Sarrazin ajiuzulu uanachama wa bodi ya benki kuu ya Ujerumani | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.09.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Sarrazin ajiuzulu uanachama wa bodi ya benki kuu ya Ujerumani

Mwanachama wa bodi ya uongozi ya Benki Kuu ya Ujerumani, Thilo Sarrazin, amejiuzulu baada ya kukabiliwa na shinikizo kutoka kwa wanasiasa kufuatia matamshi yake kuhusu wahamiaji yaliyozusha ghadhabu

Thilo Sarrazin

Thilo Sarrazin

Benki Kuu ya Ujerumani, Bundesbank, imesema Thilo Sarrazin, mwenye umri wa miaka 65, aliyewatuhumu Waturuki na Waarabu kwa kuitumia vibaya nchi hii na mfumo wake wa kijamii, kukataa kujumuika na jamii ya Wajerumani na kuteremsha kiwango cha wastani cha werevu humu nchini, ataacha kazi rasmi mwisho wa mwezi huu wa Septemba. Katika taarifa yake fupi, benki hiyo imesema Sarrazin amemtaka rais wa Ujerumani, Christian Wullf, amwachishe kazi na Sarrazin mwenyewe alithibitisha ameacha kazi wakati wa zoezi la kukisoma kitabu chake kwa umma hapo jana (09.09.2010 ) huko mjini Potsdam, karibu na mji mkuu, Berlin.

"Haikuwa rahisi kwangu. Nimetafakari na hatimaye nikaona nina mada muhimu ninayoweza kuijadili pamoja na viongozi wa kisiasa wa Ujerumani na asilimia 70 ya Wajerumani wanaopinga mawazo yangu. Hiyo ndiyo hali ilivyokuwa wiki zilizopita na nimesema hakuna awezaye kuihimili hali hii kwa muda mrefu."

Sarrazin tayari alikuwa amevuliwa baadhi ya majukumu yake katika Benki Kuu kwa kauli alizozitoa mwaka jana kuhusu wahamiaji, lakini kwa kuwa benki hiyo haina uhuru mpana na mamlaka makubwa, ilikuwa vigumu kwa benki kuu kumuondoa mwanachama huyo wa bodi ya benki hiyo. Lakini alipochapisha matamshi makali zaidi katika kitabu chake kipya alichokiita: Ujerumani yajiangamiza yenyewe" na kauli alizozitoa kabla kitabu hicho kuchapishwa, kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, na rais wa nchi hii, Christian Wullf, walitoa ishara nzito kwamba Sarrazin angejiuzulu.

Sarrazin anahoji katika kitabu chake kwamba Waislamu wanaihujumu jamii ya Wajerumani na wanatishia kuubadili utamaduni wake kwa kasi kubwa ya uzazi. Aliwakasirisha watu wengi kwa kusema Wayahudi wote wana chembechembe maalumu ya urithi.

Benki kuu ya Ujerumani ilipiga kura wiki iliyopita kumuondoa Sarrazin, uamuzi ambao ulihitaji idhini ya rais. "Nimeona ni hatari mno katika mazingira ya sasa kukabiliana na tabaka la wanasiasa na vyombo vya habari. Hiyo ingekuwa ni kazi bure na haingekuwa na maana," alisema Sarrazin wakati wa kukisoma kitabu chake, muda mfupi baada ya taarifa ya kujiuzulu kwake. "Ni mkakati wa kujiweka kando, na sasa nitazishughulikia mada ambazo ni muhimu kwangu", aliongeza kusema bwana Sarrazin.

Sarrazin awali aliapa kupambana na juhudi za kumuondoa, hivyo kuzusha uwezekano wa kutokea kesi kubwa ya mivutano mahakamani ambayo ingezua maswali kama kweli kansela Merkel na rais Wullf, walipitisha uamuzi unaofaa. Bi Merkel na mawaziri na vyama vikubwa vya kisiasa vilimkosoa Sarrazin, ambaye ni mwanachama wa chama cha Social Democratic, SPD, na waziri wa fedha wa zamani wa mji wa Berlin.

Chama cha SPD kimeanzisha mchakato wa kumfukuza chamani Sarrazin, ingawa matokeo ya kura ya maoni iliyofanywa hivi karibuni yanaonyesha kuwa hatua hiyo haitaungwa mkono na umma na wafuasi wa chama cha SPD wanaoamini chama hicho kinatakiwa kutumia muda wake kuyashughulikia masuala muhimu zaidi.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE

Mhariri: Othman Miraji

 • Tarehe 10.09.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/P8uV
 • Tarehe 10.09.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/P8uV
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com