Rais wa Yemen yutayari kujiuzulu kwa masharti
25 Aprili 2011Kimsingi, pendekezo hilo la GCC limekubaliwa pia na vuguvugu la upinzani, lakini hiyo jana maandamano yalifanywa upya katika mji mkuu, Sanaa. Mapambano ya umwagaji damu kati ya Rais wa Yemen, Ali Abdullah Saleh, na vuguvugu la upinzani linaendelea kwa takriban miezi miwili nchini humo, lakini kuna uwezekano wa mapigano hayo kumalizika. Kwani kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali, Rais Saleh, kimsingi, amekubali pendekezo lililotolewa na nchi za Ghuba. Naibu waziri wa habari, Abdu al Janadi, alipozungumza na Al Jazeera, alieleza hivi:
"Rais na chama tawala wanaunga mkono vifungu vyote vya pendekezo hilo. Na hilo litatekelezwa kuambatana na katiba ya Yemen."
Kipengele muhimu katika pendekezo hilo ni kuwa Rais Saleh na wafanya kazi wa zamani na wa hivi sasa serikalini watajiuzulu, lakini badala yake wasichukuliwe hatua ya kufikishwa mahakamani. Mwanzoni, sharti hilo lilipingwa vikali na wapinzani, lakini yaonekana kuwa msimamo huo umebadilika baada ya hadi waandamanaji 130 kuuawa katika miji mbali mbali nchini humo.
Rais Saleh angátuke moja kwa moja
Duru za upinzani zimesema kuwa pendekezo la wapatanishi kutoka nchi za Ghuba, GCC, linaweza kukubaliwa, lakini kwa masharti. Msemaji wa vuguvugu la upinzani, Mohammed Qahtan, amesema, na hapa ninamnukuu "Kwanza kabisa Rais Saleh ajiuzulu ili serikali mpya ipate kuundwa, ikiwa na rais mpya." mwisho wa kumnukuu. Kwa upande mwingine, msemaji wa vuguvugu la vijana, Khaled al Ansi, amelipinga kabisa pendekezo la GCC. Amesema, wao wanapinga mpango wo wote ule ambao hautopelekea kungoka madarakani hapo hapo Rais Saleh, wanae na jamaa zake.
Kwa maneno mengine, Saleh asiondoke madarakani baada ya siku 30, bali ang'atuke moja kwa moja. Na wapinzani wameonya kuwa tangazo la Rais Saleh kuwa tayari kuondoka madarakani haimaanishi kuwa maandamano ya upinzani yatamalizika. Maelfu ya watu wamekuwa wakimiminika barabarani kudai mageuzi katika nchi iliyo masikini kabisa katika ulimwengu wa Kiarabu.
Mwandishi: Steffe,Peter/P.Martin
Mhariri:Miraji Othman