1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la UNHCR lazungumzia wasiwasi wake juu ya ongezeko la wakimbizi duniani

Saumu Mwasimba17 Juni 2008

Ripoti ya mwaka 2007 ya shirika hilo inasema hali inazidi kutisha

https://p.dw.com/p/ELh7
Wakimbizi wa Iraq nchini Syria wakisubiri usaidizi nje ya shirika la UNHCRPicha: AP

Idadi ya wakimbizi duniani na watu walioachwa bila makaazi ndani ya nchi zao imefikia watu millioni 67 kufikia mwaka uliopita. Shirika la kimataifa la kuwahudumia wakimbizi la UNHCR limetoa ripoti yake ambayo inasema idadi hiyo kubwa imetokana na kuongezeka mizozo katika maeneo mbali mbali ya dunia. Ripoti hiyo pia inasema wakimbizi wengi wanatokea katika nchi za Afghanistan na Iraq.

Kamishna mkuu wa Umoja wa mataifa anayehusika na masuala ya wakimbizi Antonio Guterres akitangaza ripoti hiyo amesema idadi ya wakimbizi imeongezeka katika kipindi cha miaka miwili na jambo hilo linatia wasiwasi mkubwa kwa sababu hii inamaanisha ulimwengu sasa unakabiliwa na changamoto mbali mbali ambazo huenda zikasababisha kutishia zaidi ongezeko la watu wasio na makaazi katika miaka ijayo.Idadi ya wakimbizi ilikuwa imepungua kati ya mwaka 2001 hadi mwaka 2005 lakini hali ikabadilika baada ya hapo.

Kamishna huyo amesema hali inaweza kuwa mbaya zaidi miaka ijayo kutokana na kuenea mizozo,utawala mbaya,kuharibika kwa hali ya mazingira kunakotokana na mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na mfumko wa bei za vyakula.

Ripoti ya shirika la UNHCR imesema kuwa idadi ya wakimbizi na watu walioachwa bila makaazi ndani ya nchi zao ambao wanashughulikiwa na shirika hilo imepanda kwa idadi ya watu millioni 2 na nusu mwaka jana pekee na kuifanya idadi hiyo kufikia watu millioni 25.1 kufikia mwishoni mwa mwaka 2007.

Aidha ripoti hiyo imefahamisha kwamba ingekuwa wakimbizi walioko chini ya shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia wakimbizi wa Palestina la UNRWA pamoja na watu wengine walioachwa bila makaazi wangeorodheshwa katika idadi ya wakimbizi wanaohudumiwa na UNHCR basi idadi jumla ya watu wasiokuwa na pakuishi ingefikia kiasi cha watu millioni 67 mwaka jana.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya shirika la UNHCR nchi zinazoongoza kwa wakimbizi ni Afghanistan na Iraq ambapo kuna wakimbizi millioni 3.1 kutoka Afghanistan hiyo ikiwa ni asilimia 27 ya idadi ya wakimbizi wote duniani katika mwaka 2007.Iraq inafuatia katika kundi hilo ikiwa na jumla ya wakimbizi millioni 2.3 wengi wakiwa wamekimbilia Jordan na Syria.

Aidha nchini Iraq idadi ya wakimbizi wa ndani imepanda kutoka watu millioni 1.8 mwanzoni mwa mwaka jana hadi kufikia kiasi cha millioni 2.4 kufikia mwishoni mwa mwaka jana. Hali hiyo imetokana na kuongezeka kwa mzozo na mgawanyiko wa kimadhehebu pamoja na ukosefu wa suluhisho la kisiasa kuhusu mzozo wa nchi hiyo.

Kwa upande mwingine shirika la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa mataifa UNHCR linasema mapigano na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika jamhuri ya Afrika ya kati, Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo,Somalia na Sudan pia yamechangia ongezeko la wakimbizi mwaka 2007 huku wengi wao pia wakirudishwa katika nchi za Sudan,Liberia na Burundi katika mwaka huo.

Halikadhalika shirika hilo limezitaja miongoni mwa nchi nyingine,Pakistan,Iran,Ujerumani,Tanzania,Uingereza,Chad na Marekani kuwa nchi zilizokaribisha wakimbizi wengi.