransa ilikataa Ben Ali alipokua akielekea mjini Paris kwa hofu ya kuwakera Watunisia wengi wanaoishi nchini humo na ambao ni wapinzani wa dikteta huyo.

Wakati huo huo, viwanja vya ndege na anga ya Tunisia imefunguliwa tena, kuwaruhusu wageni mbalimbali, wengi wao wakiwa watalii wa nchi za Magharibi, kuondoka nchini humo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/DPA/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

 • Tarehe 15.01.2011
 • Mwandishi Mohammed Khelef
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/zy1t
 • Tarehe 15.01.2011
 • Mwandishi Mohammed Khelef
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/zy1t

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com