1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz: Nina sababu za kutoipa Ukraine makombora ya Taurus

13 Machi 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kwa mara nyengine tena ameelezea upinzani wake wa kupeleka makombora ya masafa marefu aina ya Taurus nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4dTho
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kiongozi huyo amesema suala la kupeleka silaha Ukraine ni "mstari ambao asingependelea kuuvuka" licha ya shinikizo kutoka kwa kambi ya upinzani na hata baadhi ya wabunge kutoka muungano tawala unaojumuisha chama cha Kijani, SPD na FDP. 

Scholz amekabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa kambi ya upinzani kwa kukataa kuipa Ukraine makombora ya Taurus, licha ya ombi la Kiev.

Baadhi ya wabunge katika muungano wake tawala, unaojumuisha chama cha kijani, SPD na FDP, pia wanaunga mkono kupelekwa kwa silaha nchini Ukraine.

Kiongozi huyo hata hivyo ameshikilia msimamo wake wakati wa mjadala katika bunge la Ujerumani, Bundestag, akielezea hofu yake kwamba kwa kuipa Ukraine silaha kutaisukuma Ujerumani kwenye mzozo wa moja kwa moja na Urusi.

Soma pia: Ukraine yaihimiza Ujerumani kuipatia makombora ya Taurus

Scholz ameendelea kueleza kuwa, kuipa Ukraine makombora aina ya Taurus kutamaanisha pia kulihusisha jeshi la Ujerumani katika mzozo huo.

Akitetea hoja yake mbele ya bunge, Scholz amesema,

"Huo ni mstari ambao sitaki kuuvuka kama Kansela. Na ndio maana nimechukua uamuzi huu na pia nimeleeza msimamo wangu kuhusu suala hili kama munavyojua. Naamini ni muhimu kwetu kuhakikisha kwamba askari wa Ujerumani hawahusiki katika usambazaji wa silaha."

Kambi ya upinzani yamshinikiza Scholz

Wanajeshi wa Ujerumani
Wanajeshi wa Ujerumani Picha: Marijan Murat/dpa/picture alliance

Hata hivyo, wanasiasa wa upinzani, muungano wa kihafidhina wa CDU na CSU wakiwemo pia baadhi ya wabunge wa muungano tawala wametilia mashaka hoja hiyo ya Scholz.

Mnamo mwezi Februari, Scholz alitoa sababu za kina za kwa nini anapinga wazo la kupeleka makombora hayo Ukraine.

Serikali ya shirikisho pamoja na bunge la Ujerumani, wanaendelea kufanya kila liwezekano kuhakikisha kwamba Ukraine inaweza kujilinda dhidi ya uvamizi wa Urusi. Hili ni muhimu, na Ujerumani iko katika mstari wa mbele.

Soma pia: Scholz aahidi uchunguzi wa haraka kuhusu udukuzi wa Urusi

Kambi ya upinzani inapanga kuandaa kura kesho Alhamisi juu ya azimio la kuishurutisha serikali ya Ujerumani ipeleke Ukraine makombora aina ya Taurus.

Makombora ya Taurus yana uwezo wa kuruka angani umbali wa hadi kilomita 500 na iwapo yatatumika, yatawapa wanajeshi wa Ukraine uwezo wa kulenga shabaha hata wakiwa mbali katika uwanja wa vita.

Scholz pia amepuzilia mbali hoja kwamba hana imani na Ukraine, na badala yake akisema kuwa Ujerumani, ni moja kati ya mataifa yaliyoipa Ukraine silaha nyingi zaidi kuliko nchi yoyote ile ya Ulaya.