1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Silaha zanyamaza Aleppo kwa saa 48

5 Mei 2016

Jeshi la Syria limekubali kuheshimu usitishaji mapigano wa siku mbili katika mji uliyoharibiwa vibaya wa Aleppo, kufuatia shinikizo kutoka kwa Urusi na Marekani.

https://p.dw.com/p/1IiYJ
Mji wa Aleppo umebaki magofu kwa sehemu kubwa kufuatia miaka mitano ya mapigano.
Mji wa Aleppo umebaki magofu kwa sehemu kubwa kufuatia miaka mitano ya mapigano.Picha: Reuters/A. Ismail

Hatua hiyo imekuja baada ya Washington kutangaza kuwa Marekani na Urusi zimekubaliana kuzishinikiza pande hasimu kurefusha usitishaji huo usiothabiti. "Uongozi wa juu wa jeshi la Syria unatangaza kipindi cha utulivu mjini Aleppo kwa saa 48 kuanzia saa saba usiku wa kuamkia Alhamisi," ilitanza televisheni ya taifa ya Syria.

Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema wasimamizi wake wa mapatano ya kusitisha mapigano walikubaliana na wenzao wa Marekani kusimamia mapatano hayo hadi saa sita usiku wa Mei 4. Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry alisema mapatano mapya ya Aleppo yalianza tayari usiku wa manane siku ya Jumanne, na kwamba vurugu tayari zilikuwa zimeshapungua.

Lakini waandishi wa habari walioko ndani ya Syria wameripoti kuendelea kwa mapigano makali ndani ya mji huo na maeneo yalioko magahribi mwa Damascus ambayo yalikuwa tayari chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry akizungumza na waandishi wa habari mjini Gevena, sambamba na mjumbe wa UN Staffan de Mistura.
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry akizungumza na waandishi wa habari mjini Gevena, sambamba na mjumbe wa UN Staffan de Mistura.Picha: Reuters/D.Balibouse

Ujumbe kwa serikali na wapinzani

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Mark toner alisema kumekuwepo na kupungua kwa vurugu kwa ujumla, ingawa bado kulikuwa na ripoti za kuendelea kwa mapigano katika baadhi ya maeneo. Alizitaka pande mbili kuchukuwa hatua zinazostahiki.

"Kwa hivyo ili kuendeleza usitishaji huu wa uhasama, ni juu yao na huo ndiyo ujumbe wetu kwao: Kwamba hawawezi kushirikiana na makundi ya ndani ambayo siyo sehemu ya mapatano haya," alisema Toner katika mkutano na waandishi wa habari mjini Washingotn.

Urusi na Marekani ndiyo walikuwa wafadhili wa pamoja wa mapatano ya usitishaji mapigano ya Fabruari 27, ambayo yalikuwa yameanza kusambaratika, hasa katika mkoa wa Aleppo. Mji huo umegawika kati ya vikosi vya Bashar al-Assad, vikosi vya upinzani vinyoungwa mkono na mataifa ya Magharibi na waasi wa kundi la Jabhatu al-Nusra ambao si sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

Wiki iliyopita Urusi ilikubaliana na usitishaji mapigano katika mkoa wa Latakia na kiunga cha mji wa Damascus, lakini ikasema Assad anapaswa kuruhusiwa kupambana na iliowaita magaidi wa Jabhatu al-Nusra mjini Aleppo. Mapigano makali yaliendelea mjini humo, na hospitali katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali na waasi zilishambuliwa, mashambulizi ambayo wanadiplomasia wawili wa Umoja wa Mataifa walionya siku ya Jumatano kwamba ni uhalifu wa kivita.

Katuni ya mchoraji Sergey Elkin ikionesha wahanga wa kiraia wa mashambulizi mjini Aleppo.
Katuni ya mchoraji Sergey Elkin ikionesha wahanga wa kiraia wa mashambulizi mjini Aleppo.Picha: Sergey Elkin

Wahusika wawajibishwe

Afisa wa juu wa masuala ya kisiasa wa Umoja wa Mataifa Jeffrey Feltman, na mkuu wake wa shughuli za misaada Stephen O'Brian, waliliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba wanaohusika na mashambulizi dhidi ya hospitali na mizingiro ya kuwatesa watu katika maeneo yanayoshikiwa na waasi mjini Aleppo wanapaswa kushtakiwa kwa uhalifu wa kivita.

Vita vya Syria vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 270,000 mpaka sasa na mamilioni wameyapa kisogo makaazi yao. Ufaransa ilitangaza jana kuwa itaitisha mkutano na mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Qatar, Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu, Jumatatu ijayo, kujadili namna ya kusukuma mbele majadiliano yaliokwama.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe, dpae

Mhariri: Caro Robi